Monday, August 6, 2012

JUVICUF waionya JUVICCM na BAVICHA kutotumikia matakwa ya Mafisadi wa vyama vyao.

Naibu katibu Wa Jumuiya Ya Vijana
CUF(JUVICUF)Bwana.Thomas Malima
Jumuiya ya Vijana ya CUF-Chama Cha Wananchi (JUVICUF) inapenda kutoa mwito kwa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kufanya uchaguzi utakaozingatia matakwa ya vijana siyo ya watu Fulani. JUVICUF inatambua kuwa uchaguzi wa vijana ni changamoto katika taasisi za kisiasa kwani wanasiasa wakubwa hutambua kuwa Vijana ndio nguvukazi kubwa na wapiga kura wakubwa katika nchi yetu. Na ni vijana pia ndio wana matatizo makubwa hasa la ajira. Kwa hiyo hulazimika kuwapanga vijana katika mabaraza yao ili waingiapo madarakani waweze kuwatumia watakavyo.
Hali hii husababisha Viongozi wengi wa Mabaraza ya Vijana ya vyama vya siasa hasa UVCCM na BAVICHA kuwa watumishi wa Viongozi wa vyama vyao badala ya kuwatumikia vijana walioko katika vyama vyao. Kwa sasa viongozi wa Jumuiya za vijana wamekuwa kama vipaza sauti vya Wazee badala ya kuwa vipaza sauti vya vijana. Na hii inaanza tangu wakati wa uchaguzi wa Jumuiya za vijana za vyama vya siasa ambapo wakubwa huwa wanatumia mbinu chafu za kuvuruga chaguzi na maamuzi ya vijana wakati na baada ya chaguzi za Jumuiya za vijana nchini.
JUVICUF inaamini kuwa jukumu lake kubwa ni kuwaunganisha vijana nchini kutambua umuhimu wao, jinsi wanavyoonewa, wanavyonyanyaswa, wanavyokandamizwa na wanavyonyonywa na viongozi dhalimu watokanao na kizazi kilichopitwa na wakati lakini kinangangania kukaa madarakani kwa nguvu.
JUVICUF inatambua kuwa ukombozi wa Vijana kifikra ndio msingi wa ukombozi wa wao kiuchumi , kisiasa na kijamii. Hivyo basi, ni jukumu letu kuwashauri Vijana wenzetu nchini kujitambua na kuungana nasi kutetea maslahi ya vijana nchini bila kutumikia wakubwa. Na kimsingi hatuwezi kuufikia ukombozi wa kweli wa vijana kama bado tunaendelea kutumika kwa manufaa ya wakubwa wetu.
JUVICUF inatambua kuwa RUSHWA ni adui wa haki ya kijana. Tunatambua kuwa endapo UVCCM watairuhusu rushwa kutembea wakati huu wa uchaguzi wao hakika watawapata viongozi wabovu wasiokidhi matakwa ya vijana.
Vile vile JUVICUF inaamini kuwa kampeni chafu za kupakana matope, ni ishara ya uchanga wa Demokrasia. Tunaitambua UVCCM kama jumuiya ya vijana ya siku nyingi lakini tuasikitika kwa wagombea na wapambe wao kuanza kufanya siasa chafu za kupakana matope. JUVICUF inaamini kuwa vijana wa sasa wanapingana kwa hoja sio kwa kuchafuana. Hizi siasa za kuchafuana ni siasa za kizamani zilizotumika enzi za ukoloni na ni za wazee. Ukimuona kijana wa leo anafanya siasa za namna hiyo ujue ana walakini au anatumiwa na wazee wa zamani waliozizoea na wanataka kuzirithisha kwa vijana.
Mwisho, JUVICUF inawatakia Vijana wa CCM uchaguzi mwema wenye utulivu, amani, upendo na heshima baina ya wagombea na wanachama kwa ujumla. Kiongozi bora atapimwa kwa busara, uwezo na matendo yake kwa jamii ya wanaomchagua. Hakika Chama imara kinategemea Vijana imara.
Thomas D.C Malima
Naibu Katibu -Jumuiya ya Vijana ya CUF-Taifa (JUVICUF)

No comments:

Post a Comment