Prof Ibrahim Haruna Lupumba-Mwenyekiti Wa Cuf Taifa. |
Mwanzono mwa mwezi wa Agosti nilienda Tabora kumtazama
na kumpa pole shangazi yangu anayeumwa. Hali ya bei ya chakula hasa mahindi
ilinitisha. Kwa kawaida mwezi wa Agosti ni baada ya mavuno. Bei ya mahindi huwa
bado iko chini. Debe la mahindi huwa halizidi shilingi 5000/- Mwaka huu agosti
mwanzoni bei ya debe la mahindi ni shilingi 10000/-. Ifikapa Disemba bei ya
mahindi inaweza kuruka na kufikia shilingi 15000/- au zaidi.
Tathmini ya serikali kama ilivyoelezwa na Waziri wa
Kilimo na Ushirika katika hotuba yake ya bajeti kuwa “ Matokeo ya tathmini ya
awali ya hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula na utabiri wa hali ya chakula
kwa mwaka 2012/2013 yanaonesha kwamba uzalishaji wa mazao ya chakula utafikia
tani 13,572,804 ikilinganishwa na mahitaji ya chakula yanayokadiriwa kuwa tani
11,990,115 kwa mwaka 2012/2013. Taifa linatarajia kujitosheleza kwa chakula kwa
asilimia 113 na hivyo kuwa na ziada ya tani 1,582,690. Tathmini hiyo ilibaini
kuwepo na ziada ya chakula katika mikoa nane (8) ya Iringa, Rukwa, Mbeya,
Kagera, Mtwara, Kigoma, Ruvuma na Morogoro; utoshelevu katika mikoa saba (7) ya
Pwani, Mara, Tanga, Lindi, Mwanza, Singida na Dodoma; na uhaba katika mikoa
sita (6) ya Shinyanga, Tabora, Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Dar es Salaam”
Hali ya bei ya
vyakula katika maeneo mengi ya nchi haionyeshi kuwepo kwa ziada kubwa. Vile
vile hali ya biashara ya mazao ya vyakula ndani ya mipaka ya Tanzania ina
vikwazo. Maeneo yenye ziada hayauzi chakula cha kutosha kwenye maeneo yenye
upungufu. Bei ya mahindi Tabora ingekuwa
ya chini kama wafanyabiashara wangenunua mahindi toka Mpanda mkoa wa Rukwa na
kuyauza Tabora.
Hata katika miaka ambayo chakula kilichozalishwa
nchini kinaonekana kukidhi mahitaji ya taifa, ukosefu wa lishe bora ni tatizo
la muda mrefu. Miaka 50 baada ya uhuru, theluthi moja ya Watanzania ikimaanisha Mtanzania mmoja
katika kila Watanzania watatu hawana lishe bora. Asilimia 44 ya watoto wote
wenye umri wa chini ya miaka 5 wana utapiamlo, ni wafupi kuliko wanavyostaili
kuwa kwa sababu ya kukosa chakula cha kutosha na lishe bora. Watoto wasiokuwa
na lishe bora wanashindwa kujenga kinga ya mwili, maungo yao siyo imara na
hawajengi ubongo wao vizuri na kwa hiyo wanakuwa wagumu kujifunza na kufundishwa. Kuhakikisha kuwa
kina mama wajawazito na watoto wote wanapata lishe bora ni jambo linalopaswa
kupewa kipaumbele na familia, jamii na serikali kwa ujumla.
Hali ya bei ya mazao ya nafaka hasa mahindi katika soko la dunia inatisha. Tathmini ya Waziri wa Kilimo katika
hotuba yake ya bajeti imepitwa na wakati kwani alieleza
kuwa “taarifa ya
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (Food and Agriculture Organisation - FAO) iliyotolewa mwezi Juni
2012, inaonesha kuwa katika mwaka 2011/2012, uzalishaji wa nafaka duniani
unatazamiwa kuongezeka kwa asilimia 3.2. Jumla ya tani bilioni 2.42 za nafaka zitazalishwa
ikilinganishwa na matumizi ya nafaka ya tani bilioni 2.38 kwa mwaka 2012/2013,
matumizi ya nafaka kwa ajili ya chakula cha mifugo yataongezeka kwa asilimia
3.8 wakati matumizi ya chakula yanatazamiwa kuongezeka kwa asilimia moja (1).
Akiba ya nafaka duniani inatazamiwa kuongezeka kwa tani milioni 36 na kufikia
tani milioni 548 sawa na ongezeko la asilimia saba (7) kutoka kiwango cha mwaka
jana.”
Marekani ya Magharibi ya Kati ndiyo eneo linalozalisha
mahindi kwa wingi. Mwezi wa julai mwaka huu ulikuwa na joto kali katika eneo
hili kuliko miaka yote 117 iliyopita tangu kumbukumbu za hali ya joto kuanza
kutunzwa. Marekani kwa ujumla imekumbwa na ukame mbaya kupita yote kwa muda wa
miaka 50. Marekani ndiyo inayoongoza katika kuzalisha na kuuza nafaka katika
soko la dunia. Kwa sababu ya ukame uzalishaji wa mahindi na maharage ya soya
utapungua sana mwaka huu na tayari bei za mahindi na soya zimevunja rekodi ya
bei ya mwaka 2008.
Nchini Marekani na Ulaya mahindi yanatumika sana kama
chakula cha mifugo. Mexico, nchi za Marekani ya kati na Afrika, mahindi ni
chakula muhimu cha binadamu. Nchini Marekani ng’ombe analishwa kilo 30 za
mahindi ili kupata kilo moja ya nyama.
Wamarekani pia wanatumia mahindi kutengeneza ethanol
inayotumiwa kama petroli mbadala. Katika kila majunia 100 ya mahindi
yanayozalishwa Marekani, 40 yanatumiwa kutengeneza ethanol. Mahindi
yanayotumiwa kutengeneza ethanol kujaza tenki la gari ya familia ya Marekani
yanatosha ugali wa mwaka mzima wa mkulima wa Tabora. Utumiaji wa mahindi
kutengeneza ethanol kunaongeza bei ya mahindi katika soko la dunia.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la
Umoja wa Mataifa – FAO, Jose Graziano da Silva ameiomba Marekani kusitisha mara
moja utumiaji wa mahindi kutengeneza ethanol ili kupunguza mfumko wa bei ya
mahindi katika soko la dunia. Katika mwaka wa uchaguzi mkuu, Serikali ya
Marekani haielekei kukubali wito wa Jumiya ya Kimataifa ya kusitisha matumizi
ya mahindi kutengeneza ethanol kwa sababu wakulima wa mahindi wa Marekani ya
magharibi ya kati wanaipenda sera ya kutumia mahindi kutengeneza ethanol kwa kuwa
inaongeza bei ya mahindi. Majimbo yenye wakulima wa mahindi kama vile Iowa ni
muhimu katika mkakati wa Rais Obama na chama cha Democrats kushinda uchaguzi
Novemba 2012.
Kupanda kwa bei ya chakula duniani ni changamoto na
fursa. Bei ya chakula katika soko la dunia
itaendelea kuwa juu kwa muda mrefu kwa sababu ya mahitaji ya nafaka kulisha
mifugo na matumizi ya mazao kutengeneza petroli mbadala.
Kilimo
chetu kimeendelea kuwa duni kwa sababu zisizokuwa na msingi. Tuna ardhi ya
kutosha, mito na maziwa makubwa. Jiografia ya Tanzania inafanya nchi yetu iwe
na majimbo yenye hali ya hewa tofauti. Mazao mbali mbali ya chakula na biashara
yanastawi katika ardhi ya Tanzania, nchi yetu ina uwezo mkubwa wa kuzalisha
mazao ya chakula na biashara kukidhi mahitaji ya ndani na kuuza nchi za nje.
Lakini miaka 50 baada ya Uhuru, Tanzania haijitoshelezi kwa chakula kwa sababu
ya sera na uongozi usiokuwa na dira sahihi ya maendeleo.
Nchi yetu ina
ardhi kubwa inayokubali aina mbambali ya mazao. Tunatumiai robo tu ya ardhi
yote inayofaa kwa kilimo. Ardhi inayolimwa haipandwi mbegu bora. Kati ya
wakulima 100 wa Tanzania, 90 wanatumia mbegu za kienyeji zisizokuwa na uwezo wa
uzalishaji mkubwa. Wakulima wengi hawatumii mbolea. Mfumo wa usambazaji wa
mbegu bora, mbolea na pembejeo nyingine ni hafifu sana. Utaratibu wa mikopo kwa
wakulima wakununulia zana na pembejeo haupo. Chini ya asilimia 1 ya ardhi
inayofaa kilimo cha umwagiliaji imeendelezwa na kutumiwa. Maeneo yenye mfumo wa
umwagiliaji hayatunzwi na kukarabatiwa
na kwa hiyo hayazalishi kwa uwezo wake. Matumizi ya matrekta katika kilimo bado
ni madogo sana. Kwa mfano mkoa wa Kigoma wenye ardhi kubwa, mabonde yenye
rutuba mito na vijito vingi ina matrekta makubwa 25 na matrekta ya mkono 176
tu.
Tanzania imekosa sera sahihi ya
kukuza kilimo na kuinua hali za maisha ya wakulima. Zana za kilimo na pembejeo
haziwafikii wakulima na hata zinapowafikia huwa zimechelewa na kufika nje ya
wakati. Pamoja na serikali kudai kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wetu,
kilimo hakipewi kipaumbele. Tangu tupate uhuru wa taifa letu matumizi halisi ya
sekta ya kilimo ya kila mwaka hayajawahi kuzidi asilimia tano ya bajeti yote ya
Serikali. Nchi yetu haina huduma bora kwa ajili ya kukuza kilimo cha kisasa na
kwa ujumla kumekuwa na udhaifu mkubwa hasa katika maeneo ya uwekezaji kwenye
tafiti, motisha kwa wakulima ili wajaribu mambo mapya, ushauri na utaalamu kwa
wakulima, mikopo ya zana za kilimo na pembejeo, barabara na mawasiliano
vijijini.
Hatua za muda mfupi za
kukabiliana na ongezeko kubwa la bei katika baadhi ya wilaya za Tanzania ni
kuruhusu na kurahisisha biashara ya ndani ya mazao ya chakula. Serikali
irahisishe mfumo wa kodi na ushuru wa mazao ya kilimo; ikiwa ni pamoja na
kufuta ushuru na ada zote za mazao katika ngazi ya mkulima ili kuongeza motisha
kwa wananchi kuwekeza juhudi zaidi katika uzalishaji wa mazao ya kilimo.
Vizuizi vyote visivyo na msingi katika biashara ya mazao yote ndani ya nchi
viondolewe.
Wafanyabiashara wa ndani wapewe
motisha wa kuwekeza katika ununuzi wa nafaka toka maeneo yenye ziada na kuuza
kwenye maeneo yenye upungufu. Sera za serikali katika mazao ya chakula
hazitabiriki. Wakuu wa Wilaya wanaweza kuzuia uuzaji wa nafaka nje ya wilaya
zao. Matokeo yake hakuna wafanyabiashara wa nafaka inayozalishwa nchini wenye
mtazamo wa muda mrefu badala yake kuna walanguzi wenye mtazamo wa muda mfupi.
Hivi sasa serikali ianze
uhamasishaji wa uzalishaji wa mazao yanayokomaa kwa muda mfupi katika maeneo
yanayopata mvua za vuli. Utaratibu mzuri wa usambazaji wa mbegu bora, mbolea na
pembejeo unahitajika. Usambazaji wa vocha za mbolea umejaa ufisadi. Mbolea
inachakachuliwa na haikidhi viwango na kuwapa hasara wakulima.
Wakuu wengi wa wilaya wameteuliwa
kwa upendeleo wa kisiasa na hisia binafsi na hawana uwezo wa kusimamia
maendeleo ya kilimo. Badala yake Wakuu wa wilaya ni vikwazo vya maendeleo ya
kilimo. Wanatoa maagizo na amri zinazowakwaza wakulima. Uteuzi wa Wakuu wa
wilaya na wa mikoa uzingatie uwezo wa kuongoza na kusimamia maendeleo ya
kilimo.
Sera ya Kilimo Kwanza imejikita katika
kuwatumia wakulima wakubwa kuwaendeleza wakulima wadogo wadogo. Hii ni ndoto ya
Alnacha. Wakulima wakubwa wanahitaji ardhi na vibarua. Maslahi ya wakulima
wakubwa yanakinzana na maslahi ya wakulima wadogo wadogo. Kwa kuwa tuna ardhi
ya kutosha wakulima wakubwa wenye mitaji wana nafasi katika kukuza kilimo cha
Tanzania lakini wasitegemewe kuwa ndiyo chachu ya kuwaendeleza wakulima wadogo
wadogo. Sera muafaka kwa Tanzania ni kuhakikisha kuwa wakulima wadogo wadogo
wanashiriki katika kilimo cha biashara cha kuzalisha mazao ya ziada na kuyauza
kwenye soko. Mafunzo kwa wakulima na huduma za ugani kuhusu kilimo cha kisasa
ni muhimu sana. Taaluma ya ubwana na ubibi shamba irejeshewe hadhi yake na
wataalam wa kilimo wapewe motisha ya kufanya kazi yao. Wakulima wapate pembejeo
ikiwa ni pamoja na mbegu bora na mbolea, na zana za kilimo.
Ile ahadi ya serikali za nchi za
nchi za SADC ya kutumia alau asilimia 10 ya bajeti ya serikali katika sekta ya
kilimo itekelezwe. Maeneo muhimu ya kuwekeza ni pamoja na utafiti wa kilimo,
barabara za vijijini na mawasiliano, mfumo wa kilimo cha umwagiliaji maji, usambazaji
wa pembejeo, huduma za fedha za kuweka akiba na kukopa kununulia pembejeo.
Tanzania ina fursa ya kukuza
sekta ya kilimo kwa wastani wa asilimia 8 kwa mwaka kwa muda ya miaka 10 ijayo
ukilinganisha na ukuaji wa wastani wa asilimia 4 katika miaka 10 iliyopita .
Tuna ardhi ya kutosha kukidhi mahitaji yetu ya chakula na kuuza nchi za nje.
Sekta ya kilimo inapokua kwa kasi inachochea ukuaji wa sekta nyingine.
Upatikanaji wa chakula kwa bei nafuu unapunguza gharama za maisha na gharama za
kuajiri wafanyakazi wenye afya njema. Kilimo cha kisasa kinahitaji mbolea,
mbegu bora na utaalamu. Gesi iliyonguduliwa inaweza kutumiwa kutengeneza
mbolea. Kilimo kinahitaji huduma za usafiri – kusafirisha pembejeo na mazao
ambao unaongeza ajira. Mazao ya kilimo ni malighafi katika viwanda vya
kusindika nafaka, matunda, maziwa na nyama. Viwanda vya nguo na bidhaa za ngozi
vinatumia malighafi inayozalishwa na kilimo. Kipato cha wakulima kinapoongezeka
wananunua bidhaa za viwandani kama vile nguo, vyombo vya nyumbani, samani,
mabati, saruji na vifaa vinginevyo. Mapinduzi ya kilimo yatachochea ukuaji wa
sekta ya viwanda na kuongeza ajira katika sekta rasmi.
Ili kuasisi mapinduzi endelevu ya
kilimo yatakayomsaidia mkulima wa kawaida Tanzania inahitaji uongozi wenye
dira. Serikali ya CCM imewasaliti wakulima wa Tanzania na kuwaongezea umaskini.
Jukumu muhimu la wanaharakati wa dira ya mabadiliko ni kuwaelimisha na
kuwahamasisha wakulima washiriki kikamilifu katika mabadiliko ya kisiasa
yatakayoasisi mapinduzi ya kilimo yatakayowanufaisha Watanzania wote.
No comments:
Post a Comment