Mwenyekiti Wa Cuf Taifa Prof Ibrahim Lipumba-Wa Pili Kushoto akisoma Tamko,kulia kwake ni Mh Kambaya, kushoto kwake ni Mh Mketo na Mh Chalamila. |
CUF –
Chama cha Wananchi tunalaani mauaji ya mwandishi wa Habari wa Channel Ten kituo
cha Mkoa wa Iringa yaliyofanywa na jeshi la Polisi, ambaye pia alikuwa ni
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoani humo (IPC) Daud Mwangosi
aliyeuwawa kwa kupigwa na bomu (kama inavyosemekana) katika vurugu za kisiasa
baina ya Jeshi la Polisi na Wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) juzi Jumapili, Septemba 2, 2012 katika kijiji cha Nyololo, wilayani
Mufindi mkoani Iringa.
Kwa
mujibu wa taarifa zinazotatanisha zilizotolewa na Vyombo vya Habari pamoja na
kunukuu taarifa za jeshi la Polisi, kuwa Mwandishi huyo aliuwawa kwa mlipuko
akiwa mikononi mwa jeshi hilo la Polisi hadi kupelekea hata Askari Polisi waliokuwa
karibu yake kujeruhiwa na mwengine kukimbizwa Hospitali.
Taarifa
hizo zinazotatanisha zinasema kwamba Mwandishi huyo alikimbilia kwa jeshi la
Polisi kama kujisalimisha hadi kufikia kukumbatiana na OCS aliyekuwepo katika
eneo hilo la tukio hili ni kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, lakini
wakati huohuo vyombo hivyo hivyo vya Habari vinaripoti kuwa Marehemu alikwenda kumtetea
mwandishi mwenzake wa vyombo vya IPP Media na Polisi huyo OCS alikuwa akimuhami
marehemu asiendelee kupata kipigo kutoka kwa askari wenzake kwani alikuwa
akimfahamu, ndipo hapo alipopigwa na mlipuko huo na kutawanya matumbo yake nje.
Tukio kama hili la mauaji kwa raia katika vurugu za kisiasa baina ya
wafuasi wa CHADEMA na Jeshi la Polisi si la kwanza, ukiacha lile lililotokea
siku za nyuma kule Arusha lililopelekea watu watatu kuuawa, tukio jengine la
kusikitisha ni lile lililotokea Agosti 27, Jumatatu ya wiki iliyopita mjini
Morogoro ambapo mtu mmoja alietambulika kwa jina la Ali Nzona (Muuza magazeti)
alieuwawa katika vurugu kama hizo, ambapo taarifa zake zinautata wakati ambapo
CHADEMA wakidai ameuwawa kwa
risasi, taarifa ya Jeshi la Polisi inasema ameuwawa kwa kupigwa na kitu kizito
kichwani.
Inasemekana
kuwa chanzo cha vurugu zote hizi za Morogoro na Iringa, ni kwa sababu Chama cha
Demokrasia na Maendeleo kimekaidi amri ya Jeshi la Polisi kutokukusanyika ama
kufanya maandamano katika kipindi hiki cha zoezi la uandikishaji sensa
likiendelea hadi hapo litakapomalizika ambapo awali lilipangwa limemalizike
Septemba 1, na baadae kuongezwa siku hadi Septemba 8, awali katika makubalino
ya CHADEMA na Jeshi la Polisi kabla ya mkutano huo ni kwamba walitakiwa
waendelee na mikutano yao.
Kwa
mtazamo huu CUF – Chama cha Wananchi tunaona wanaopaswa kubeba lawama hili ni
jeshi la Polisi na wala si CHADEMA, kwani kama tulivyoeleza awali ilitosha
kuheshimu makubaliano yaliyokuwa yamefanyika baina yao, hata kama kulitokea
vurugu haikuhitajika kutumika nguvu kubwa kiasi hiki.
CUF
pamoja na kulaani mauaji hayo yanaendelea kutokea lakini pia tunasikitishwa na
kupotea kwa nguvu kazi ya Taifa kwa sababu zinazoweza kuepukika, ili hali kuna
uwezekano mkubwa kama busara zingetumika kwa pande zote zinazohusika mauaji
kama haya yasingetokea, kwani tunaamini katika vurugu kama hizo zilizotokea
hakuna zoezi lolote la sensa lililoendelea kufanyika katika maeneo hayo husika
kwa wakati huo.
Kama
hivyo ndivyo ilivyo hakukuwa na ulazima wowote wakuzuia watu kukusanyika au
kuandamana, kwani wanaokusanyika na kuandamana sio wote, bado kuna watu watakao
bakia katika makazi yao ambao wangetosha kutoa taarifa za ndugu na jamaa zao
ambao hawapo au hata kuhesabiwa kwa siku zingine kwani zoezi bado linaendelea,
na waandikishaji sensa wangeweza kuendelea na majukumu yao bila hofu wala
vitisho juu usalama wa maisha yao kutokana na vurugu, kama ambavyo ilivyotokea.
CUF – Kwa kipindi kirefu tumekuwa
tukilililalamikia jeshi la Polisi kuwa liache kufanya kazi kwa ukada bali
lizingatie maadili yake ya kazi ambayo ni kulinda usalama wa raia na mali zake,
matukio
kama haya ya jeshi la Polisi yalianza ndani ya chama chetu, ambapo itakumbukwa
mauaji ya kimbari yaliyofanywa na jeshi hilo Januari 26 na 27 mwaka 2001 wakati
tulipokuwa tukidai Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura, Tume Huru ya Uchaguzi na kurudiwa kwa Uchaguzi Mkuu wa
Zanzibar wa mwaka 2000.
CUF Tunamuomba
Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuunda Tume Huru itakayoshirikisha Watetezi wa Haki
za Binadamu, Madaktari, Wakuu Jeshi la Polisi na Upelelezi na Wajumbe wengine
kutoka vyama vya siasa ili kuchunguza mauaji haya yenye taarifa za kutatanisha,
ili kuupata ukweli utakaofanyiwa kazi ya kukomesha mauaji kama haya yasiendelee
kutokea, ambayo tunahisi yataendelea kutokea kama hatua madhubuti
hazikuchukuliwa.
Prof. Ibrahim H. Lipumba
MWENYEKITI
No comments:
Post a Comment