Mwenyekiti Cuf Taifa- Prof Ibrahim Lipumba |
Taarifa ya kila mwaka inayotolewa
na taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya World Economic Forum (WEF) kuhusu
ushindani wa kiuchumi wa mataifa(The Global Competitiveness Report 2012/13)
inaonesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 120 kati ya nchi 144 wakati nchi
jirani ya Rwanda imeshika nafasi ya 63.
Nchi inayoongoza kwa ushindani wa
kiuchumi wa mataifa ni Uswissi (Switzerland), ikifuatiwa na Singapore, Finland,
Uswidi (Sweden), Uholanzi (Netherlands), Ujerumani, Marekani, Uingereza,
Hongkong na Japan.
Katika nchi za Afrika inayoongoza
kwa ushindani wa kiuchumi ni Afrika ya Kusini inayoshika namba ya 52,
ikifuatiwa na Mauritius ambayo ni ya 54 na ya tatu ni Rwanda iliyoshika nafasi
ya 63 katika orodha ya nchi 144.
Watafiti wa WEF wanaeleza kuwa
ushindani wa uchumi wa taifa unatokana na asasi za uchumi na utawala, sera,
raslimali na nguvukazi (raslimali watu) zinazobainisha kiwango cha tija katika
uzalishaji wa bidhaa na huduma katika nchi na kwa hiyo kuiwezesha nchi kukuza
uchumi kwa kasi, kuongeza utajiri wa nchi na neema kwa wananchi wake.
Ili kupima ushindani wa kiuchumi
wa kila nchi, watafiti wamechunguza mambo ya msingi yanayochochea ukuaji wa
uchumi na uletaji wa maendeleo kwa ujumla. Nchi zenye ushindani wa kiuchumi
zinafanikiwa kuongeza ufanisi na tija katika uzalishaji wa bidhaa na usambazaji
wa huduma. Zinatumia vizuri raslimali na nguvukazi na kwa hiyo kufanikiwa
kukuza uchumi kwa muda mrefu. Katika ulimwengu wa utandawazi ambapo nchi zina
fursa ya kuuza na kununua bidhaa na huduma katika soko la dunia ushindani wa
kiuchumi ni nyenzo muhimu ya kuongeza kasi ya kukuza uchumi kwa kuvutia
wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Watafiti wa WEF wanaanda
kielelezo (farihisi) cha ushindani wa uchumi wa mataifa. Kielelezo hiki kutunamia
vigezo vingi kupima ushindani wa kiuchumi unaotokana na asasi, sera, raslimali
na vipengele vingine ambavyo vinabainisha uwezo, ufanisi na kiwango cha tija
katika uzalishaji mali wa sekta mbali mbali za uchumi na huduma. Kiwango cha
tija na ufanisi katika uzalishaji ndicho kinachovutia uwekezaji wa ndani na nje
na kuchochochea ukuaji wa uchumi na ongezeko la wastani la pato la kila
mwananchi.
Utafiti wa WEF umebaini nguzo 12
za ushindani wa kiuchumi wa mataifa. Nguzo ya kwanza ni asasi za uchumi,
utawala na sheria ambazo zinajenga mazingira ya kushirikiana katika shughuli za
kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja, kampuni na serikali katika shughuli za uzalishaji
na kuongeza utajiri wa taifa. Umuhimu wa mfumo wa asasi ulio wazi na kufanya
kazi kwa ufanisi na haki umebainika hata kwa nchi zilizoendelea baada ya
mtikisiko na mgogoro wa sekta ya fedha ulioanza Marekani mwaka 2008 na kuikumba
dunia yote. Ukosefu na udhaifu wa usimamizi wa asasi za fedha katika nchi zilizoendelea
na hasa Marekani ndiyo chanzo cha kuporomoka na kuyumba kwa uchumi wa dunia kwa
muda wa miaka minne iliyopita.
Ubora wa asasi za uchumi na
utawala ni jambo la msingi katika ushindani wa kiuchumi wa kila taifa. Mfumo na
utendaji wa asasi hizi ndiyo unaoshawishi uwekezaji wa vitega uchumi na
uzalishaji wa bidhaa na huduma. Mfumo wa asasi ndiyo kigezo muhimu cha mgawanyo
wa pato la taifa na gharama za utekeleza wa mikakati ya kukuza uchumi. Kwa
mfano kuwepo kwa hakimiliki za kuaminika ni muhimu sana katika kushawishi
uwekezaji. Ikiwa mali ya mtu inaweza kuporwa kwaurahisi na watu wengine au
serikali, uwekezaji wa vitega uchumi utapungua.
Ubora wa mfumo wa asasi ni pamoja
na kuwepo utawala bora, ufanisi katika shughuli na usambazaji wa huduma za serikali,
kutokuwepo kwa rushwa, ukusanyaji mzuri wa kodi na uadilifu katika matumizi ya
fedha za umma. Utendaji, ufanisi na maadili ya sekta binafsi yanachangia katika
kujenga ushindani wa kiuchumi wa taifa husika.
Nguzo ya pili ya ushindani wa
kiuchumi ni miundombinu. Miundombinu inayojumlisha usafiri- barabara, reli,
bandari na viwanja vya ndege; ufuaji na usambazaji wa umeme; ugawaji na
usambazaji wa maji; miundombinu ya majitaka, na miundombinu ya mawasiliano
inayoharikisha upeanaji wa taarifa na habari. Ubora wa miundombinu unachangia
sana katika kuongeza ufanisi na tija ili kukuza uzalishaji na kuchochea ukuaji
wa uchumi.
Nguzo ya tatu ni utengamavu wa
uchumi mpana (macroeconomic stability) kwa maana ya mfumko wa bei wa kadri,
riba ziwe za nafuu na pasiwe na tofauti kubwa sana kati ya riba ya mikopo na
riba wanaolipwa waweka akiba, thamani ya
sarafu iwe tengamavu na ya ushindani kwa wazalishaji wa bidhaa na huduma wa
ndani ya nchi, akiba ya kutosha ya fedha za kigeni ya kuagizia bidhaa na huduma
za nje, matumizi ya serikali yasizidi mapato ya serikali kwa kiasi kikubwa.
Utengamavu wa uchumi mpana pekee haukuzi uchumi, bali unajenga mazingira ya
kuvutia uwekezaji na ukuaji wa uchumi ikiwa mambo mengine kama vile miundombinu
na asasi bora vipo. Kutokuwepo kwa utengamavu wa uchumi mpana kunaathiri
motisha wa uwekezaji na uzalishaji kwani kunaweka mashaka makubwa kwa bei
halisi za raslimali, nguvukazi, bidhaa na huduma mbalimbali.
Nguzo ya nne ni afya na elimu
bora ya msingi. Wananchi wenye afya njema wana uwezo wa kufanya kazi kwa
ufanisi na tija ya juu. Wananchi weye afya mbovu siyo wazalishaji wazuri. Afya
duni inaongeza gharama za uzalishaji. Ubora wa elimu ya msingi kwa wananchi
wote inawezesha wafanyakazi waweze kufundishika. Wafanyakazi wasiokuwa na elimu
bora ya msingi na kujua kusoma vizuri siyo wepesi kujifunza teknolojia mpya ya
uzalishaji.
Nguzo ya tano ni elimu na mafunzo
ya juu. Elimu bora ya juu na hususan elimu ya sayansi na teknolojia ni muhimu
kwa nchi zinazohitaji kuzalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu na bidhaa za
teknolojia. Katika ulimwengu wa utandawazi , kuwa na watu wenye elimu ya juu ya
sayansi na teknolojia ni muhimu katika kujenga ushindani wa uzalishaji wa
bidhaa za kisasa.
Nguzo ya sita ni ufanisi wa soko
la bidhaa. Nchi zenye masoko ya bidha yenye ufanisi na ushindani halali
yanavutia uwekezaji na uzalishaji wa bidhaa na huduma bora. Ushindani wa soko
ni muhimu katika kumotisha uvumbuzi na ufanisi katika uzalishaji. Kodi za juu
zinaondoa motisha na kuathiri ushindani wa kiuchumi. Katika soko ambalo wateja
wake wana utamaduni wa kutaka bidhaa bora unasaidia kulazimisha kampuni
zishindane katika kuzalisha bidhaa bora.
Nguzo ya saba ni ufanisi wa soko
la ajira. Ufanisi na mnyumbuliko wa soko la ajira ni jambo la msingi katika
kuhakikisha kuwa watu wanaajiriwa katika nyanja ambazo watakuwa na uzalishaji
wenye tija kubwa kulingana na uwezo na ujuzi wao. Uchumi unaokua kwa kasi kubwa
na kubadilika mfumo wake unahitaji wafanyakazi wapungue kwenye sekta
zinazodidimia au kutoweka kabisa na waongezeke
katika sekta zinazokua kwa kasi. Bila kuwepo kwa mnyumbuliko wa soko la
ajira, mabadiliko ya haraka ya mfumo wa uchumi kama vile kupungua kwa sekta ya
kilimo na kuongezeka kwa sekta ya viwanda, hayawezi kutokea. Soko la ajira
lenye ufanisi linawapa mishahara mizuri wafanyakazi hodari na makini ili kuwapa
motisha wa kuendelea kuchapa kazi. Wafanyakazi wavivu na wazembe wanapata
kipato kidogo ukilinganisha na wafanyakazi hodari. Wafanyakazi wote wanajua
kuwa wakiendelea na uzembe watapoteza ajira.
Nguzo ya nane ni maendeleo ya
soko la mitaji na huduma za fedha. Uchumi wa kisasa unahitaji huduma za mikopo
na mitaji. Ukusanyaji wa akiba kwa ufanisi unaruhusu kuwepo kwa mikopo yenye
riba nafuu. Akiba itumiwe vizuri kuwapa mikopo wazalishaji wenye tija ya juu.
Benki na taasisi nyingine za fedha zina kazi ya kutambua wajasiriamali wenye
miradi mizuri yenye tija na kuwakopesha mitaji. Kuwepo kwa benki na taasisi
nyingine za fedha zinazofanya kazi kwa ufanisi kunachochea ukuaji wa uchumi.
Nguzo ya tisa ni utayari wa
kiteknolojia. Katika ulimwengu wa utandawazi ambapo kuna mabadiliko ya mara kwa
mara ya teknolojia ni muhimu kwa nchi kujenga uwezo wa wananchi na kampuni
zilizomo nchini kupokea, kumudu na kutumia teknolojia mpya. Hivi sasa
teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) imekuwa na matumizi katika nyanja
zote za uzalishaji, elimu, afya na huduma nyingine. Taifa lenye miundombinu ya
TEHAMA na wafanyakazi na jamii inayoweza kutumia TEHAMA ina fursa ya kuzalisha
bidhaa na huduma kwa ufanisi wa juu, kuongeza tija na kukuza uchumi.
Nguzo ya kumi ni ukubwa wa soko.
Ukubwa wa soko unatoa fursa kwa uzalishaji mkubwa unaopunguza wastani wa
gharama za uzalishaji. Nchi zenye soko kubwa la ndani inaweza kuanzisha na
kuimarisha kampuni za uzalishaji kwa kutegemea soko la ndani. Katika ulimwengu
wa utandawazi, soko la dunia linatoa fursa kwa nchi ndogo, kupunguza wastani wa
gharama za uzalishaji kwa kuuza bidhaa na huduma zake kwenye soko la nje ya
nchi. Kwa nchi ndogo kushiriki katika soko la dunia hasa kwa kuuza bidhaa za
viwandani kunaongeza kasi ya kukua kwa uchumi.
Nguzo ya 11 ni kuwepo kwa kampuni
na ufanyaji biashara wa kisasa. Kampuni ndio vituo vya uzalishaji vinavyotumia
teknolojia mpya kuongeza ufanisi na tija. Ubora wa mtandao wa biashara na
kuwepo kwa kampuni za kisasa zenye mikakati na uendeshaji wenye ufanisi
kunaongeza tija na kuchochea ukuaji wa uchumi. Nguzo hii ni muhimu zaidi kwa
nchi zilizo mstari wa mbele katika maendeleo ya uchumi. Klasta (kishada) za
kampuni za kisasa katika eneo moja zinasaidia sana katika uvumbuzi wa
teknolojia mpya za uzalishaji wa bidhaa na usambazaji wa huduma. Klasta ya
bonde la silicon (Silicon Valley), California, Marekani limechangia katika uvumbuzi
mbalimbali wa TEHAMA.
Nguzo ya 12 ni uwezo wa uvumbuzi
wa teknolojia mpya za uzalishaji wa bidhaa na usambazaji wa huduma. Uvumbuzi wa
teknolojia mpya ndiyo unaochochea ukuaji na maendeleo ya uchumi kwa nchi
zilizoko mstari wa mbele wa maendeleo kama vile Marekani, Ujerumani, Japan,
Uswidi (Sweden) Uingereza, Uswissi (Switzerland) na zinginezo.
Nguzo hizi 12 za ushindani wa
kiuchumi wa kimataifa zinahusiana. Nchi ikiwa dhaifu katika eneo moja basi
kutakuwa na uwezekano wa kuwa dhaifu katika maeneo mengine. Kwa mfano uwezo wa
uvumbuzi wa teknolojia hauwezi kuwepo bila kuwa na raslimali watu yenye afya
njema na elimu nzuri na yenye uwezo wa kumudu teknolojia. Mfumo mzuri wa benki
na soko la mitaji unahitajika ili kuhakikisha uvumbuzi wa teknolojia mpya yenye
tija unafikishwa sokoni na kutumiwa katika uzalishaji wa bidhaa na usambazaji
wa huduma.
Umuhimu wa nguzo moja moja kati
ya nguzo zote 12 katika kuongeza ushindani wa kiuchumi wa mataifa na kwa hiyo
kuchochea ukuaji wa uchumi unategemea hatua ya maendeleo iliyofikiwa na nchi
husika. Njia bora ya Tanzania kuongeza ushindani wake wa kiuchumi siyo sawa na
Uswidi kwani Tanzania ni maskini ina miundombinu mibovu na Uswidi iko mstari wa
mbele katika maendeleo ya kiuchumi na teknolojia. Mishahara ya Uswidi ni ya juu
wakati mishahara ya Tanzania ni ya chini na wananchi wachache sana wenye ajira
za uhakika. Watanzania wengi wanategemea kilimo cha kujikimu na sekta isiyo
rasmi.
Ukuaji wa uchumi katika nchi
ambazo ziko chini kimaendeleo kama vile Tanzania kunategemea utumiaji wa ardhi
na maliasili nyingine, na nguvukazi isiyokuwa na elimu na mafunzo ya kutosha.
Kampuni zake zinashindana zaidi kwa bei za bidhaa za kawaida. Katika nchi zilizo
katika hatua ya mwanzo ya maendeleo, ushindani wa kiuchumi unategemea nguzo ya
kwanza ya asasi za uchumi, utawala na sheria, nguzo ya pili ya miundombinu,
nguzo ya tatu ya utengamavu wa uchumi mpana (macroeconomic stability) na nguzo
ya nne ya afya na elimu bora ya msingi.
Kwa kadri nchi inavyoendelea na
kukamilisha matakwa ya nguzo ya kwanza mpaka ya nne ndivyo mishahara
inavyoongezeka , ukuaji wa uchumi utategemea sana ongezeko la ufanisi katika
uzalishaji na kuongeza ubora wa bidhaa. Katika hatua hii ya maendeleo
iliyofikiwa na nchi kama Mauritius, Namibia na Afrika ya Kusini, ongezeko la
tija na ukuaji wa uchumi unategemea nguzo ya tano ya elimu na mafunzo ya juu,
nguzo ya sita ya ufanisi wa soko la bidhaa, nguzo ya saba ya ufanisi wa soko la
ajira, nguzo ya nane ya maendeleo ya soko la mitaji na huduma za fedha, nguzo
ya tisa ya utayari wa kiteknolojia, na nguzo ya kumi ya ukubwa wa soko la ndani na
uwezo wa kushindana katika soko la nje
Nchi zilizo mstari wa mbele
katika maendeleo zinategemea zaidi nguzo ya 11 ya kuwepo kwa kampuni bora na
ufanyaji biashara wa kisasa na nguzo ya 12 ya
uvumbuzi wa teknolojia mpya ili kuongeza ushindani wa kiuchumi. Lakini
nguzo nyingine pia ni muhimu. Kwa mfano miundombinu ya Marekani ikiwa ni pamoja
na barabara na reli zinahitaji ukarabati mkubwa. Vilevile ubora wa elimu ya
msingi na sekondari wa Marekani hasa katika shule za serikali katika maeneo ya
watu masikini umeporomoka sana na unahitaji sera mwafaka ili ubora wa shule
hizi ukaribie shule za nchi nyingine zilizoendelea.
Katika Taarifa ya WEF ya mwaka
2012/13, Rwanda imepanda nafasi 7 na
kuwa ya 63 ukilinganisha na Taarifa ya mwaka 2011/12 ambapo ilikuwa ya 70.
Rwanda inasifika kwa kuwa na asasi imara zinazozuia rushwa. Soko la ajira lina
ufanisi na mnyumbuliko wa kutosha. Mabenki na soko la mitaji yameimarika na
yanafanya kazi nzuri ya kukusanya akiba na kuwekeza vitega uchumi. Rwanda
imewekeza kwenye TEHAMA na kuongeza kwa kiasi kikubwa utayari wake wa
kiteknolojia. Kwa kuwa Rwanda haina bandari, ushindani wake wa kiuchumi
unakwazwa na miundombinu ya nchi jirani ambako inalazimika kupitisha bidhaa
zake.
Tanzania ilikuwa ya 120 katika
Taarifa ya WEF ya mwaka 2011/12 na bado imebakia katika nafasi hiyo katika
Ripoti ya 2012/13. Tanzania iko chini sana katika ushindani wa kiuchumi kwa
sababu ya miundombinu mibovu. Tanzania ni ya 132 kati ya nchi 144 kwa ubora wa
miundombinu. Tanzania bado iko chini katika elimu ya sekondari na elimu ya juu.
Inashikilia nafasi ya 137 kati ya nchi 144. Tanzania pia iko chini sana katika
utayari wa kupokea, kumudu na kutumia teknolojia na hasa matumizi ya mtandao wa
internet ambapo inashikilia nafasi ya 122.
Ili Tanzania iweze kushindana na
kunufaika katika ulimwengu wa utandawazi inahitaji iwekeze katika miundombinu
ya barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege, ufuaji na usambazaji wa umeme,
miundombinu ya maji safi na maji taka TEHAMA na kuboresha elimu ya msingi,
sekondari na vyuo vikuu. Ikiwa Rwanda imeweza kuongeza ushindani wake wa
kiuchumi hakuna sababu kwa nini Tanzania ishindwe kufanya hivyo. Nchi inahitaji
uongozi wenye dira, uadilifu na matumizi mazuri ya fedha za umma kuimarisha
miundombinu na kuwekeza kwenye elimu bora ya vijana. Bila kuimarisha ushindani
wa kiuchumi hatuwezi kuongeza ajira katika sekta za uchumi za kisasa.
No comments:
Post a Comment