Wednesday, August 8, 2012

JUVICUF YATOA POLE KWA WANAFUNZI NA WAZAZI WA SHULE YA SEKONDARI YA MOROGORO

Naibu Katibu Wa JUVICUF
JUMUIYA ya Vijana  wa Chama Cha Wananchi-CUF (JUVICUF) inapenda kutoa pole kwa wanafunzi , wazazi na walimu wa Shule ya Sekondari ya Morogoro (Wasichana) kutokana na ajali ya moto iliyowakumba kwa baadhi ya majengo yake yakiwemo mabweni ya wanafunzi kuungua na kuteketetea kwa moto uliotokana na hitilafu ya umeme na kusabaisha zaidi ya wanafuzi 600 kuathirika kwa namna moja au nyingine.
JUVICUF inatambua kuwa japokuwa hakuna aliyepoteza maisha lakini wanafunzi wamepoteza masomo, mali, na wamekubwa na athari za kisaikolojia wakati wote wa ajali na baada ya ajali. Tunatambua nafasi yenu kama vijana wa Tanzania katika ujenzi wa Taifa lenu na mmepata ajali hii mkiitafuta elimu ili muijenge nchi yenu vizuri. Ni kutokana na umuhimu huo, ndio maana JUVICUF inaungana nanyi katika kipindi hiki cha matatizo.

JUVICUF inakubaliana na taarifa za awali za Jeshi la Polisi, wanafunzi na walimu wa shule hiyo kuwa  ajali hiyo ilitokana na miundombinu mibovu ya umeme shuleni hapo. Na kwa kuwa tatizo hili haliko katika shule ya Sekondari ya Morogoro(wasichana) pekee bali ni kwa zaidi ya shule 50 kongwe hapa nchini. Hii ni kwa sababu ya serikali kushindwa kuzipangia bajeti ya kutosha ya ukarabati kila mwaka. Shule hizi zilijengwa kabla na mara tu baada ya uhuru lakini hazifanyiwi ukarabati kabisa.

JUVICUF inaitaka serikali ifanye utafiti wa kina kwa shule zote za zamani kutokana na uchakavu mkubwa  wa miundombinu ya umeme na maji katika mazingira yake. Shule nyingi ziko taabani kwani majengo yake yamezeeka, miundombinu ya maji safi na majitaka pamoja na miundombinu ya umeme vimezeeka na kuharibika kabisa kiasi cha kuhatarisha afya na uhai wa wanafunzi na walimu wao.

Pia JUVICUF inaitaka serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais (Maafa) iangalie namna ya kuwawezesha wanafunzi hao waliopoteza nguo na vifaa vyao vya kusomea wapate nguo na vifaa vya kusomea ili waendelee kusoma bila matatizo wakati huu wa matatizo bila kuathiri ratiba za masomo yao ya kila siku.

Na ni wajibu wa serikali kuwahudumia  kimatibabu wanafunzi wote waliopatwa na majeraha pamoja mshituko wakati wa ajali hiyo ya moto shuleni hapo bila kuhitaji malipo kutoka kwa wazi/walezi wa wanafunzi hao. Hili ni jukumu la serikali siyo hisani kwao. Kwa hiyo tunaitaka serikali igharimie matibabu yao.

Leo tukio hili limetokea Morogoro Sekondari (Wasichana), kesho tukio kama hili linaweza likatokea shule nyingine na kuleta maafa makubwa. Kwa hiyo lazima serikali iwe makini kuzuia majanga kabla ya

kusubiri kuokoa pindi majanga yanapotokea. Lazima tuwe makini kulinda maisha ya vijana wetu hata kwa gharama kubwa maana ndio tegemeo letu kwa maendeleo ya Taifa letu. Ni heri kulinda maisha na ustawi wa watu wako kwa gharama kubwa kuliko kusubiri kuwaokoa kwa gharama kubwa.

JUVICUF inatambua athari kubwa zinazoweza kujitokeza endapo serikali haitakuwa makini na uboreshaji wa miundombinu ya shule zakekwani zinawakutanisha wanafunzi wengi katika mazingira mabovu yanayoweza kusababisha magonjwa ya milipuko, hitilafu za umeme au janga la aina yoyote ile.

JUVICUF inawapa pole na kuungana na wanafunzi hao pamoja na wazazi wao kwa kuwaomba wawe wavumilivu katika kipindi hiki cha matatizo.
Imetolewa na:
Thomas D.C Malima
Naibu Katibu –TAIFA
JUMUIYA YA VIJANA YA CUF (JUVICUF)






No comments:

Post a Comment