Sunday, November 25, 2012

MSIMAMO WA JUMUIYA YA VIJANA KWA TFDA NA WAUZAJI WA MADAWA YA KULEVYA NCHINI.

Naibu katibu Mkuu JUVICF-Thomas Malima

 TFDA ibomolewe, isukwe upya, wahujumu wa madawa ya umma washitakiwe.
Vinara wa Madawa ya kulevya nao watajwe na kufikishwa mahakamani.
Serikali ya Tanzania kupitia wizara ya Afya, Mamlaka ya Chakula na Dawa, pamoja na Mamlaka ya Bandari vimekuwa mawakala wakubwa wa biashara haramu ya afya za watanzania. Afya za watanzania zinaendelea kuwekwa rehani na waliopewa mamlaka ya kuongoza.
Wizara ya Afya imekuwa ikiruhusu uwepo wa zahanati na maduka ya madawa yasiyo na wataalamu wa afya ambapo watanzania wengi wamekuwa wakipewa dawa zisiendana na magonjwa wanayoumwa. Hali imesababisha madhara makubwa kwa wagonjwa. Utafiti uliofanywa na Youth Initiative Tanzania (yiTa) na TWAWEZA kuanzia Novemba 2011 hadi Agosti 2012 ulibaini kuwa zaidi ya 93% ya huduma zinazotolewa katika zahanati na maduka binafsi ya dawa jijini Dar es salaam, hutolewa bila kutumia utaalamu wa afya. Je, wizara ya Afya ina mpango gani wa kukomesha hali hii?.
Pamoja na hali kuwa mbaya kiasi hicho, TFDA imekuwa ikpata kashfa kubwa za kuhatariasha maisha ya watu kila kukicha lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa dhidi ya mabosi wa TFDA. Watanzania watakumbuka kuwa mwishoni mwa mwaka 2011 watafiti wa ugonjwa wa Maralia toka Uingereza wakiongozwa na Dr. Washington walitoa ripoti juu namna ambavyo Serikali za Afrika zimekuwa zikipokea madawa bandia toka China na namna ambavyo madawa hayo yanavyoathiri afya za watu. Lakin cha ajabu TFDA ilikana kupokea madawa bandia, lakini baada ya miezi miwili madawa bandia ya Maralia yakakamatwa Mwanza na Kilimanjaro. Ndipo baadaye viongozi wa TFDA walipojitokeza kwa aibu na kukiri kuwapo kwa madawa hayo bandia nchini. Lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi yao.
Hivi karibuni, kumepatika dawa feki za kuongeza nguvu za waathirika wa VVU, lakini pia hakuna hatua zozote zilizokwisha chukuliwa.
Na cha kusikitisha zaidi, ni pale Watanzania wanaambiwa kuwa hakuna dawa katika hospitali za umma wakati hospitali za binafsi zina shehena ya dawa zilizoandikwa “NOT FOR SALE”. Na cha ajabu zaidi TFDA wanakili kuwa wameibiwa dawa zilizotakiwa zitolewe bure kwenye zahanati na hospitali za serikali lakini zimepotea na zinapatikana katika hospitali na maduka binafsi ya dawa zikiwa zimefutwa nembo ya NOT FOR SALE. Wakati haya yanatendeka, hospitali za umma ziko taabani, hakuna dawa. Imebaki kwenda hospitali na kupima, kisha unaambiwa nenda ukanunue dawa katika dawa Fulani. Lakini serikali imekaa kimya dhiti ya mamlaka hizi.
Jumuiya ya Vijana ya CUF (JUVICUF), inatambua kuwa endapo hatua za haraka hazitachukuliwa, kunahatri kubwa ya kuwapoteza watoto wengi ambao ndio vijana wa kesho. Akina mama na Vijana nao wako hatarini kupotea. Hivyo tunaitaka serikali kuwaachisha kazi wakurugenzi wote wa TFDA ili hatua za kisheria zichukue mkondo wake.
Nalo suala la watuhumiwa wa madawa ya kulevya limewekwa kwapuni kwa sasa. Serikali ilishahidi kutoa orodha yao lakini haitaki kutoa hadi sasa. Hili ni suala linaloathiri maisha na nguvu kazi ya vijana moja kwa moja. Vijana wengi wanapotea kwa kuathirika na madawa ya kulevya.
JUVICUF inaitaka serikali iwataje wauzaji na wasambazaji wa madawa ya kulevya nchini bila kujali vyeo na haiba yao katika jamii. Na baada ya kuwataja, wafikishwe mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Endapo serikali haitachukua hatua za kuisafisha TFDA na kuwataja pamoja na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa madawa ya kulevya kama ilivyoahidi, na kwa kuwa waathirika wakubwa madawa ya Kulevya na madhara ya kuuzwa kwa dawa kiholela pamoja hospitali za umma kukosa dawa ni Vijana, JUVICUF itafanya maandamano ya amani hadi wizara ya afya kushinikiza hatua za uwajibikaji na kisheria zichukuliwe.
Imeandaliwa na:
Thomas D.C Malima
Naibu Katibu
Jumuiya ya Vijana ya CUF (JUVICUF)-Taifa.

No comments:

Post a Comment