Wednesday, December 26, 2012

UCHUMI WA DUNIA UNAELEKEA WAPI IFIKAPO 2030?

Mwenyekiti Wa CUF-Prof Ibrahim H Lipumba

Tangu mwaka 1997, Baraza la Kijasusi la Taifa la Marekani (The National Intelligence Council (NIC)) linatoa taarifa kuhusu mielekeo muhimu ya Dunia (Global Trends) kila baada ya miaka minne kufuati kumalizika kwa uchaguzi wa Rais wa Marekani. Mwezi huu wa Desemba Baraza hilo limetoa taarifa yake ya tano ya Mielekeo ya Dunia 2030 (Global Trends 2030). Taarifa hii inachambua muelekeo wa kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiusalama kwa miaka 15 ijayo mpaka ifikapo 2030. Madhumuni ya taarifa hii ni kusaidia viongozi na hususan Rais wa Marekani kuelewa mielekeo muhimu ya dunia ambayo inastahiki kuzingatiwa katika kubuni na kutekeleza sera zenye lengo ya kulinda maslahi ya Marekani.
Global Trends 2030 inaonyesha kuwa katika nyanja za uchumi, China itaongoza na kuwa na uchumi mkubwa kuliko Marekani miaka michache kabla ya 2030.Mchango wa nchi za Ulaya Magharibi, Japan na Urusi katika uchumi wa dunia utaendelea kupungua. Nchi za Asia na hasa China na India zitakuwa na nguvu kubwa za kiuchumi na kijeshi. Ukiritimba wa Marekani wa nguvu za kiuchumi, kisiasa na kijeshi ulioanza baada ya vita vya pili mwaka 1945, hivi sasa unaporomoka kwa kasi kubwa.
Kwa kutumia kipimo kinachojumuisha ukubwa wa uchumi, wingi wa watu, uwekezaji katika teknolojia na matumizi katika majeshi na vyombo vya ulinzi, China itakuwa na nguvu na uwezo zaidi kuliko Marekani. Hata hivyo Marekani itaendelea kuwa na nguvu nyepesi (soft power) kwa kuendelea  kuwa na mvuto mkubwa zaidi katika medani ya utamaduni kama vile muziki, sinema, vyombo vya habari, michezo ya riadha, na uwezo wa kushirikiana na nchi nyingine hasa zile zenye mifumo ya kidemokrasia.
Mielekeo mikubwa iliyochambuliwa na Global Trends 2030 ni ongezeko kubwa la uwezo wa watu binafsi kwa sababu ya kuongezeka kwa kipato na kupungua kwa umaskini. Watu wanaoishi katika tabaka  la kati (middle class) katika nchi nyingi na hasa za Asia wataongezeka kwa kiasi kikubwa. Historia inaonyesha kuwa ongezeko la wananchi wenye kipato cha tabaka la kati huambatana na madai ya kushiriki katika maamuzi ya mambo yanayogusa maisha yao na kwa hiyo kudai na kushamiri kwa mifumo ya demokrasia.
Marekani itapoteza ukiritimba wa nguvu za kiuchumi, kisiasa na kijeshi lakini hapatatokea nchi nyingine kuwa na nguvu na uwezo kama wa Marekani katika miaka ya 1945 mpaka 2010. Mashirikiana baina ya nchi ndiko kutawezesha nchi hizo kuweza kuwa uwezo na ushawishi katika siasa za kimataifa.
Nchi zilizoendelea hivi sasa nchi za Ulaya na Japan pamoja na China zitakabiliwa na ongezeko la wazee na kupungua kwa vijana. Kasi ya ongezeko la watu katika nchi hizi utapungua sana na nyingine kama Urusi na Japan zitakabiliwa na kupungua kwa wingi wa watu. Uwiano wa watu wenye umri wa kufanya kazi ukilinganisha na wazee waliostaafu utapungua sana na kuweza kusababisha tatizo kubwa la kuhudumia wazee. Baadhi ya nchi hizi zitahitaji wahamiaji kutoka nchi nyingine ili kufanikisha azma ya kukuza uchumi na kuhudumia wazee waliostaafu.
Nchi nyingi za Afrika ikiwemo Tanzania zitaendelea kuwa na vijana wengi. Changamoto ya kuongeza ajira itaendelea kuwa kubwa. Nchi zitakazoweza kuongeza ajira ya vijana zitakuza uchumi wake kwa kasi kubwa. Ikiwa nchi zitashindwa kuongeza ajira, wingi wa vijana ambao hawana matumiani katika maisha yao kutachochea uvunjifu wa amani na vurugu za kisiasa.
Watu wengi watahamia mijini. Dunia kwa ujumla itakuwa na watu wengi wanaokaa mijini kuliko wanaokaa vijijini. Nchi ambazo hazina mipango miji mizuri na uwekezaji katika miundombinu zitakuwa na miji yenye maeneo mengi ya ovyo (slums) ambayo yatakuwa vituo vya makosa ya jinai na matumizi ya nguvu.
Dunia kwa ujumla itakuwa na mahitaji makubwa ya chakula, maji na nishati.Upungufu wa chakula na maji kwa matumizi ya binadamu utaathiriwa sana na mabadiliko ya tabia nchi. Ukame utaongezeka katika nchi ambazo hazipati mvua za kutosha. Mvua nyingi kupia kiasi na mafuriko yatatishia nchi ambazo zinapata mvua nyingi hivi sasa. Matukio ya hali ya hewa iliyovuka mipaka kama vile ukame wa kutisha na tufani na dhoruba zitaongezeka na kuathiri sana maisha ya binadamu na uzalishaji wa chakula.
Kuongezeka kwa watu wenye kipato cha tabaka la kati ambao watataka kuwa na gari na vifaa vya umeme kama vile friji na viyoyozi kutaongeza mahitaji na matumizi ya nishati na kuongeza hewa ukaa (greenhouse gases) inayoongeza joto duniani na kuchochea mabadiliko ya tabia nchi.
Uchumi wa dunia utakabiliwa na mahitaji makubwa ya chakula, maji, nishati na malighafi za viwanda. Suala la msingi ni vipi ushindani wa kupata bidhaa kama vile chakula, mafuta ya petroli na gesi, chuma, shaba na madini mengine kunaweza kusababisha migogoro ya kuichumi, kisiasa na kiusalama. Mtikisiko wa sekta ya fedha na uchumi uliotokea mwaka 2008 na ambao bado unaathiri uchumi wa dunia itadhibitiwa au itaendelea kutokea? Je nchi zitashirikiana ili kusimamia utandawazi uwe na manufaa kwa washiriki wote wa uchumi wa dunia na kuzuia athari kubwa zisitokee na uchumi wa dunia kuporomoka?
Je serikali na asasi za kimataifa zitakuwa na uwezo wa utawala bora wa kukabiliana na mabadiliko yatakayotokea katika uchumi wa dunia na kuweza kubuni na kutekeleza sera muafaka zinazokwenda na mabadiliko yanayotokea?
Je Marekani itaelewa na kukubali kuwa ukiritimba wa nguvu zake za kiuchumi, kisiasa na kijeshi umeporomoka na kukubali kutoa nafasi na kushirikiana na mataifa mengine na hasa China ambayo nguvu zake za kichumi na kijeshi zitaongezeka? Uongozi wa dola ya Marekani na hasa kushindwa kufikia mwafaka kati ya Bunge la Wawakilishi linaloongozwa na Republican, na Rais Obama na Baraza la Senate lenye maseneta wengi wa Chama cha Demokrati kunaashiria kuwa Marekani, inaweza kuwa na tatizo la kuwepo kwa utawala bora wenye uwezo wa kukubali na kuyashughulikia ipasavyo mabadiliko  makubwa yanayopunguza ukiriritimba wa dola ya Marekani katika mahusiano ya kimataifa.
Ukuaji wa uchumi wa dunia umechochewa na mabadiliko ya teknolojia. Katika miaka 15 ijayo mabadiliko gani ya teknolojia yanaweza yakaongeza ukuaji wa uchumi na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na ongezeko kubwa la watu watakaokuwa wanaishi mijini?
 Mabadiliko ya teknolojia ya kuchimba gesi na mafuta yanaweza kusababisha mabadiliko makubwa ya uchumi. Makampuni ya Marekani yamevumbua teknolojia inayoweza kuchimba gesi na mafuta yaliyoko kwenye miamba ya mawe chini ya ardhi ambayo siku za nyuma iliaminiwa kuwa gesi na mafuta hayo hayawezwi kuchimbwa. Ongezeko la uzalishaji wa gesi toka kwenye miamba umepunguza sana bei ya gesi Marekani kwa zaidi ya asilimia 70. Marekani inategemewa kuwa mzalishaji mkubwa namba moja wa mafuta ya petroli kuzidi Saudi Arabia na Urusi ifikapo mwaka 2017. Teknolojia hii itafanya Marekani kujitegemea kwa nishati na hata kuwa muuzaji wa gesi na mafuta nchi za nje. Kuna uwezekano wa bei ya mafuta na gesi katika soko la dunia kupungua sana na kuathiri nchi zinazotegemea uuzaji wa mafuta kama vile Saud Arabia na nchi nyingine za ghuba ya Uajemi
Ongezeko la uzalishaji wa gesi umeongeza ushindani wa Marekani katika viwanda vya plastiki na kemikali vinavyotumia gesi kama malighafi. Uwekezaji mkubwa wa dola bilioni 80 utafanyika katika viwanda hivi katika miaka michache ijayo. Ulaya na hasa Ujerumani yenye viwanda vikubwa vya kemikali inaanza kutaharuki kuwa kuongezeka kwa ushindani wa Marekani katika viwanda vya kemikali kwa sababu ya bei rahisi ya gesi kutaathiri viwanda vyake.
China ina miamba mingi yenye gesi lakini bado haijamudu na kumiliki teknolojia mya ya kuchimba gesi hiyo. Teknolojia hii mpya inahitaji matumizi makubwa ya maji ambayo ni haba katika nchi ya China. Isitoshe teknolojia hii inaweza kusababisha matetemeko madogo ya ardhi ambayo athari zake zinawaeza kuwa kubwa. Ikiwa teknolojia hii itaendelezwa na ikapunguza matumizi ya maji na makampuni ya China yakamudu teknolojia hii basi nchi zinauzouza mafuta ya petroli zitaathiriwa vibaya zaidi na kuporomoka kwa bei ya mafuta.
Kupungua kwa bei ya gesi nchini Marekani kunaweza kuathiri juhudi za kuwekeza na kuendeleza nishati mbadala ya jua, upepo na bayogesi na kwa hiyo kuendeleza uchafuzi wa mazingira.
Teknolojia ya viwanda pia inaendelea kubadilika. Matumizi ya kompyuta na roboti kutaka uzalishaji kunapunguza mahitaji ya nguvu kazi inayolipwa mishahara midogo. Kwa mfano utengenezaji wa bodi mama (mother board) ya Kompyuta ambacho ndiyo kifaa muhimu chenye chipu zinazoendesha na kuhifadhi nakala zote, hivi sasa kinatengenezwa na roboti badala ya binadamu. Mabadiliko haya ya teknolojia yanaweza kupunguza sana mahitaji ya wafanyakazi viwandani na yakarudisha viwanda vingi kwenye nchi zilizoendelea.
Tanzania ina wajibu wa kujipanga kutumia fursa za mieleko mikuu ya uchumi wa dunia na kujihami kwa athari zinazoweza kutokea. Kwanza kuimarisha, kuboresha na kuongeza tija katika sekta ya kilimo ni jambo muhimu kuongeza uzalishaji wa chakula kukidhi mahitaji ya ndani na kuuza katika soko la dunia. China na India zitakuwa na uchumi mkubwa na biashara ya kimataifa. Tanzania ijipange vizuri kuweza kunufaika na biashara na nchi hizo badala ya kuwa wazalishaji wa malighafi tu.
Mkakati wa kukuza uchumi unao ongeza ajira unapaswa kuzingatia mabadiliko yanayoweza kutokea. Tuandae maeneo maalum ya uchumi karibu na bandari ambayo ni makubwa yatakayosheheni miundombinu inayohitajiwa na viwanda ili gharama za uzalishaji ziwe ndogo na tuweze kuwa washindani katika soko la ndani, soko la kanda na soko la dunia.
Sekta ya gesi na mafuta iendelezwe haraka kabla ya tishio la kuporomoka kwa bei. Yajengwe mazingira ya kuanzisha viwanda vinavyotumia gesi kama malighafi. Mji wa Mtwara wenye bandari asilia uendelezwe kuwa makao Makuu ya sekta na viwanda vya gesi
Jiji la  Dar es Salaam limekua bila kufuata taratibu za mpango mji. Ni vyema tuwe na mipango mizuri ya kukuza miji yetu ili iwe na huduma na gharama nafuu za uzalishaji wa bidhaa na huduma.
Global Trends pia imechambua nchi ambazo zinaweza kuwa na misukosuko mikubwa ya kisiasa na kijamii inayoweza kusababisha kuporomoka kabisa kwa utawala wa dola (state failure) kati ya sasa na mwaka 2030. Nchi nyingi za jirani ikiwemo Burundi, Rwanda, Uganda, Malawi na Congo zinaweza kuathirika na kuporomoka kwa utawala wa dola. Tanzania inapaswa kuzingatia uwezekano huo katika kuandaa vyombo vyake vya ulinzi.
Navishauri vyombo vyetu vya ulinzi na Tume ya Mipango vipitie taarifa hii na vijipange kufanya uchambuzi wa nchi za kanda yetu ili tuweze kubuni na kutekeleza sera muafaka za kukuza uchumi unaoleta neema kwa Watanzania wote huku tukilinda mazingira na kujihami kiusalama.

No comments:

Post a Comment