Tuesday, November 6, 2012

Wabunge wataka Serikali tatu

(Kifupi: WAPENDEKEZA MAWAZIRI WASIWE WABUNGE, VITI MAALUMU VIFUTWE, URAIS MIAKA 35)
WABUNGE jana walijilipua baada ya baadhi yao kupendekeza kuwa muundo wa Muungano ubadilishwe kuwa wa Serikali tatu na kwamba, mawaziri wasiwe  wabunge.
Pamoja na mapendekezo hayo, wengine walitaka umri wa kugombea urais ushushwe na kuwa miaka 35, badala ya sasa ya miaka 45.
Wakitoa maoni yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba mjini Dodoma jana, wabunge hao pia walitaka viti maalumu vya ubunge vifutwe, badala yake wanawake warejee kugombea ubunge majimboni.
Katika mkutano huo, zaidi ya wabunge 36 walitumia nafasi hiyo kutoa maoni yao kuhusu masuala mbalimbali yenye masilahi kwa taifa, waliyoona yanafaa kuingizwa kwenye Katiba Mpya, ambayo mchakato wa ukusanyaji maoni ya uundwaji wake, unaendelea.
Muungano
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya alitaka muundo wa muungano ubadilishwe na kuwa wa Serikali tatu, badala ya uliopo sasa aliosema una kasoro nyingi.
Moja ya kasoro hiyo ni wawakilishi kuruhusiwa kuingia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano, huku wabunge wa Bara wakiwa hawana uwakilishi katika Baraza la Wawakilishi.
“Mwenyekiti, tuwe na Serikali tatu katika muungano, vinginevyo kila mmoja abaki na chake," alisema.
Pia alitaka viti maalumu vifutwe, badala yake wanawake wawekewe majimbo ya wilaya, ambayo watagombea na wenzao.
Mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shelukindo naye alitaka muundo wa muungano uwe wa Serikali tatu pamoja na kuruhusiwa kwa mgombea binafsi katika  nafasi mbalimbali.
Alisema kuwa mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wasitokane na wabunge kwa sababu hawataweza kufanya kazi kwa ufanisi na ni mgongano wa kimasilahi.
Mbunge wa Mkanyangeni (CUF), Mohamed Mnyaa alitaka kuwapo na Serikali tatu katika muungano.
Alisema kama Tanzania Bara watakataa kuita nchi yao Tanganyika basi wanaweza kuiita jina lolote hata Mzizima.
“Muungano uwe wa Serikali tatu, Tanganyika wawe na nchi yao na sisi tuwe na Zanzibar yetu, kama bara hawataki kuiita nchi yao Tanganyika basi wanaweza kuiita hata Mzizima,”  alisema.
Kwa upande wake Mbunge wa Chakechake, (CUF), Mussa Haji Kombo alitaka muundo wa Muungano uliopo ubadilishwe badala yake uwe wa mkataba.
Chanzo: mwananchi

No comments:

Post a Comment