Prof Ibrahim Lipumba Mwenyekiti Wa Cuf Taifa |
Katika nchi nyingi
maskini, mipango na miradi ya maendeleo na usambazaji wa huduma za msingi
unakwamishwa na serikali isiyokuwa na fedha za kutosha. Katika kusimamia
maendeleo hakuna sera muhimu ya serikali inayozidi mfumo na viwango vya kodi. Hata
hivyo kurekebisha mfumo na kuongeza viwango vya kodi kunaweza kusababisha
serikali kuanguka. Matumizi ya serikali yanahitajika katika kuhakikisha kuwepo
kwa amani, utulivu na usalama wa raia. Huduma za msingi za jamii kama vile
elimu bora kwa watoto wote, huduma za afya za msingi kwa wananchi zinahitajika
ili wananchi wafurahie maisha yao lakini vile vile wananchi wenye elimu na afya
bora wanakuwa na tija kubwa katika uzalishaji wa bidhaa na huduma. Kukuza
uchumi utakaowaletea neema wananchi wote kunahitaji miundombinu ya barabara,
reli, bandari, viwanja vya ndege, ufuaji na usambazaji wa umeme, utafiti wa
kilimo na huduma za ugani. Katika maeneo mengi ya miundimbinu, sekta binafsi
haiwezi kuwekeza. Serikali ina jukumu la kuendeleza miundombinu na kusambaza
huduma za jamii.
Kwa muda mrefu
bajeti ya Tanzania imetegemea kwa kiwango kikubwa cha asilimia 30-40 fedha kutoka
kwa wahisani wa nchi za nje. Ukusanyaji wa mapato ya ndani umeongezeka. Lakini
nakisi ya bajeti ya serikali pia imekuwa inaongezeka mpaka kufikia zaidi ya
asilimia 11 katika miaka mitatu ya fedha 2009/10 – 2011/12. Katika miaka ya
fedha 15 iliyopita mapato ya ndani hayakidhi matumizi ya kawaida. Kwa hiyo mapato
ya kodi hayachangii bajeti ya maendeleo. Tanzania inahitaji iongeze ukusanyaji
wa kodi ufikie asilimia 22 – 25 ya pato la taifa ukilinganisha na ukusanyaji wa
mapato ya ndani ya asilimi 16 hivi sasa.
Mchakato wa ujenzi
na uimarishaji wa dola unaenda sambamba na uwezo wa serikali kukusanya kodi na
mapato mengine. Ulipaji na ukusanyaji wa kodi na usambazaji wa huduma za
serikali unatoa fursa ya ujenzi wa uhalali wa dola katika jamii. Ikiwa
ukusanyaji wa kodi ni wa kutumia mabavu na kuwanyanyasa wananchi kama ilivyokuwa
katika ukusanyaji wa kodi ya kichwa wakati wa ukoloni ambayo baada ya uhuru
ilibatizwa jina zuri na kuitwa kodi ya maendeleo, uhalali wa dola unaathirika
na mahusiano ya dola na raia yanakuwa mabovu. Ikiwa mfumo na viwango vya kodi
vinatokana na majadiliano na makubaliano kati ya serikali na wananchi, ulipaji
na ukusanyaji wa kodi una fursa ya kuchangia katika ujenzi wa dola yenye
uhalali mbele ya jamii. Mapinduzi ya Marekani ya mwaka 1776 yalianza kama mgomo
wa kulipa kodi kwa serikali ya Mfalme wa Uingereza. Kauli mbiu ya Wamarekani
ilikuwa “No taxation without representation” tafsiri yake ikiwa hakuna kulipa
kodi bila kuwakilishwa.
Sera za kodi
zinapaswa kutazamwa na kuchambuliwa kwa upana zaidi. Ulipaji na ukusanyaji kodi
uwe nyezo ya kujenga dola yenye uhalali na inayowajibika kwa wananchi. Ili azma
hii ya ujenzi wa dola yenye uhalali iweze kufikiwa ni lazima mfumo wa kodi uwe
na uonekane kuwa ni wa haki na unaendeleza usawa katika jamii. Matumizi ya
serikali yawe adilifu na wananchi waone wananufaika na kodi wanazolipa. Ikiwa
kazi kubwa ya polisi ni kupokea rushwa na kuwabambikizia kesi wananchi,
majambazi yanawapora wananchi, hakuna usalama wa raia na mali zao, mahakama
zimejaa rushwa, huduma za afya mbovu, watoto hawapati elimu bora, barabara hazitengenezwi,
umeme unakatika kila wakati ni vigumu kuwahamasisha wananchi kulipa kodi na
kutumia mfumo wa kodi kujenga dola yenye uhalali kwa wananchi.
Watanzania wengi
wanaamini kuwa mfumo wa kodi hauna haki na unawabana wananchi maskini. Theluthi
moja ya mapato ya kodi inatokana na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ambayo
kila mnunuzi wa bidhaa na huduma analipa kiwango sawa cha kodi bila kujali kama
ana kipato kikubwa au kidogo. Makampuni makubwa na hususan makampuni ya madini
yamepewa misamaha ya kodi. Wawekezaji wa nje wanasamehewa kodi lakini makampuni
ya ndani yanabanwa kulipa kodi. Mawaziri, Wabunge, Maafisa waandamizi katika
serikali na mashirika ya umma wanasamehewa kodi wanapoagiza magari na vifaa
vingine kutoka nje.
Ili kujenga
utamaduni wa kulipa kodi kwa hiari na kuongeza mapato ya serikali ni lazima
kurekebisha mfumo wa kodi uwe wa haki na usawa. Wananchi washirikishwe kwa
kupewa elimu ya kweli kuhusu mfumo wa kodi. Mijadala kuhusu mfumo wa kodi iwe
wazi.
Kuwepo kwa
utamaduni mzuri wa kulipa kodi unamfanya mwananchi aone fahari kulipa kodi kwa
mujibu wa sheria zilizopo. Ulipaji kodi wa hiari unategemea sana imani ya
walipa kodi kuhusu mfumo mzima wa kodi na jinsi mamalaka ya kodi inavyotekeleza
wajibu wake. Ulipaji wa kodi wa hiari unakuwepo ikiwa wananchi wanahisi kuwa
kama raia wana wajibu wa kulipa kodi. Kuwa na hisia kuwa kulipa kodi ni wajibu
kanategemea sana wananchi kuamini kuwa serikali inatumia vizuri na kwa uadilifu
fedha za kodi kwa manufaa ya umma.
Utendaji ulio wazi
na wa haki wa wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato unasaidia sana katika kujenga
utamaduni wa kulipa kodi kwa hiari. Ikiwa jamii inaamini kuwa rushwa imekithiri
katika mamlaka ya mapato, utamaduni wa kulipa kodi kwa hiari hauwezi kujengeka.
Kuongeza uwezo na nguvu za mamlaka ya mapato zinaweza kusaidia zaidi kuongeza
mapato ya wakusanya kodi kuliko mapato ya serikali. Katika kuandaa na
kutekeleza sera za kodi ni muhimu kuzingatia hali halisi ya uchumi na jamii ya
nchi husika. Sera za kodi za nchi zilizoendelea zinasisitiza sana ufanisi
katika mfumo, viwango na ukusanyaji wa kodi. Pia huzungumzia masuala ya kukwepa
kulipa kodi lakini mara nyingi hawachambui matatizo ya rushwa katika ulipaji na
ukusanyaji wa kodi. Tatizo la kukabiliana na rushwa linapaswa kuzingatiwa kwa makini
katika kuandaa na kutekeleza sera za kodi. Mfumo wa kodi unaofaa kwa nchi
nyingi zinazoendelea kama Tanzania ni ule utakaopunguza mianya ya rushwa.
Viwango vya kodi
vinaweza kukwaza ilipaji wa kodi wa hiari. Mzigo wa kodi ukiwa mkubwa sana watu
watakwepa kulipa kodi. Ikiwa utaratibu wa kulipa kodi ni mwepesi na hauna
gharama kubwa ya muda na pesa, ulipaji wa kodi wa hiari utaongezeka. Kama kuna
watu wengi na kampuni nyingi zinazokwepa kulipa kodi, zitawakatisha tamaa wale
wanaolipa kodi kwa hiari. Kuwepo kwa ukwepaji kodi ambao hauadhibiwi kunaongeza
ukwepaji kodi. Kama wananchi wanaamini kuwa hakuna ukwepaji wa kodi mkubwa,
wengi watajitokeza kulipa kodi.
Maeneo muhimu ya
kuimarisha ulipaji wa kodi wa hiari ni pamoja na sera za kodi, utawala na
uendeshaji wa mamlaka ya kukusanya mapato na uadilifu katika matumizi ya fedha
za umma.
Sera za kodi
zinapaswa kuwa wazi, nyepesi kuzielewa na zisimamie haki na usawa. Viwango vya
kodi viwe vya wastani na vichache. Changamoto kubwa inayoathiri ujenzi wa mfumo
wa kodi ulio na uwazi na unaowajibika kwa jamii ni misamaha ya kodi kwa
wawekezaji wa nje. Misamaha ya kodi inapunguza mapato na kuchochea rushwa na
ukwepaji wa kodi. Likizo za kodi ya mapato ya wawekezaji wa nje zinatumiwa
vibaya kujenga utaratibu wa kuongeza gharama za uendeshaji ili kupunguza faida
na kwa hiyo kulipa kodi kidogo. Kwa mfano makampuni binafsi ya usafiri wa ndege
yalikopa katika benki za hapa hapa nchini kununua ndege za abiria. Baada ya
kumaliza kulipia mkopo, walihamisha usajili wa ndege hizo kwenda Cyprus
haidhuru ndege zimenunuliwa hapa hapa na zipo nchini. Sasa makampuni haya yanaandaa
hesabu za mapato na matumizi zinazoonyesha kuwa
wamekodisha ndege toka Cyprus na kwa hiyo wanalipa ada ya kukodisha na
kupunguza faida wanayopata na kodi ya mapato wanayolipa. Vitendo kama
vinaendelea kufanyika kwa sababu ya kuwepo rushwa ndani ya mamlaka
zinazosimamia usafiri wa anga na ukusanyaji wa kodi.
Watanzania wengi
wanaamini kuwa mfumo wa kodi hauna haki unapendelea wawekezaji wa nje. Katika
mazingira haya ni vigumu kujenga utamaduni wa kulipa kodi kwa hiari. Kufuta
misamaha ya kodi ni hatua muhimu katika kuhamasisha ulipaji wa kodi wa hiari na
kuishirikisha wananchi katika mijadala ya kodi itakayosaidia kujenga jamii
itakayokuwa na fahari katika ulipaji wa kodi.
Mamlaka ya mapato
ina kazi muhimu tatu. Mosi kujenga utaratibu rahisi wa kulipa kodi. Pili, kufuatilia
na kuhakikisha kuwa wahusika wote wanalipa kodi zinazowahusu na wale wanaokwepa
kulipa kodi wanachukuliwa hatua za kisheria. Tatu kuboresha utaratibu wa kulipa
kodi ili wananchi wengi walipe kodi kwa hiari. Mamlaka ya mapato ina wajibu wa
kujenga mazingira ya kurahisha ulipaji wa kodi na iwe na ufuatiliaji makini wa
kuhakikisha kodi zinalipwa na wanaokwepa wanaadhibiwa kwa mujibu wa sheria.
Ili wananchi wajue
wajibu wao wa kulipa kodi, elimu ya uraia kuhusu kodi ni muhimu. Kwa wananchi
wa kawaida katika sekta isiyo rasmi ni vizuri elimu kuhusu kodi iambatane na
mafunzo ya ujasiriamali na uendeshaji wa shughuli za biashara. Huduma kwa
walipa kodi zihakikishe kuwa utaratibu wa kulipa kodi unakuwa mwepesi. Gharama
za kukwepa kodi kwa maksudi ziwe kubwa ili wananchi wawe na motisha wa kulipa
kodi. Wanaolipa kodi kwa hiari wataongezeka ikiwa maafisa wa Mamalaka ya Mapato
itawaheshimu na kuwatendea haki bila upendeleo kwa baadhi ya walipa kodi.
Vitendo vya ufisadi vya baadhi ya maafisa wa Mamlaka ya Mapato ya kuwabana
wafanyabiashara watoe rushwa ili wasiongezewe kodi vinaathiri sana ujenzi wa
utamaduni wa kulipa kodi.
Ni muhimu kuwepo na
uhusiano wa karibu na unaoonekana kati ya kulipa kodi na huduma za serikali.
Uadilifu katika matumizi ya serikali na huduma bora zinazogharimiwa na serikali
zinasaidia kuongeza motisha wa kulipa kodi. Kwa mfano serikali iwe wazi katika kuonyesha
ujenzi na ukarabati wa barabara unaolipiwa na kodi ya mafuta ya petroli kwa
ajili ya kujenga barabara.
Watanzania wengi
hawashiriki katika kulipa kodi ya mapato. Katika nchi yenye watu milioni 44, ni
wananchi laki tano tu ndiyo wenye namba za kulipia kodi. Wananchi wengi
wameajiriwa au kujiajiri katika sekta ya kilimo asilia vijijini na sekta isiyo
rasmi. Baadhi ya wananchi katika sekta isiyo rasmi wana vipato vikubwa vya
kuweza kulipa kodi. Kuzirasimisha shughuli za sekta isiyo rasmi kuna faida kwa
wajasiriamali wa sekta hiyo. Shughuli zao zinapofahamika wanaweza kupata mikopo
ya kupanua biashara zao, mafunzo ya ujasiriamali, masoko na teknolojia bora ya
kuendeleza shughuli zao. Mkakati wa kupanua wigo wa walipa kodi toka sekta
isiyo rasmi ujikite katika mafunzo ya ujasiriamali yatakayoongeza ufanisi na
faida kwa wafanya biashara wa sekta isiyo rasmi na kuwawezesha kulipa kodi bila
kuathiri sana mapato yao.
Athari kwa utawala
bora kwa nchi inayotegemea wigo mkubwa wa walipa kodi na uwezo wa serikali
kukusanya kodi ni pamoja na kuwa na dola inayowajibika katika matumizi ya fedha
za walipa kodi kuhakikisha inawaletea neema wananchi wake wote. Ili serikali
ikusanye kodi za kutosha toka kwa wananchi inabidi ijenge uwezo wa kupata
taarifa ya mapato na matumizi ya raia ili kuweza kukusanya kodi kwa ufanisi na
uadilifu. Juhudi za kujenga uwezo wa kukusanya kodi zinaifanya serikali kwa
ujumla wake kuwa na uwezo wa kiutawala.
Raia wanaotozwa
kodi wanakuwa na shauku ya kujua matumizi ya kodi zao na kwa hiyo kuishinikiza
serikali kuwajibika katika matumizi yake. Mchakato wa kutoza na kukusanya kodi
unawafanya raia kuafiki kulipa kodi kwa hiari ikiwa wanaamini kodi zao
zinatumiwa vizuri kwa manufaa ya umma. Viwango vya kodi visiwe vya juu sana
vinavyoathiri vibaya maisha ya mlipa kodi. Kushiriki kwa wananchi katika
mijadala ya sera za kodi na matumizi ya serikali kunasaidia kuweka viwango na
mfumo wa kodi unaotabirika. Bunge linapata nguvu ya kuiwajibisha serikali.
Bila kuweka
utaratibu wa mkataba wa jamii (social contract) kati ya wananchi na dola
kupitia ulipaji kodi, wananchi hawawezi kuwa na motisha wa kujenga uwezo wa
kuchunguza na kukagua matumizi ya serikali na kuiwajibisha. Bila wananchi kuwa
ngangari wa kujua matumizi ya fedha zao za kodi, hapawezi kuwepo na ufanisi wa
kutosha katika matumizi ya serikali.
Wananchi watakuwa
na motisha kufuatilia ufanisi wa matumizi ya serikali ikiwa kwa kiasi kikubwa matumizi
hayo yanatokana na ulipaji wa kodi wa wananchi wenyewe na siyo misaada kutoka
nje. Kuendelea kutegemea misaada ya nje kunaathiri kujenga dola inayowajibika
kwa wananchi. CCM imejenga dola tegemezi. Ni muhimu kwa Watanzania kujipanga na
kuchagua uongozi wenye dira utakaouhakikisha kuwa misamaha holela ya kodi
inaondolewa, wawekezaji wa nje wanalipa kodi, mfumo wa kodi unakuwa wa haki
sawa kwa wote na utaratibu wa kulipa kodi unaasisi mkataba wa jamii wa
kuiwajibisha serikali na kuhakikisha matumizi ya serikali yanaelekezwa kukidhi
mahitaji ya wananchi na kuchochea maendeleo.
No comments:
Post a Comment