TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU JUHUDI ZA CUF ZA KUENDELEZA AMANI NA UTULIVU BAADA YA SALA YA IJUMAA TAREHE
Mwenyekiti Cuf Taifa - Prof Ibrahim Haruna Lipumba
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi) TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU JUHUDI ZA CUF ZA KUENDELEZA AMANI NA UTULIVU BAADA YA SALA YA IJUMAA TAREHE 2 NOVEMBA 2012
Siku ya Alhamis nikielekea Muhimbili kumpeleka shangazi yangu hospitali
nilipata taarifa kuwa Imam wa msikiti wa Masjid Haq (ulioko jirani na
Afisi Kuu ya CUF na ambapo nasali sala ya Ijumaa nikiwa Afisi Kuu) na
watu wengine watatu akiwemo Sheikh Ramadhan S. Sanze (ambaye namfahamu
kwa muda mrefu). Sadik Gogo na Mzee Abdillah wamekamatwa na wamefikishwa
kituo cha polisi cha kati (Central Police Station). Nilistushwa na
kamata kamata hii na nikahofia kuwa inaweza kuongeza jazba miongoni mwa
waumini wa Kiislam. Baada ya shangazi kupata tiba katika hospitali ya
Muhimbili nilimrudisha nyumbani na nikampigia simu Mkurugenzi wa Haki za
Binadamu na mahusiano ya umma, Abdul Kambaya, tukutane kituo cha
polisi cha kati kuulizia sababu za kukamatwa Imam wa Masjid Haq na
wenzake watatu na kama tunaweza kuwawekea dhamana. Tulipofika kituo
cha polisi tulibaini kuwa Imam wa Msikiti wa Masjid Haq hajakamatwa bali
kuna muumini mwingine kwa jina la Mkadam Swalehe ndiye aliyekamatwa.
Tulizungumza na RPC Kova na RCO Msangi kuhusu kuachiliwa kwa wale
waliokamatwa. Tukafahamishwa kuwa itabidi wafanyiwe mahojiano na baadaye
wataachiliwa isipokuwa Mkadam Swalehe ambaye ana faili jingine pale
polisi linaloendelea kufanyiwa upelelezi. Tulifahamishwa kuwa nitume mtu
saa 10:30 jioni ili aweze kufuatilia utaratibu wa kuachiliwa watuhumiwa
watatu akiwemo Sheikh Ramadhan Sanze, Sadik Gogo na Mzee Abdillah.
Nilishauriana na Wakurugenzi wa CUF walioko Dar es Salaam na Naibu
Katibu Mkuu, Julius Mtatiro hatua za kuchukua. Taarifa za kukamatwa
Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake zilikuwa zinaenea na kupandisha jazba
ya Waislam wengi. Tulipata wasiwasi kuwa jazba hii inaweza kupelekea
Waislam wengi kuandamana baada ya sala ya Ijumaa. Ikiwa Sheikh Ramadhan
Sanze na wenzake wataachiwa na Waislam wakapata taarifa hiyo inaweza
kusaidia kupunguza jazba na watu wasishiriki maandamano baada ya sala ya
Ijumaa. Nilimpa jukum Abdul Kambaya afuatilie Central
PoliceStation, suala la kuachiliwa Sheikh Sanze na wenzake.
Niliwasiliana naye kwa simu na kuzungumza na RCO na nikaamini kuwa
Sheikh Ramadhan Sanze, Sadik Gogo na Mzee Abdillah wataachiwa baada ya
kukamilisha mahojiano. Ilikuwa inakaribia saa 12 jioni. Muda wa kuitisha
Press Conference haukuwepo. Tukakubaliana Naibu Katibu Mkuu awasiliane
na wahariri wa habari wa vituo vya televisheni Channel 10, TBC1, Star
TV, Mlimani TV na ITV ili niweze kutoa taarifa ya kuwasihi Waislam
warudi majumbani na kwenye shughuli zao baada ya sala ya Ijumaa.
Niliweza kufanya mahojiano na Channel 10, TBC1, na ITV. Kwa bahati
mbaya Camera person wa Star TV alikuwa kwenye shughuli nyingine na kwa
hiyo sikuweza kufanya mahojiano na Star TV. Vilevile wapiga picha wa
Mlimani TV hawakuwepo kwenye studio. Pia nilipata bahati ya kuzungumza
na Radio Iman inayosikilizwa na Waislam wengi na kueleza maoni yangu
kuwa Waislam wasiandamane baada ya sala ya Ijumaa. Baada ya kutoa
taarifa kwenye vituo vitatu vya televisheni na Radio Iman kuwa Sheikh
Ramadhan Sanze na wenzake wataachiliwa na kuwasihi Waislam wasishiriki
maandamano baada ya sala ya Ijumaa nilimpigia simu Abdul Kambaya
kuulizia kama naweza kuzungumza na Sheikh Ramadhan Sanze. Kambaya
akanieleza mambo yamebadilika na hawajaachiwa. Niliwasiliana na RCO na
nikabaini kuwa suala hilo haliko tena chini ya uamuzi wake na
litakamilishwa siku ijayo. Usiku wa alhamisi kuamkia Ijumaa
nilijaribu kuwasiliana na Rais Kikwete kupitia wasaidizi wake ili
nimfahamishe mantiki na sababu ya hatua nilizochukua na atumie uwezo
wake alionao Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake waachiliwe. Kwa bahati
msaidizi mmoja alipata ujumbe wangu wa simu na akanipigia simu saa 6:50
usiku na kunifahamisha atajitahidi kuufikisha ujumbe wangu kwa Mhe.
Rais ili nipate kuongea naye kuhusu jamaa wanaoshikiliwa na polisi
waachiwe ili kupunguza jazba na kuepusha shari. Niliyezungumza naye
alikuwa Dodoma na Rais alikuwa Arusha na ratiba yake ilikuwa imebana
sana na kwa hiyo hakuweza kupata fursa ya kunipigia simu siku hiyo ya
Ijumaa. Siku ya Ijumaa Abdul Kambaya aliendelea kufuatilia kuachiwa
kwa Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake Central Police Station. Nami katika
kuhangaika ili waliokamatwa waachiliwe nilipata fursa ya kuzungumza na
IGP na kumfahamisha sababu ya juhudi nilizochukua na mategemeo yangu
kuwa Sheikh Sanze na wenzake wangeachiwa. Ninakiri kuwa katika
mazungumzo ya simu, IGP Mwema alikuwa msikivu na mkarimu sana katika
kauli yake. Alinishukuru kwa kauli niliyoitoa katika vituo vya
televisheni na kuwa atafuatilia suala nililomueleza. Hatimaye Sheikh
Ramadhan Sanze na wenzake waliachiwa. Naamini kama Sheikh Ramadhan
Sanze na wenzake wangeachiwa ingesaidia sana kupunguza jazba. Hata hivyo
Waislam wengi na wananchi wengine kwa ujumla walipokea vizuri wito
wangu na hawakushiriki katika maandamano. Baadhi wamenikosoa na kushauri
kuwa ilifaa nisubiri mpaka baada ya maandamano kufanyika na kama
patatokea majeruhi na vifo ndipo nitoe tamko la kulaani vitendo vya
polisi na serikali. Katika mitandao ya kijamii wengine wamekejeli
juhudi zangu. Nilikubali kushiriki katika kipindi cha Makutano show
kinachoendeshwa na Bi. Fina ambapo hupata maswali toka Jamii Forum. Moja
ya swali lililotolewa ni “Muulize very very solid, kuna agenda gani
kati ya Cuf na uislam? mtaani leo wanasema kauli ya Lipumba ya jana
kusitisha maandamano wameitii, na ukiangalia mikutano yake pale jangwani
utafikiri kuna mawaidha ni balaghashia na baibui.” Fina hakupata muda
wa kuniuliza swali hili. Jibu lake ni la wazi. CUF inasimamia Haki Sawa
kwa Wananchi Wote. Kuna Watanzania wengi ambao ni Waislam na wao pia
wanastahiki kutendewa haki katika nchi yao. Kuhusu balaghashia na baibui
ni vyema vijana wakatazama picha za umati wa watu uliokuwa unahutubiwa
na Mwalimu Nyerere wakati wa kupigania uhuru wa nchi hii. Picha hizo pia
zinaonyesha waliokuwa wakipigania uhuru wengi walivaa balaghashia na
baibui hata Mwalimu Nyerere alipewa zawadi nyingi za balaghashia na
akaamua kuzivaa. Kushamiri kwa demokrasia ya kweli msingi wake
mkubwa ni amani na utulivu. Amani ya kweli haipatikani bila kuwepo haki.
Kesi ya Sheikh Ponda msingi wake na madai ya kiwanja. Ki msingi kesi ya
madai ya kusuluhishwa na Mahakama ya ardhi. Sheikh Ponda ana haki ya
msingi ya kupewa dhamana hata kama kauli zake haziifurahishi serikali.
Nasikitika sana katika kipindi hiki tete, viongozi wa serikali
wameshindwa kuchukua juhudi za makusudi kuzungumza na Maimam wa misikiti
na viongozi wa asasi za Kiislam kupunguza jazba. Badala yake wameachia
kauli za vitisho vya Kamanda Kova ndiyo viwe mawasiliano kati ya
serikali na Waislam. Ni vyema serikali ikatumia busara na kuwasiliana na
Maimamu wa misikiti na viongozi wa asasi za Kiislam kuelewa hoja na
malalamiko yao. Hatimaye nimepata fursa ya kuzungumza na Mheshimiwa
Rais leo asubuhi na nikamueleza juhudi nilizozichukua kuweza kupunguza
jazba na kuwaomba Waislam wasishiriki kwenye maandamano baada ya sala ya
Ijumaa. Ni wazi hali hii ya mtafaruku ndani ya jamii inamsononesha sana
Mheshimiwa Rais na ninaamini atajitahidi kwa uwezo wake wote kutafuta
suluhisho. Katika kutafuta suluhu ya mtafaruku huu nitaendelea na
jitihada za kutafuta fursa niweze kubadilishana mawazo na Rais Kikwete.
Nitazungumza na viongozi wa asasi za Kiislam. Nitazungumza na viongozi
wa Makanisa ya Kikristo. Madhumuni ya mazungumzo yangu ni kuwafahamisha
mantiki ya juhudi nilizofanya na kushauriana misingi muhimu ya Waumini
wote kuheshimiana na kuvumiliana ili tujenge Tanzania yenye haki sawa
kwa wote.
No comments:
Post a Comment