Wednesday, August 8, 2012

JUMUIYA YA VIJANA YA CUF YALAANI MAUAJI YA WANASIASA VIJANA KUKITHIRI NCHINI:

Naibu Katibu JUVICUF
Jumuiya ya Vijana ya CUF inasikitishwa na kusononeshwa na vitendo vya mauaji ya wanasiasa vijana inayoendelea hapa nchini Tanzania. Hii ni kutokana na mauaji ya kila mara ya vijana hasa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambayo yanaonekana kama mauaji ya kulipizana kisasi. Huu si ustaarabu wa kidemokrsia bali ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Ni hivi karibuni watanzania walishuhudia mauaji ya kikatiri ya kiongozi wa vijana wa CHADEMA kule Arusha mara baada ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki. Lakini pia tumeshitushwa na mauaji mengine ya kijana kiongozi wa CCM jimboni Iramba Magharibi juzi baada ya mkutano wa hadhara wa CHADEMA.
Mauaji ya namna hii huleta hofu kwa vijana kushiriki siasa za moja kwa moja kwa kuogopa kuuawa. Iwapo mauaji haya ya vijana wanasiasa hayatapatiwa ufumbuzi kuna hatari ya vijana wenye uwezo kuikimbia siasa na hatimaye Taifa likakosa viongozi bora wa sasa na baadaye.
Jumuiya ya Vijana ya CUF inaamini kuwa bila kuwa na utamaduni wa kuvumiliana  japokuwa tunatofautiana kimtazamo, itkikadi, dini na kabila zetu , kamwe hatutaifikia demokrasia ya kweli. Uvumilivu ni msingi mkuu wa Demokrasia ha hivyo ni wajibu wetu vijana kuacha kutumikia hisia na mihemko ya miili yetu na vyama vyetu na kuutanguliza Utanzania wetu na udugu wetu mbele.
Jumuiya ya Vijana ya CUF inawaomba vijana wa CCM na CHADEMA kuwa makini wakati tukiwa katika mchakato huu wa kuitafuta Demokrasia ya kweli inayojali misingi ya Haki za binadamu, utawala bora na ushindani wa hoja bila kuchukiana na kujenga uadui baina yetu kwani sote tuna nia ya kuijenga Tanzania yenye neema ambayo rasilimali zake zitawafaidisha watanzania wote.
Jumuiya ya Vijana ya CUF imesikitishwa sana na mauaji hayo ya vijana yanayofanywa na vijana wenyewe kwa wenyewe. Hii ni ishara kuwa Vijana wa CCM na CHADEMA hawajaiva kisiasa kwani wanashindwa kutofautisha Upinzani na Uadui. Na kutokana na mauaji haya ni wajibu wa watanzania kutambua kuwa CCM na CHADEMA hawana dira na sera za kuwafikisha watanzania kwenye neema bali wana nia ya kuwamaliza kwa kuwaua kikatiri.
Jumuiya ya Vijana ya CUF inawaomba watanzania wawe macho na mienendo ya vijana wa CHADEMA na CCM maana mauaji wanayoendelea kulipizana hayatakwisha leo wala kesho. Kwa hiyo wanapaswa kukigeukia chama chao kipenzi cha Wananchi –CUF ambacho ni chama cha makabwela na  wanyonge wa Tanzania.
Imetolewa na:
Thomas D.C Malima
Naibu Katibu Mkuu
 Sekretarieti ya Vijana-Taifa
CUF-Chama Cha Wananchi.

No comments:

Post a Comment