Mwenyekiti Wa Cuf Taifa-Prof Ibrahim Lipumba |
Tanzania inakabiliwa na changamoto mbili kubwa kujenga uchumi wenye manufaa
kwa wananchi wote na kujenga demokrasia ya kweli itakayohakikisha nchi
inaendeshwa kwa kufuata sheria zinazotoa haki sawa kwa wananchi wote. Nchi yetu
inahitaji uongozi ambao unaona siasa ni utumishi wa dhati na uliotukuka kwa
umma uliozindukana na siyo nyenzo ya kukimbilia na kupigania vyeo, fursa na
nguvu ya ushawishi kwa malengo ya kujilimbikizia uwezo wa maamuzi na wa utajiri
binafsi usiohojiwa.
Uongozi wa nchi
unawajibika kubuni sera kwa kuzingatia uhalisia na hali ya uchumi wa nchi,
fursa zilizopo na vikwazo vinavyoikabili nchi katika kukuza uchumi wake. Baada ya kubuni sera uongozi unawajibika
kuzieleza sera hizo kwa wananchi na kuwahamasisha waziunge mkono na waelewe
kuwa ili kujinasua toka dimbwi la umaskini wanawajibika kuchapa kazi kwa bidii,
kuweka akiba, kuwa wajasiriamali wabunifu na kukubali kasi ya mabadiliko inayoendana
na ukuaji wa uchumi. Uongozi utafanikiwa
ikiwa sera zake zinaaminika na zinatekelezeka, na matunda ya sera hizo yanaleta
neema kwa wananchi wote.
Uongozi makini
utakaoweza kuchochea maendeleo ya muda mrefu unapaswa kuwa na subira, uwe na
dira na mipango ya muda mrefu na ujikite katika lengo la kukuza uchumi utakaoongeza
ajira na kuleta neema kwa wananchi wote.
Katika zama za
demokrasia ya vyama vingi ni muhimu kwa wadau vikiwemo Vyama Vya Siasa
kukubaliana alau kwa ujumla dira ya maendeleo ya nchi na kila chama
kitakachoingia madarakani kitekeleze sera zitakazokuza uchumi unaoleta tija na
neema kwa wananchi wote. Watendaji
wazuri wa serikali walio waadilifu na uwezo mzuri wanasaidia sana katika
kushauri wanasiasa walioko madarakani sera zinazotekelezeka na zenye manufaa
kwa wananchi.
Baada ya muda
mrefu bila ya kuwa na maendeleo ya kutosha, urekebishaji wa sera ni jambo
muhimu. Hata hivyo kurekebisha siyo
lengo la mwisho. Lengo ni matunda
yanayotokana na kurekebisha sera hizo.
Nchi zilizofanikiwa kupata maendeleo ya muda mrefu, zimetegemea na kuutumia
mfumo wa uchumi wa soko. Kuutegemea na kuutumia Uchumi wa soko hakumaanishi
kuwa soko huria pekee ndiyo chanzo cha kukua uchumi. Serikali madhubuti zilijenga mazingira ya
kuwezesha sekta binafsi kutumia uchumi wa soko kuongeza kasi ya kukua kwa
uchumi.
Uchumi wa soko
ulioendelea unajikita katika historia na asasi muhimu katika jamii husika. Asasi hizo ni pamoja na kuwepo haki na uhuru
wa kumiliki mali, mikataba, hususan katika shughuli za biashara na uchumi
huheshimiwa na inapovunjwa kuna mamlaka zinazosuluhisha na kuhakikisha kuwa
mikataba inasuluhishwa kwa gharama za wastani wa wale wenye haki wanapata fidia
na hawadhulumiwi. Taarifa kuhusu masoko
zinawafikia wadau wote.
Katika hatua za
awali za kutafuta na kuleta maendeleo, serikali makini zinafanya majaribio ya
sera zake katika maeneo machache kabla ya utekelezaji katika nchi nzima. Moja ya mapungufu makubwa katika kubuni na
kutekeleza sera katika Tanzania ni ukosefu wa kufanya majaribio na kupima
mafanikio yake kabla ya kutekeleza nchi nzima.
Matatizo haya yalikuwa makubwa wakati wa sera za ujamaa. Kwa mfano sera za kuhamia vijiji vya kudumu
kuwa ni amri mwaka 1974, Sera ya elimu kwa msingi kwa wote katika mwaka mmoja,
sera ya kufunga maduka binafsi na kadhalika zilitekelezwa kabla ya kufanyiwa
majaribio. Hivi karibuni sera ya
kuanzisha shule za sekondari za kata haikufanyiwa majaribio kabla ya
kuitekeleza nchi nzima. Ni muhimu katika
utekelezaji wa sera, serikali ikafanya majaribio (pilot projects) na kujifunza
katika majaribio hayo kabla ya kuitekeleza sera katika eneo kubwa.
Kubuni sera nzuri
ni mwanzo tu. Sera zinazopaswa kuwekwa
katika mipango ya utekelezaji na kutekelezwa kwa umakini wa hali ya juu. Utekelezaji na matokeo yake yafanyiwe
tathmini ya mara kwa mara ili makosa yangunduliwe na kurekebishwa. Kujenga utumishi bora, wenye ujuzi, usiyoyumbishwa
na rushwa ndani ya serikali ni changamoto muhimu. Utumishi mzuri ulio imara haujengwi siku
moja. Viongozi wa kisiasa ni wepesi
kuhujumu kuwepo kwa utendaji mzuri serikalini ikiwa watawatumia watendaji wa
serikali kufanikisha malengo ya kisiasa ya kubaki madarakani kwa kuiba kura
wakati wa uchaguzi au utekelezaji wa miradi ya muda mfupi kwa malengo ya
kuvutia wapiga kura. Serikali
inawajibika kuvutia watumishi wenye uwezo na ari ya kufanya kazi. Ni muhimu mishahara ya wafanyakazi serikalini
iwe inavutia lakini utunishi serikalini uzingatie uwezo na siyo mtoto wa nani
au unamjua nani!
Serikali yenyewe
siyo inayoleta ukuaji wa uchumi. Kazi
hiyo kwa sehemu kubwa ni ya sekta binafsi yenye wajasiriamali wazuri
wanaowekeza na kutumia teknolojia bora na kuzitumia fursa zilizopo katika
uchumi wa soko. Hata hivyo serikali
adilifu, yenye sera nzuri zinazojulikana na kutekelezwa kwa makini, isiyoyumba
ni muhimu sana kwa maendeleo ya muda mrefu.
Kazi muhimu ya serikali ni pamoja na kuhakikisha kuna utulivu katika
uchumi mpana kwa maana ya kutokuwepo mfumko wa bei kuwepo kwa akiba ya kutosha
na fedha za kigeni kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nchi
za nje, matumizi ya serikali na sekta ya umma yalingane na mapato ya serikali,
na serikali iwekeze katika miundo mbinu muhimu.
Nchi
zilizofanikiwa kukuza uchumi kwa muda mrefu zinafanya hivyo kwa kuwa na sera
zinazoenda na mabadiliko ya uchumi ndani na nje ya nchi. Mikakati ya kukuza uchumi ibadilike kufuatana
na mabadiliko ya mfumo wa uchumi. Siasa
za ndani ya nchi pia zinastahiki kubadilika na kwenda na wakati. Kukua kwa uchumi kutaongeza idadi ya watu
wenye kipato cha kati na watu wenye elimu ambao watadai kushiriki katika
maamuzi ya sera zinazowagusa na kuwa na sauti nchi yao.
Sera za
kurekebisha uchumi ili kuchochea ukuaji wake na maeneo ya kuwekeza katika
miundo mbinu ni mengi na yanazidi uwezo wa mapato ya serikali. Mkakati wa
kukuza uchumi lazima uweke vipaumbele vya maeneo ambayo serikali
itayashughulikia mwanzo.
Sera za kukuza
uchumi endelevu zinajenga, mazingira mazuri ya uwekezaji mkubwa wa vitega
uchumi, ongezeko la ajira, ushindani wa kibiashara, wepesi wa raslimali
kutumiwa kwa shughuli mbadala (mobility of resources) hifadhi ya jamii na
wananchi wote kufaidi matunda ya kukua kwa uchumi.
Hakuna nchi
iliyofanikiwa kukuza uchumi kwa kasi ya juu kwa muda mrefu bila serikali
kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika miundo mbinu – barabara, nishati, reli,
bandari na mawasiliano, elimu na afya.
Uwekezaji wa serikali katika
sekta ya miundo mbinu, elimu na afya unajenga msingi imara unaovutia sekta
binafsi kuwekeza katika shughuli za uzalishaji na biashara. Uwekezaji wa sekta ya umma katika maeneo hayo
unatengeneza njia yakuwezesha viwanda na makampuni mapya kuanzishwa na kuongeza
faida ya shughuli zote za kibiashara zinazofaidika kwa kuwepo wafanyakazi wenye
afya njema na walioelimika, kuwepo kwa barabara nzuri zinazopitika wakati wote,
na kuwepo kwa umeme wa uhakika.
Nchini Tanzania,
uwekezaji katika miundombinu umekuwa mdogo na hutegemea fedha za misaada toka
nje. Ukarabati wa miundo mbinu
haufanyiki ipasavyo. Barabara inajengwa
inatumiwa mpaka inaharibika kabisa. Ili
ikarabatiwe tunaomba msaada kwa wafadhili waijenge upya. Mifano ni Mingi. Barabara ya Mandera, Barabara ya Dar es
Salaam - Morogoro, Barabara ya Chalinze – Segera – Tanga, n.k
Ukuaji wa uchumi
unaambatana na mabadiliko ya mfumo wa uchumi kutoka kutegemea sana kilimo na
kuelekea kwenye ongezeko la ajira viwandani, kutoka nguvu kazi inayoishi
vijijini kuelekea nguvu kazi inayoishi mijini.
Mabadiliko ya mfumo wa uchumi husababishwa na ushindani wa soko. Serikali zenye malengo ya kukuza uchumi
endelevu zinawajibika kujenga ushindani katika masoko yote kuruhusu makampuni
mapya yenye tija kuanza na makampuni yanayopata hasara kufilisika. Soko la ajira liwe jepesi kuruhusu makampuni
mapya kuajiri wafanya kazi na makampuni yanayopata hasara kupunguza
wafanyakazi. Sheria za kazi zijikite
katika kurahisisha uanzishwaji wa ajira. Ni muhimu sana kuwa na utaratibu wa
hifadhi za jamii kwa wafanya kazi wanaopoteza ajira ili kupunguza makali na
kuwepo kwa soko la ajira linalonyumbulika.
Wanaopoteza ajira wapate kipato cha kuwawezesha kuishi wakati wakitafuta
ajira mpya.
Elimu bora
inayowapa wafanyakazi uwezo wa kujifunza na kupata ujuzi mpya ni kinga muhimu
ya kutopoteza ajira kwa muda mrefu. Vile
vile zinaongeza kasi ya ajira mpya kuanzishwa kwa wingi na kwa hiyo kuhakikisha
nguvu kazi inaajiriwa.
Mkakati wa kukuza
uchumi lazima uzingatie kuwa toafuati kubwa za vipato vya wananchi kati ya
maskini na matajiri havisaidii ukuaji wa uchumi na vinaongeza upinzani dhidi ya
sera za kurekebisha uchumi. Ni wazi uchumi
unapoanza kukua tofauti za vipato zinaongezeka.
Sera zijikite katika kutoa fursa ya kupata ajira kwa wananchi wengi
iwezekanavyo na misaada maalum itolewe
kwa watu maskini waweze kujinasua toka dimbwi la umaskini. Vurugu za kisasa kupinga wachache kuwa
matajiri wakati wengi ni maskini zitaathiri mikakati ya kukuza uchumi.
Kigezo muhimu cha
kupima kama sera zinatoa fursa sawa kwa wote ni fursa za wasichana kupata elimu
iliyo bora. Wanawake walipata elimu,
wanakuwa na watoto wachache wenye afya bora ambao wanawazaa wakati maungo yao
yamekua. Kina mama wenye elimu
wanasisitiza na kuhakikisha kuwa watoto wao nao wanapata elimu. Kuwaelimisha wasichana na kuwapa fursa ya
kupata ajira ni nyenzo madhubuti ya kuutokomeza umaskini.
Nchi zilizofanikiwa
kukuza uchumi kwa kasi zilitumia vizuri fursa zilizopo katika soko la dunia na
kuongeza uuzaji wa bidhaa zao za viwandani katika soko hilo. Sera za kuongeza uzalishaji wa bidhaa za
viwanda hazikutegemea utaratibu wa soko huria tu. Serikali zilijaribu sera mbali mbali za kutoa
motisha wa kuongeza uzalishaji viwandani na kuuza bidhaa za viwandani nchi za
nje. Sera za kukuza sekta ya viwandani
ni pamoja na ruzuku katika uzalishaji wa bidhaa mpya, uwekezaji wa miundo mbinu
mizuri katika maeneo maalum ya kuanzisha viwanda vipya, misamaha ya kodi. Ni muhimu motisha maalum kwenye viwanda
vitakavyouza bidhaa nchi za nje zisiwe za kudumu. Ikiwa sera hazikufanikiwa kuongeza kasi ya
kukua kwa sekta ya viwanda na uuzaji wa bidhaa nchi za nje, sera hizo
zibadilishwe.
Utandawazi
umefanya uchumi wa dunia hivi sasa kuwa wazi zaidi na kuingiliana sana katika
biashara, uwekezaji, huduma za fedha na teknolojia. Nchi zilizokua kwa kasi ya juu zimefanya
hivyo kwa kuingiza maarifa, teknolojia na ujuzi kutoka nchi za nje. Njia moja ya kupata maarifa na teknolojia kutoka
nje ni kupitia uwekezaji unaofanywa na makampuni ya nje. Njia nyingine ni kupata elimu, maarifa na
teknolojia iliyopo katika nchi zilizoendelea na kuitumia kwa kuzingatia uhalisi
na mazingira ya nchi yako.
Uchumi wa dunia
unatoa fursa ya soko kubwa kwa nchi zinazoendelea. Kinadharia, Tanzania
inaweza kuuza bidhaa zote za viwandani
inazozalisha kwa bei ya soko la dunia. Suala la msingi ni je kuuza nchi za nje
ndiyo njia pekee ya kukuza uchumi au tunaweza kukuza uchumi kwa kutegemea soko
la ndani ya nchi?
Mikakati ya
kuendeleza uchumi kwa kutumia soko la ndani inaweza kufanikiwa kwa muda mfupi
hasa kwa nchi kubwa zenye watu wengi.
Zaidi ya hapo matatizo ya kutetereka uchumi yanaweza kutokea ikiwa nchi
itafungua mipaka yake ghafla kwa bidhaa kutoka nje. Hata hivyo mikakati ya uchumi inayotegemea
soko la ndani tu hufikia ukomo wake mapema. Soko la ndani ni dogo mno
kuendeleza ukuaji wa uchumi kwa muda mrefu na hautoi fursa ya kujikita na
kubobea katika eneo la uzalishaji ambalo nchi ina ushindani au inaweza
kujijengea ushindani mkubwa.
Ukuaji wa haraka
wa uchumi katika nchi maskini hutegemea upatikanaji wa ajira kwa nguvu kazi ya
ziada iliyomo nchini. Kwa kadri uchumi unavyokua ndivyo unavyoajiri nguvukazi
ya ziada iliyomo nchini hasa vijijini katika sekta ya kilimo na iliyoko mijini
katika sekta isiyo rasmi yenye tija ndogo.
Raslimali za nchi hasa nguvu kazi ni lazima ziwe tayari kuhama toka eneo
au sekta yenye tija ndogo kwenda kwenye eneo na sekta zenye tija kubwa ambazo
kwa kawaida huanzishwa mijini ambako ni rahisi kupata watu wengi wenye ujuzi na
huduma muhimu kwa viwanda kama vile umeme na maji. Ukuaji wa uchumi huambatana na ukuaji wa miji
na nguvu kazi kuhamia mijini. Hata hivyo ili miji iwe vitovu vya ukuaji
endelevu ya uchumi inahitaji miundombinu mizuri.
Sera za kukuza
uchumi ni lazima zizingatie kuweko na utulivu katika uchumi mpana kama vile
kuepukana na mfumko wa bei, ukosefu wa fedha za kigeni, ulimbikizaji mkubwa wa
madeni ya sekta ya umma unaotokana na nakisi katika bajeti ya serikali na
hasara za mashirika ya umma. Vile vile
mkakati wa uchumi unapaswa kutoa motisha kwa wajasiliamali, wadogo, wa kati na
wakubwa kuwekeza katika sekta mbali mbali kwa kuwahakikishia kuwa wakifanya
shughuli zao kwa ufanisi na kufanikiwa kupata faida, faida yao hiyo haitaporwa
na vyombo vya dola au majambazi. Vile
vile ni muhimu kuwa na mikakati ya hifadhi ya jamii ya kupunguza makali ya
maisha kwa watu watakao athirika na mabadiliko ya uchumi.
Kwa nchi zenye
ziada ya nguvu kazi ukomo wa kasi ya kukua kwa uchumi unategemea kasi ya
uwekezeshaji wa vitega uchumi. Uwekezaji
wa vitega uchumi hutegemea ukubwa wa akiba.
Ili uchumi ukue kwa kasi nchi inapaswa iweke akiba alau asilimia 25 – 30
ya pato la Taifa na kulimbikiza vizuri katika vitega uchumi vyenye tija
kubwa. Misaada kutoka nje haiwezi kuwa
mbadala wa juhudi za kuweka akiba za ndani ya nchi za kila kaya, sekta binafsi
na sekta ya umma ili akiba ilimbikizwe katika vitega uchumi muhimu.
Hivi sasa nchi
yetu inakabiliwa na ombwe la uongozi na tumeshindwa kutumia raslimaliwatu na
maliasili yetu kujenga uchumi unaoongeza ajira na kutokomeza umaskini. Nchi
inahitaji uongozi utakaowaunganisha Watanzania kukabiliana na changamoto
nilizozianisha katika mada hii. Watanzania tunapaswa kujiuliza bila kujali,
itikadi, udini, ukabila na umajimbo nani katika viongozi wetu wa kisiasa wana
dira na uwezo wa kuwaunganisha Watanzania kutekeleza dira ya mabadiliko
itakayojenga uchumi imara, unaongeza ajira na kutokomeza umaskini? Tukiipoteza
fursa ya kulijibu swali hili kwa vitendo mwaka 2015, tunaweza kujikuta
tunapoteza miaka mingine 50 ya uhuru wetu bila kujiletea maendeleo na wananchi
wengi kiendelea kubakia maskini wa kutupwa.
No comments:
Post a Comment