Naibu katibu Mkuu JUVICF-Thomas Malima |
Wengi tunaamini kuwa Elimu ni ufunguo
wa maisha. Waandishi wamesomeshwa kwa kodi za watanzania kwa lengo la kupata
elimu ya kuwahabarisha watanzania habari za ukweli na uhakika juu ya
mustakabali wa maisha yao.
Lengo la elimu ni kujenga uwezo
wa mambo makuu matatu kwa kila mwananchi ambayo ni uwezo wa kuhoji au kuuliza,
uwezo wa kujifunza na uwezo wa kujiamini. Katika haya yote mkazo upo katika
ubora na si vinginevyo, yaani kumjenga msomaji hasa mwandishi uwezo wa kufikiri,
kusikiliza, kuuliza maswali, kupambanua na kuwasiliana na jamii bila kupotosha.
Baadhi ya waandishi wa habari
nchini hawana uwezo uliotajwa hapo juu kutokana na kuandika makala zisizo na
utafiti wala umakini kwa umma. Makala iliyoandikwa na mwandishi Mashaka Mgeta
katika gazeti la Nipashe la tarehe 19 Septemba 2012 yenye kichwa CUF INAPOPANDIA
BEHEWA LA CHADEMA ni ya kishabiki na yenye lengo la kuudanganya umma na zaidi
ya yote imemdhalilisha mwandishi huyo pamoja na mhariri wa gazeti hilo kwa kuandika
habari zisizo za utafiti.
CUF ilianza kauli mbiu yake ya
VISION FOR CHANGE mwaka 2008 na kuiweka
rasmi kwenye Manifesto yake ya uchaguzi ya mwaka 2010. Tangu mwaka huo CUF
haikuwahi kubadili kauli mbiu hiyo hadi wakati huu. Lakini cha kushangaza ni
pale CHADEMA walipodandia kauli mbiu hiyo kwa kuzindua Movement for change M4C
mwaka 2011. Ikumbukwe kuwa CUF iliinadi V4C nchi nzima wakati wa kampeni za
uchaguzi za mwaka 2010 lakini leo baadhi ya waandishi wanajaribu kuupotosha umma wa Watanzania kuwa CUF
imedandia M4C ya CHADEMA. Je kwa ushahidi huo kati ya CUF na CDM nani amedandia
hoja ya mwingine?.
Hili si jambo la kwanza kwa CDM
kuiga kutoka kwa CUF. Watanzania watakumbuka kuwa rangi za mwanzo za bendera ya
CHADEMA zilikuwa ni BLUE NA NYEUPE lakini
baada ya kuona bendera za CUF zinavutia na zinaashiria mabadiliko ya kweli
waliziiga na hatimaye kubadilisha bendera ya Chama chao ili zifanane na CUF kwa
lengo la kuwatapeli wanachama na wafuasi wa CUF mikoani kuwa wao na CUF ni kitu
kimoja hivyo wawape ushirikiano kwani wote ni wapinzani wa CCM.
CHADEMA pia waliendelea kuiga kauli mbiu iliyokuwa inatumiwa na viongozi wa CUF
kwenye mikutano yao. Watanzania watakumbuka kuwa kaulimbiu ya mwanzo ya CHADEMA ilikuwa
CHADEMA ……VEMA huku wakinyanyua vidole viwili. Lakini katika mkutano wa CUF
kama chama kikuu cha upinzani kilichokuwa kinalea vyama vingine vidogo ikiwamo
CHADEMA pale Viwanja vya BAKHRESSA mwaka 2004 ndipo aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu
wa CUF Zanzibar mheshimiwa Juma Duni alipozindua kauli mbiu ya NGUVU YA UMMA….CHACHU
YA MABADILIKO. Baada ya mkutano huo ulioshirikisha vyama vingine kama CHADEMA
ndipo Viongozi wa CHADEMA walipoamua kubadilisha kauli mbiu yake kuwa PEOPLES
…..POWER. Iweje leo watu wasahaulishwe ukweli wa nani si mbunifu na nani anayesubiria
mwingine abuni ili yeye aje na kukopi?.
Watanzania watakumbuka kuwa tangu
CUF ilipoanzishwa ilikuwa na hoja ya Tanzania kuwa serikali 3 wakati
CHADEMA ilikuwa inadai serikali ya MAJIMBO. Lakini cha kushangaza leo hii
CHADEMA wamehama katika hoja yao ya Serikali ya majimbo na kuanza kuibaka hoja
ya CUF ya serikali 3. Je hili nalo hamulioni kuwa CHADEMA hawana jipya bali
wanasubiri CUF waibue hoja na wao ndo wanaibukia juu kwa juu?.
Suala mahitaji ya Katiba Mpya
nalo limeonesha kuwa CUF ndicho chama pekee kilicho kinara cha Mabadiliko
nchini maana CUF imesimamia suala hilo
tangu kuasisiwa kwake hadi leo. WanaCUF walifikia hatua ya kufyatuliwa Risasi
za Moto na kuwaangamiza zaidi ya wanaCUF 40 nchi nzima. Lakini leo juhudi hizo
zinaelekea kupotezwa. Ni CUF pekee ndiyo ilikuwa na agenda ya Katiba mpya tangu
1995 lakini CDM imekuja kujitokeza 2010 tu. Je hapa pia hawakudandia hoja ya
CUF ya Katiba mpya?.
Watanzania watakumbuka kuwa
Mwenyekiti wa CUF alipotoka Marekani mwanzoni mwa mwaka huu aliwaeleza
watanzania namna ambavyo rasilimali za nchi hii zikitumika vizuri zinaweza
kuleta mabadiliko na kuwanufaisha watanzania. Profesa Lipumba alisema hayo
baada ya kufanya utafiti kwa muda wa miezi 6 nchini Marekani , ambapo
alipendekeza kuwaomba wapenzi na wanachama wa vyama vya siasa kuchangia vyama
vyao ili vipate nguvu ya kifedha itakayoleta mabadiliko kwa kuingoa CCM. Baada
ya kutoa hotuba hiyo,CHADEMA waliamua kufanya harambee ya kuchangia chama chao
mwanzoni mwa mwezi juni 2012. Cha ajabu CUF waliofanyia utafiti uchangiaji huo,
walipoamua kuweka katika vitendo juzi, wanaCHADEMA wameibuka na kusema CUF
imewaiga. Je, kati ya CUF iliyotumia miezi 6 kutafiti na CHADEMA walioiga baada
utafiti wa CUF nani amedandia hoja ya mwingine?.
Mwisho napenda kutoa wito kwa
watanzania kutambua kuwa kila wanachokiona kinafanywa na CUF leo kimefanyiwa
utafiti wa kina na kuthibitika kuwa kinafaa. CUF itaendelea kuwa baba wa
ubunifu kwa vyama vyingine. CHADEMA wataendelea kuiga kutoka kwa CUF maana
viongozi wake bado ni wababaishaji na wapiga domo tu.
Thomas D.C Malima
Mwandishi wa makala hii ni Naibu Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya vijana ya
CUF-Chama cha Wananchi na anapatikana kwa simu namba 0715172256 na e-mail
thommalima@yahoo.com.
No comments:
Post a Comment