Mwenyekiti Wa Cuf Taifa-Prof Ibrahim Haruna Lipumba |
Uchumi wa nchi muhimu zilizoendelea
ikiwemo Marekani, Jumuia ya Ulaya na Japan bado unayumba miaka minne baada ya
mtikisiko mkubwa wa uchumi mwaka 2008. Mtikisiko huo ulisababishwa na sera
mbovu ya usimamizi wa sekta ya fedha ilioruhusu mfumko wa bei za nyumba na
uwekezaji mkubwa katika sekta hiyo. Tufe la mfumko wa bei za nyumba
lilipopasuka na bei hizo kuporomoka, mabenki mengi yalikabiliwa na tatizo la
kufilisika kwa sababu mikopo yao katika sekta ya nyumba haikuweza kulipika na
amana zilizohusiana na sekta ya nyumba ziliporomoka. Familia nyingi zilikopa
kwa kutumia thamani ya nyumba zao kama dhamana. Kuporomoka kwa bei za nyumba
ziliondoa uwezo wa kukopa na kuwalazimisha walipe madeni yao na kwa hiyo
kupunguza matumizi ya kununua bidhaa na huduma. Familia zinapopunguza matumizi
ya kawaida makampuni yanayotengeneza bidhaa na kutoa huduma yanakosa soko na
kulazimika kupunguza uzalishaji wa bidhaa na huduma na kupunguza wafanyakazi.
Watu wa kikosa ajira wanapunguza matumizi na hivyo kuathiri uzalishaji wa
bidhaa na huduma na kuchochea uachishwaji wa kazi wa watu wengi zaidi.
Makampuni yanayoshindwa kuuza bidhaa zao yanapunguza wafanyakazi na yanaacha
kuwekeza vitega uchumi kupanua shughuli zao kwa ukosefu wa soko la bidhaa na
huduma zao. Kupunguza uwekezaji kunaongeza ukosefu wa ajira.
Mahitaji ya soko la bidhaa na huduma
yanapopungua, Benki Kuu inaweza kusaidia kuongeza mahitaji hayo kwa kupunguza
riba. Riba inapopungua gharama za mikopo inakuwa rahisi na kwa hiyo familia na
wawekezaji wanaweza kukopa. Katika mtikisiko wa uchumi ulioanza mwaka 2008,
riba za Benki Kuu zimepunguzwa mpaka kufikia karibu ya sufuri na kwa hiyo
haziwezi kupunguzwa zaidi ya hapo. Uwezo wa sera za riba kusaidia kuongeza
matumizi ya sekta binafsi na kaya umetoweka kwa sababu riba za Benki Kuu
haziwezi kwenda chini ya sufuri. Zaidi ya hapo ikiwa makampuni hayana imani
kuwa kutakuwa na ongezeko la mahitaji ya bidhaa zao, hawewezi kuongeza
uwekezaji hata kama riba ni za chini.
Benki Kuu inaweza kuongeza matumizi ya
kaya na sekta binafsi ikiwa itaonyesha kuwa sera zake zitaongeza mfumko wa bei.
Ikiwa mfumko wa bei ni wa juu, akiba ya fedha taslimu inapungua thamani yake. Watu
watabaini kuwa vyema kununua bidhaa za kudumu kuliko kuweka akiba ya pesa
taslimu. Wachumi wengi wamependekeza sera hii ya kuongeza mfumko wa bei kutoka
asilimia 2 na kufikia asilimia 4. Hata hivyo Benki Kuu nyingi za nchi
zilizoendelea zinaongozwa na mahifidhina wanaoamini kuwa jukumu lao kubwa ni
kuhakikisha mfumko wa bei hauzidi asilimia 2. Hawaikubali kabisa sera
itakayoongeza mfumko wa bei kwa muda ili kuhamasisha sekta binafsi inunue
bidhaa na huduma badala ya kuweka akiba.
Katika hali ya ukosefu wa soko la kuuza
bidhaa na huduma kila kampuni inafanya uamuzi wa busara wa kupunguza matumizi
na uwekezaji. Familia zinazokabiliwa na kupungua kwa utajiri walionao na
kuongezeka kwa madeni wanaamua kupunguza matumizi na kuongeza akiba. Uamuzi wa
familia moja moja na kampuni moja moja una mantiki lakini kwa pamoja kila
familia na kampuni zikipunguza matumizi pato lao la pamoja linapungua kwani
matumizi yako ndiyo mapato ya mwingine. Ili kukabiliana na tatizo hili serikali
ya nchi zilizoendelea zinawajibu wa kuongeza matumizi kuziba pengo lililoachwa
na sekta binafsi. Serikali inaweza kuongeza matumizi kwa kuongeza nakisi ya
bajeti. Sekta binafsi inapokuwa na kipato kidogo, mapato ya serikali ambayo
yanatokana na kodi yanapungua. Kuongeza matumizi wakati mapato yanapungua maana
yake ni kuongeza nakisi ya bajeti na kwa hiyo kuongeza deni la serikali. Sera
ya kuongeza matumizi ya serikali na nakisi ya bajeti ni ya muda mfupi.Uchumi
ukiimarika serikali itakusanya kodi nyingi na pia ina fursa ya kupunguza
matumizi na kwa hiyo kuwa na ziada katika bajeti yake na kupunguza deni lake.
Sera za kuongeza matumizi ya serikali
na hivyo kuwa na nakisi ya bajeti kubwa na kuongeza deni la serikali imepingwa
na wahafidhina. Nchini Marekani Chama cha Republican ambacho kina Wawakilishi
wengi katika Baraza la Wawakilishi kinapinga kuongeza matumizi ya serikali kwa
madai kuwa itaongeza nakisi na kuongeza deni la taifa. Sera za nchi za Jumuiya
za Ulaya, kanda ya euro zinaongozwa na fikra za Serikali ya Ujerumani ambayo
inapinga serikali kuwa na nakisi kubwa ya bajeti. Nchi wanachama wa kanda ya
euro hawana Benki Kuu zao zilizo huru na hawana sarafu zao wenyewe. Hawana
uwezo wa kuongeza nakisi ya bajeti zao bila kuongeza riba. Serikali za nchi za
Ulaya Kusini – Hispania, Italia, Ureno na Ireland wanalipa riba kubwa sana
wanapokopa katika masoko ya fedha. Uingereza ambayo nakisi yake ya bajeti ni
kubwa zaidi ya Hispania inatozwa riba ndogo kwa sababu ina Benki Kuu na sarafu yake yenyewe na kwa hiyo ina uwezo wa
kulipa madeni yake kwa kuchapisha fedha zake kwa wingi.
Hatua za mwanzo za kukabiliana na
mtikisiko wa uchumi mwaka 2008 ulikuwa sahihi. Nchi nyingi ziliongeza matumizi
ya serikali. Kwa sababu ya itikadi za kihafidhina, kuongezeka kwa nakisi ya
bajeti na kukua kwa deni la taifa likaleta mabadiliko ya sera serikali zikaanza
kubana matumizi kabla ya uchumi kutengamaa na sekta binafsi kuimarika. Sera
sahihi ni kuendelea kuongeza matumizi ya serikali katika kipindi cha muda mfupi
na kuweka mpango wa kukabiliana na nakisi ya bajeti na deni la serikali kwa
muda wa kati baada ya sekta binafsi kuimarika na hivyo kuongeza ajira na kodi
za serikali. Misamaha ya kodi kwa matajiri iondolewe wakati wananchi wenye
kipato cha chini na cha kati waendelee kunufaika na misamaha ya kodi katika
kipindi cha muda mfupi mpaka uchumi utakapoimarika.
Baada ya mgogoro wa fedha duniani wa
mwaka 2008, jumla la pato la dunia lilianguka kwa asilimia 0.6 mwaka 2009.
Uchumi wa nchi zilizoendelea ndiyo ulioanguka zaidi. Pato la taifa la Ujerumani
lilianguka kwa asilimia 5.1, Japan na Italia kwa asilimia 5.5, Uingereza
asilimia 4.4 na Marekani kwa asilimia 3.5. China haikuathirika sana na
mtikisiko wa uchumi wa dunia kwa sababu ya hatua zilizochukuliwa na serikali ya
China za kuongeza matumizi kukabiliana na kupungua kwa mahitaji katika soko la
bidhaa. Kasi ya kukua kwa pato la taifa la China ulipungua kutoka asilimia 14.2
mwaka 2007 na kufikia asilimia 9.2. Juhudi za pamoja za kufufua uchumi za Marekani, nchi za Jumuiya
ya Ulaya na nchi zinazoendelea hasa Uchina, India na Brazil zilisaidia kuongeza
ukuaji wa uchumi wa dunia na kufikia asilimia 5.3 mwaka 2010. Lakini kupunguza
kwa matumizi ya serikali na mgogoro wa Euro umepunguza ukuaji wa uchumi na
kufikia asilimia 3.9 mwaka 2011 na makadirio ya 3.5 mwaka 2012.
Nchi za Jumuiya ya Ulaya zinakabiliwa
na mdororo mwingine wa uchumi kwa sababu ya matatizo ya Euro. Pato la kanda ya
Euro linakadiriwa kupungua kwa asilimia 0.3 mwaka 2012. Nchi za Ulaya ya Kusini
– Ugiriki, Hispania, Italia na Ureno ndizo zimeathirika zaidi kwa kuporomoka
kwa uchumi na kuongezeka kwa ukosefu wa ajira. Pato la taifa la Marekani litakua
kidogo tu kwa asilimia 2.1. Ukosefu wa ajira unabakia juu sana zaidi ya
asilimia 8.0.
Inasikitisha kuwa nchi zilizoendelea
zimekumbwa na itikadi ya kihafidhina na wameshindwa kufuata ushauri wa wachumi
wa kimataifa wa kuongeza matumizi ya serikali katika kipindi cha muda mfupi na
kushughulikia nakisi ya bajeti na ukuaji wa deni la taifa katika kipindi cha
muda wa kati. Kususua kwa uchumi wa nchi zilizoendelea kunaongeza matatizo kwa
nchi maskini katika mikakati yao ya kukuza uchumi, kuongeza ajira na
kuutokomeza umaskini. Nchi maskini kama Tanzania inategemea soko la nchi
zilizoendelea kuuza bidhaa zake, wengi wa watalii wanaokuja Tanzania wanatoka
nchi za Ulaya, Wawekezaji wa vitega uchumi wanatoka nchi zilizoendelea na
serikali inategemea misaada na mikopo toka nchi hizo.
Kati karne ya 21 nguvu za uchumi za
mataifa umeanza kubadilika. Uwezo wa kiuchumi wa nchi za magharibi unapungua
ukilinganisha na nchi za Asia. Nchi nyingi zinazoendelea na hasa China
zimeendelea kukuza uchumi wao pamoja na kuathiriwa na mtikisiko wa uchumi wa
nchi zilizoendelea. Nchi yetu inabidi iweke mkakati wa kushirikiana na nchi
zinazoibuka na kuwa na nguvu za kiuchumi kwa manufaa ya nchi yetu lakini
tusigezwe kuwa soko la bidhaa duni toka nchi hizo.
Kwa kuwa nchi yetu iko nyuma katika
maendeleo ya uchumi, tuna fursa nyingi za kutumia elimu, utaalamu na teknolojia
ambayo imeishagunduliwa ili tukuze pato letu la taifa, tuongeza ajira yenye
kipato kizuri, na hatua kwa hatua tuotokomeza umaskini. Ni muhimu kwa
Watanzania tujihamasishe na tuwe na motisha wa kujifunza na kutumia teknolojia
iliyopo tukizingatia mazingira tuliyonayo. Kuna fursa kubwa ya kuongeza
uzalishaji na tija kwa kutumia teknolojia bora katika sekta ya kilimo, mifugo,
uvuvi, misitu, madini, nishati, viwanda, usafiri na mawasiliano, na huduma za
jamii.
Kuwepo kwa fursa za kukuza uchumi
katika sekta mbalimbali hakuna maana kuwa fursa hizo zinaweza kutumiwa
kirahisi. Kuwa na uchumi wa soko na utengamano wa uchumi mpana (macroeconomic
stability), fedha za kigeni kupatikana kwa bei ya soko na kuondoa vikwazo vya
biashara ya nje hakutoshi kuiwezesha nchi kukua kwa asilimia 8-10 kwa muda wa
miaka 20-30 na kuubadilisha mfumo wa uchumi wake kutoka kutegemea kilimo na
sekta isiyo rasmi na kuongeza ajira katika sekta ya viwanda na huduma za
kisasa. Kukua kwa uchumi kwa kasi hiyo
kunahitajika ili kuhakikisha tunautokomeza umaskini.
Tunahitaji sera za maksudi za kuasisi
maendeleo makubwa ya viwanda kwa kuanzia na viwanda vinavyotumia malighafi
inayozalishwa nchini. Kuanzisha na kuendeleza viwanda hakutafanikiwa kwa
kuachia mfumo wa soko peke yake uamue maeneo ya uwekezaji. Juhudi maalum ya
serikali na nidhamu ya hali ya juu ya utekelezaji inahitajika. Serikali
inapaswa kutambua vikwazo vinavyokwamisha maendeleo ya viwanda na kuviondoa.
Miundombinu ya usafiri na umeme ni muhimu kwa maendeleo ya kasi ya viwanda na
uchumi kwa ujumla. Pamoja na kuelewa kuwepo kwa tatizo hili kwa muda mrefu,
inasikitisha kuwa serikali imeshindwa kabisa kutekekeleza mipango yakutatua matatizo
ya miundombinu. Serikali imeshindwa kuweka vipaumbele na kutekeleza miradi
michache ikakamilika kabla ya kuanza miradi mingine.
Serikali imekuwa na mipango mingi isiyo
tekelezwa au kutekelezeka. Kuna Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 ambayo
inalenga kuwa Tanzania iwe ni nchi yenye kiwango cha kati cha mapato (middle
income country) na hali bora ya maisha kwa wananchi. Mpango Maalum wa
Kuharakisha Maendeleo ya Tanzania (Tanzania Mini Tiger Plan 2020) ambao
haijulikani umeishia wapi. Mpango wa
Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania – MKUKUTA I na MKUKUTA II na
Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano 2010-15. MKUKUTA I na MKUKUTA II
hazikufanyiwa makadirio ya gharama za utekelezaji wake. Gharama za mpango wa
miaka mitano ni kubwa mno na serikali haina fedha ya kuugharamia.
Pamoja na matatizo ya uchumi wa dunia, Tanzania inaweza ikatumia
fursa ya kuwa nyuma na kutumia teknolojia iliyopo kukuza uchumi wake. Watanzania
tunahitaji tutafakari hali halisi tuliyonayo na tubuni sera na mikakati ya
pamoja inayotekelezeka ili tujikwamue toka dimbwi la umaskini. Misingi muhimu
ya sera na mikakati hiyo iwe kuitumia vizuri mali ya asili ya Tanzania kwa
manufaa ya wananchi wote huku tukilinda mazingira yetu. Kuwekeza kwenye afya ya
watoto wa Tanzania toka wakiwa katika mimba za mama zao kwa kuhakikisha kina
mama wajawazito na watoto wachanga wanapata lishe bora. Kuwekeza katika elimu
ya watoto wa Tanzania toka shule za chekechea na kuendelea. Kuweka msisitizo
maalum katika elimu ya hesabu, sayansi na teknolojia. Kuwekeza katika kilimo
hasa cha chakula kama vile mahindi, mpunga, maharage, jamii ya kunde na mbegu
za mafuta kukidhi mahitaji ya ndani na kuuza masoko ya nje hasa nchi za jirani.
Kuwekeza katika miundombinu ya barabara, umeme, maji na mawasiliano. Kuweka
mkakati madhubuti wa kuanzisha na kuendeleza viwanda vinavyotumia malighafi ya
ndani na kuajiri watu wengi kama vile viwanda vya nguo na mavazi, viatu na
bidhaa za ngozi, vifaa vya matumizi ya nyumbani na vifaa vya umeme na elektroniki.
Kubuni na kutekeleza mikakati hii Tanzania inahitaji uongozi wenye
dira utakaowaunganisha na kuwahamasisha Watanzania tujielimishe na tutumie
raslimali na mali ya asili ya nchi yetu kuwaletea neema wananchi wote.
No comments:
Post a Comment