SOMA MAKALA YAKE YENYE KICHWA CHA HABARI
PROFESSA LIPUMBA NI MBUMBUMBU WA SHERIA,ACHA SHERIA ICHUKUE MKONDO WAKE
NA HAPPINESS KATABAZI
KWA mara ya pili sasa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi
(CUF), Professa Ibrahim Lipumba amekuwa akiitisha mikutano na waandishi wa habari
kuzungumzia vurugu za kidini zilizotokea hapa nchini hususani jijini Dar es
Salaam.
Profesa Lipumba pamoja na mambo mengine amekuwa akisema tena
kwa ujasiri kuwa kesi ya jinai namba 245/2012 inayomkabili Sheikh Issa Ponda na
wenzake 49 iliyofunguliwa na upande wa jamhuri Oktoba 18 mwaka huu, ambayo ipo
mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Victoria
Nongwa na inendwa na wakili mwandamizi wa serikali Tumaini Kweka wakati upande
wa utetezi unatetewa na wakili wa kujitegemea Mansoor Nassor ilipaswa iwe ya
madai na siyo jinai na kwamba eti Ponda alistahili dhamana na kuwa anafanya
mpango wa kukutana na Rais Jakaya Kikwete amshauri serikali ifanye mazungumzo
na Maimamu wa misikiti ili waweze kupata suluhu ya tatizo la vurugu hizo za
kidini.
Binafsi ni mwandishi wa habari za mahakamani hapa nchini na
kesi hii ni miongoni mwa kesi ambazo minaziudhulia siku ilipofunguliwa kwa mara
ya kwanza ,na hata Novemba Mosi mwaka
huu,kesi hiyo ilipokuja kwaajili ya kutajwa na wakili wa serikali Kweka
aliieleza mahakama kuwa uplelezi wa shauri hilo umekamilika nilikuwepo tangu
saa moja asubuhi mahakamani hapo, na hata
hiyo Novemba 15 mwaka huu, panapo
majaliwa ya mwenyezi mungu kesi hiyo itakapokuja kwaajili ya upane wa jamhuri
kuwasomea maelezo ya awali washitakiwa nitakuwepo ndani ya ukumbi namba moja wa
mahakama hiyo kwaajili ya kuiripoti kesi hiyo kwa uweledi wa aina yake.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka ya kesi hiyo inayomkabili
Ponda na wenzake ambayo nakala yake ninayo, ina jumla ya mshitaka matano ambapo
mashitaka yote matano yanamkabili Ponda na mashitaka manne yanamkabili
mshitakiwa 2-50.
Kosa la kwanza ni la
kula njama kutenda kosa kinyume na kifungu cha
384 cha Sheri ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, ambapo washitakiwa wote
wanaidaiwa kuwa Oktoba 12 mwaka huu katika eneo la Chang’ombe Marksi walikula njama kwania ya kutenda
kosa.Kosa la pili ni kuingia kwa
nguvu kwa nia ya kutenda kosa kinyume na kifungu cha 85,35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu
,kuwa Oktoba 12 mwaka huu, katika eneo
la Chang’ombe Markasi ,kwa jinai na wasipokuwa na sababu waliingia kwenye kiwanja cha eneo hilo
kinachomilikiwa na Kiwanda cha Agritanza.
Wakati kosa la tatu ni
la kujimilikisha kwa jinai kiwanja hicho kinyume na kifungu cha 86 na 35
cha Sheria hiyo kuwa kati ya Oktoba
12-16 mwaka huu, katika eneo hilo pasipo na uhalali washitakiwa wote katika hali ya kupelekea uvunjifu wa
amani,walijimilikisha kwa nguvu ardhi ya
kampuni ya Agritanza.
Shitaka la nne ni la wizi kinyume na kifungu cha 258 na 225
cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka
2002 kuwa washitakiwa wote kati ya
Oktoba 12-16 mwaka huu, waliiba vifaa,malighafi
kama nondo,matofali ,kokoto zenye jumla ya Sh 59,650,000 mali ya Kampuni
hiyo.
Aidha shitaka la tano ni kwaajili ya Ponda peke yake ambalo
ni la uchochezi kinyume na kifungu cha 390 na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu
ya mwaka 2002 kuwa Oktoba 12 katika eneo hilo la Chang’ombe kwa maelezo kuwa yeye ni Katibu aliwashawishi wafuasi wake ambao ni
washitakiwa hao watende makosa hayo.Na washitakiwa wote walikanusha mashitaka hayo
na Hakimu Nongwa akasema mashitaka yote yanadhamana kwa mujibu wa sheria na akatoa
masharti ya dhamana kwa mshitakiwa 2-50 .
Na kusema ili wapate dhamana nilazima kila mmoja awe na
mdhamini mmoja wa kuaminika atakayesaini bondi ya milioni moja, licha Hakimu
Nongwa alisema mahakama yake haiwezi kutoa dhamana kwa Ponda licha anastahili
dhamana kwasababu Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP),Dk.Eliezer Feleshi aliwasilisha
mahakamani hapo hati ya kufunga dhamana ya Ponda kwa mujibu wa kifungu cha
148(4) cha Sheria Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002.Na hati hiyo ya DPP
inakuwa imeifunga mikono mahakama hadi hapo siku DPP atakapoona haja ya
kuiondoa hati hiyo hivyo Ponda ataendelea kusota rumande hadi hati hiyo
itakapoondolewa na DPP .
Kauli ya Profesa Lipumba kuhusu kesi ya Ponda imenifanya
nianze kuamini kuwa hata ukiwa msomi wa hali ya juu kama Profesa Lipumba
unaweza pia kutoa maoni ya kipuuzi ambayo hayapaswi kutolewa na msomi wa aina
yake mbele ya umma.
Tumuulize huyu Lipumba kabla ya kutoa kauli hizo
aliwasiliana na wanasheria wa chama chake wakampa ushauri wa kisheria wa nini
cha kuzungumza mbele ya umma kuhusu kesi ya Ponda inayooendelea pale katika
Mahakama ya Kisutu?Naamini hakupata ushauri
mzuri toka kwa wanasheria wa chama chake au kama alipata basi wanasheria
huo waliamua kumpatia ushauri ambao umemdhalilisha Lipumba mbele ya jamii ya
wasomi wa sheria na jamii inayoheshimu utawala wa sheria hapa nchini.
Profesa Lipumba kwanza kabla ya kutoa kauli hizo kuhusu kesi
ya Sheikh Ponda kuwa kesi hiyo ya jinai namba 245 /2010 eti ilipaswa iwe ya
jinai, ungeitafuta hati hati ya mashitaka ungeisoma vizuri na ungeweza kuelewa
makosa wanayoshtakiwa nayo ni ya madai au jinai
halafu ungeenda kuisoma Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal
Code;2002),Sheria ya Mashauri ya Madai(Civil Procedure Code:2002) na Sheria ya
Mwenendo wa Makosa ya Jinai (Criminal Procedure Act, RE:2002) na Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naamini vingekupa mwongozo mzuri sana kwa
kufahamu mashitaka yanayowakabili, kifungu gani kimetumika kufunga dhamana ya
Ponda na ni kwanini dhamana yake imefungwa na pia ungeweza kufahamu vyema
majukumu ya mahakama ni ya pili nay a serikali ni yapi.
Na hapo ndipo ninapokubaliana na kauli ya Rais Kikwete
aliyoitoa mwishoni mwa wiki ambayo
inawataka wanasiasa waache unafki kwani wao wanaisasa wanaishi maisha kifahali
na uhuru wakati wale wafuasi wao wanaishi maisha ya tabu na wamekuwa
wakiwapandikisha uongo wafuasi wao.
Sasa kwa kauli hiyo ya Kikwete minaona katika matamko hayo
ya Lipumba inamgusa pia, kwani uenda Lipumba anataka kujipatia umaarufu chee wa
kisiasa kupitia kesi ya Ponda ila hafahamu kuwa mahakama haiendeshwi wala
haisikilizi kauliza wanasiasa pindi
inapofanyakazi zake kwa mujibu wa sheria.
Wewe Lipumba kwakuwa unasema kesi ya jinai ya Ponda ilipaswa
iwe ni ya madai, hivi ni kwanini unashindwa kuomba kazi ya kuwatetea
washitakiwa hao kama (Bush Lawyer )mahakamani hapo na siku kesi ikianza
kusikilizwa ukawasilisha hilo pingamizi lako lakutaka kesi hiyo ya jinai ifutwe
kwani imefunguliwa kimakosa ilitakiwa washitakiwa hao wafunguliwe kesi ya
madai).
Maana unapozungumzia kesi hiyo kwenye majukwaa na mbele ya
waandishi wa habari haimsaidii Ponda kwa lolote zaidi zaidi unazidi
kumgandamiza Ponda bila wewe kujua?
Profesa mzima tena wa uchumi unayeheshimika nchi mbalimbali
unashindwa kufahamu mtu anayetuhumiwa kwa kosa la wizi au kuingia kwa nguvu
kwenye kiwanja au chochezi basi mtu huyo makosa hayo yataangukia kwenye jamii
ya makosa ya jinai? Lakini wewe sijui kwa upotoshaji au unalako jambo unadiriki
kujitokeza adharani kuuposha umma kwa kusema walipaswa washitakiwe kwa kesi ya
madai?
Mwenyekiti mzima wa chama kikubwa kama CUF,ambacho chama
hicho chini ya uongozi wako ni miongoni mwa chama kilichokuwa kidai Tanzania
iandike Katiba mpya kwa madai kuwa Katiba ya sasa imepitwa na wakati,na kwa
maana hiyo unaifahamu vyema ibara za Katiba hiyo , unashindwa kuifahamu Katiba
ya nchi ambayo Ibara ya 59B(1) inayosomeka
hivi; “Kutakuwa na Mkurugenzi wa Mashtaka
ambaye atateuliwa na Rais,kutoka
miongoni mwa watu wenye sifa zilizoanishwa katika ibara ndogo (2) ya ibara 59 na amekuwa
na sifa hizo mfululizo kwa muad
usiopungua miaka kumi.
Ibara ya 59(4) inasema; ‘Katika kutekeleza mamlaka yake,Mkurugenzi wa Mashitaka atakuwa huru ,hataingiliwa na mtu yeyote
au mamlaka yeyote na atazingatia mambo yafuatayo; (a) nia ya kutenda haki,
kuzuia matumuzi mabaya ya taratibu za
utoaji haki na maslahi ya umma.
Na kifungu cha 148(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya
jinai, kina mpa mamlaka DPP kufunga dhamana ya mshitakiwa na ndiyo kifungu
hicho kilichotumia na DPP kufunga dhamana ya Ponda.
Ni kweli dhamana ni haki ya kila mtu ila kuna baadhi ya
makosa hayana dhamana na mfano kesi ya mauji, utakatishaji fedha haramu( Money
Laundry),unyang’anyi wa kutumia silaha(Amry Robbery) mauji,uhaini na ugaidi
(Terrorisms) lakini kama kifungu hicho
cha 148(4) cha Sheria ya Makosa ya Jinai, kinampa mamlaka DPP kumfungua dhamana
mshitakiwa anayekabiliwa na makosa yanayodhaminika.
Sasa kwa mtiririko huo ,misimwelewi Lipumba ana ajenda gani
iliyojificha kwenye hii kesi ya Ponda.Kwani Ponda na wenzake bado ni watuhumiwa
kama wengine tub ado hajaukumiwa.DPP ametumia madaraka aliyonayo kufunga
dhamana ya Ponda na kuwafungulia
mashitaka ya jinai washitakiwa hao ,sasa sijui tabu inatoka wapi.
Mbona viongozi wa iliyokuwa Taasisi ya Upatu (DECI)
walivyofunguliwa kesi pale Mahakama ya Kisutu mwaka 2009, na makosa
yanayowakabili yalikuwa yanadhaminika kwa mujibu wa sheria lakini DPP huyu huyu Dk.Feleshi aliwasilisha hati ya
kuwafungua dhamana na vigogo ambao kesi yao iliyopo mbele ya Hakimu Stewart
Sanga imefikia hatua ya wao wameanza kujitetea,aliwafungia dhamana na walisota
gerezani kwa zaidi ya miezi mitatu, mbona hatukuwasikia wanasiasa wala waumini
wa dini ya Kikristo au wewe Lipumba na wale wafuasi wengine mnaondamana kila
Ijumaa kushinikiza Ponda aachiliwe huru, hamkuandamana kushinikiza waachiliwe
huru na kwamba kesi yao vigogo wa DECI ni ya madia?
Tuachane na uhuni huu unaofanywa na wasiasa waliopoteza dira
na mwelekeo na waliofirisika kisiasa ambao wao masuala hatarishi na
yanayoingilia uhuru wa mahakama ambao uhuru wa mahakama umeainishwa wazi katika
Ibara ya 107B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,
ambayo inasomeka hivi; “Katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki ,mahakama zote
zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia
tu masharti ya Katiba na Sheria za Nchi’.
Na ibara 107A (1) ya Katiba ya nchi inasema “Mamlaka yenye
mamlaka ya mwisho ya utoaji haki katika
jamhuri ya Muungano itakuwa ni Mahakama.
Kwahiyo kama kesi
inayomkabili Ponda ni ya madai , si jukumu la wewe Lipumba sasa kusema hilo ni
jukumu la Mahakama siku ikifika itasema hivyo.
Mwisho napenda kuwaasa wale wanaojiita wafuasi wanaojiita
wao ni wafuasi wa Ponda na sheikh Farid
waache kushiriki kwenye vitendo vya uvunjifu wa amani kwa kisingizo cha kuishinikiza
serikali na mahakama imwachilie huru Ponda kwani kufanya hivyo ni wazi wakae
wakijua watakuwa wanafunja sheria za nchi watajikuta wanaingia matatani na wao
waishia kwa kufunguliwa kesi za jinai mahakamani na kutupwa jela.
Na wale wahuni wachache ambao ni wazi wamechoka kuishi
Tanzania kwenye amani wanaoleta vurugu za kidini kwa kisingizio eti wanaitetea
dini ya kiislamu, wakome mara moja na kwa uwezo wa mungu hiyo dhamira yao mbaya
na kishetani ya kutaka kuingiza Tanzania kwenye machafuko haitafanikiwa nao
mwisho wa siku wataambulia kipigo kutoka kwa wanausalama wetu na kufikishwa
mahakamani na mwishowe kupelekwa kupumzika katika gereza la Segerea,Keko na
kula ugali wa bure na kuwa chini ya ulinzi.
Naendelea kuvipongeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa
kazi nzuri wanayoifanya ya kuwadhibiti wahuni hawa wachache wanajaribu kutaka
kuatarisha usalama wa taifa letu kwa visingizio visivyokuwa na kichwa wala
miguu.Na ninaviomba vyombo vya dola viwashughulikie kikamilifu wale wote
wanaoleta vurugu kwa kisingizio cha kutetea dini ya kiislamu wakati bado
wakristo,waislamu na wapagani hapa nchini tunaishi kwa upendo,tunafanyakazi
pamoja.
Mwisho nimalizie kwa kuwataka waandishi wa habari wenzangu
na wanaharakati na wanasiasa ambao huko nyuma tulikuwa mstari wa mbele sana
kushikilia bango hadi kuandaa maandamano na kutengeneza mabango na fulani za
kulaani tuhuma za ufisadi katika Mkataba wa Dowans,Richmond, mauji ya
mwanahabari mwenzetu David Mwangosi,kufungiwa kwa vyombo mbalimbali vya habari.
Mbona wanahabari wenzangu wengi,wanaharakati,na wanasiasa
machahari mbona tumeonekana kuwa wapole sana katika matukio haya yanayotaka
kuleta chochoko za kidini?
Hivi je
matukio haya yanayoashiria chokochoko ya udini siyana madhara ya haraka,wazi
ambayo yasingezibitiwaharaka na vyombo vya dola na hekima ya viongozi wa dini
ya Kikristo na wale wa kiislamu leo hii Tanzania ingekuwa imeingia kwenye
machafuko ya kidini?
Tuache unafki,amani ni kitu muhimu sana pote pale duniani na
chenye kipaumbele halafu hayo mambo mengine yanafuata.Kwani bila ya kuwepo na
amani huo ufisadi usingenyika.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika
0716 774494
Mwisho wa makala yake, chadema wanasemaje juu ya kadhia hiyo?
Chadema waweka bayana msimamo wao juu yaliowasibu ma-shiekh
Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimekutana na waandisihi wa habari
makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam leo, ambapo wajumbe wa
Kamati Kuu, Profesa Abdallah Safari na Mabere Marando, wameweka waziwazi
msimamo wa chama hicho kuhusiana na mgogoro kati ya waislamu na
serikali na kukamatwa kwa Sheikh Farid huko Zanzibar.
Wanasheria hao wa CHADEMA wamesema kuwa kitendo cha serikali kumnyima
dhamana Sheikh Ponda ni kinyume cha katiba na kwamba Chadema kama chama
kinachojiandaa kuchukua dola, hakiwezi kuvumilia kuona haki za raia
zikivunjwa.
“Tunaweza kuwa miongoni mwetu, wapo watu wanaomchukia Sheikh Ponda,
lakini hatuwezi kuficha ukweli kwamba Sheikh Ponda kama raia wa Jamhuri
ya Muungano au mkazi wa Jamhuri hii, anayo haki ya kusikilizwa na kupewa
dhamana. Makosa ambayo Sheikh Ponda ameshitakiwa yanadhaminika kwa
mujibu wa sheria, hivyo ni makosa kwa serikali kufanya hila kumnyima
dhamana kiongozi huyu wa kidini,” ameeleza Marando katika mkutano huo.
Marando alifika mbali zaidi kwa kusema tatizo lililopo sasa kati ya
serikali na waislamu, limetokana na hatua ya serikali kuwalazimisha
waislamu wote kuwa waumini wa Bakwata, chombo ambacho wengi wanakiona
kinatumika kuwakandamiza.
Naye Profesa Safari alionya matumizi ya nguvu za kijeshi yanayotumiwa
na serikali kwa kisingizio cha kulinda amani, huku akieleza kuwa
matumizi ya kijeshi siyo suluhu ya kutatua matatizo yaliopo.
Kuhusu kukamatwa kwa Sheikh Faridi na kumzuia kwa siku tatu, wanasheria hao wamesisitiza kuwa kitendo hicho hakikubaliki.
“Kitendo cha kumkamata na kumshikiria Sheikh Faridi, huku serikali na
vyombo vyake vikisema havihusiki, wakati ukweli ni kuwa alikuwa
anashikiliwa na watu wa USALAMA wa TAIFA, ni uharamia mkubwa unaopaswa
kulaaniwa na wote wanaolitakia mema taifa hili,” ameeleza Marando.
Kuhusu uvunjwaji wa makanisa, Profesa Safari amesema CHADEMA
kimelaani hatua hiyo iliyotokana na wananchi kujichukulia sheria
mkononi. Amewataka waislamu kuvuta subira.
Hata hivyo, Profesa Safari amesena matatizo yanayotokea sasa,
yameletwa na CCM kutokana na hatua yao ya kuwatumia baadhi ya waislamu
kupandikiza mbegu ya udini nchini.
Chanzo Chadema Blog
Mwisho wa msimamo wa chadema, unaofuata ni msimamo wa cuf uliotolewa na Prof Ibrahim Haruna Lipumba.
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF –Chama Cha Wananchi) TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU JUHUDI ZA CUF ZA KUENDELEZA AMANI NA UTULIVU BAADA YA SALA YA IJUMAA TAREHE 2 NOVEMBA 2012
Siku ya Alhamis nikielekea Muhimbili kumpeleka shangazi yangu hospitali
nilipata taarifa kuwa Imam wa msikiti wa Masjid Haq (ulioko jirani na
Afisi Kuuya CUF na ambapo nasali sala ya Ijumaa nikiwa Afisi Kuu) na
watu wengine watatu akiwemo Sheikh Ramadhan S. Sanze (ambaye namfahamu
kwa muda mrefu). Sadik Gogo na Mzee Abdillah wamekamatwa na wamefikishwa
kituo cha polisi cha kati (Central Police Station). Nilistushwa na
kamata kamata hiina nikahofia kuwa inaweza kuongeza jazba miongoni mwa
waumini wa Kiislam. Baada ya shangazi kupata tiba katika hospitali ya
Muhimbili nilimrudisha nyumbani na nikampigia simu Mkurugenzi wa Haki za
Binadamu na mahusiano ya umma, Abdul Kambaya, tukutane kituo cha polisi
cha kati kuulizia sababu za kukamatwa Imam wa MasjidHaq na wenzake
watatu na kama tunaweza kuwawekea dhamana.Tulipof ika kituo cha polisi
tulibaini kuwa Imam wa Msikiti wa Masjid Haq hajakamatwa bali kuna
muumini mwingine kwa jina la Mkadam Swalehe ndiye aliyekamatwa.
Tulizungumza na RPC Kova na RCO Msangi kuhusu kuachiliwa kwa wale
waliokamatwa. Tukafahamishwa kuwa itabidi wafanyiwe mahojiano na baadaye
wataachiliwa isipokuwa Mkadam Swalehe ambaye ana faili jingine pale
polisi linaloendelea kufanyiwa upelelezi. Tulifahamishwa kuwa nitume mtu
saa 10:30 jioni ili aweze kufuatilia utaratibu wa kuachiliwa watuhumiwa
watatu akiwemo Sheikh Ramadhan Sanze, Sadik Gogo na Mzee
Abdillah.Nilish auriana na Wakurugenzi wa CUF walioko Dar es Salaam na
Naibu Katibu Mkuu, Julius Mtatiro hatua za kuchukua. Taarifa za
kukamatwa Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake zilikuwa zinaenea na
kupandisha jazba ya Waislam wengi. Tulipata wasiwasi kuwa jazba hii
inaweza kupelekea Waislam wengi kuandamana baada ya sala ya Ijumaa.Ikiwa
Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake wataachiwa na Waislam wakapata taarifa
hiyo inaweza kusaidia kupunguza jazba na watu wasishiriki maandamano
baada ya sala ya Ijumaa.Nilimpa jukum Abdul Kambaya afuatilie Central
PoliceStation, suala la kuachiliwa Sheikh Sanze na wenzake.
Niliwasiliana naye kwa simu na kuzungumza na RCO na nikaamini kuwa
Sheikh Ramadhan Sanze, Sadik Gogo na Mzee Abdillah wataachiwa baada ya
kukamilishamaho jiano. Ilikuwa inakaribia saa 12 jioni. Muda wa kuitisha
Press Conference haukuwepo. Tukakubaliana Naibu Katibu Mkuu awasiliane
na wahariri wa habari wa vituo vya televisheni Channel10, TBC1, Star TV,
Mlimani TV na ITV ili niweze kutoa taarifa ya kuwasihi Waislam warudi
majumbani na kwenye shughuli zao baada ya sala ya Ijumaa. Niliweza
kufanya mahojiano na Channel 10, TBC1, na ITV. Kwa bahati mbaya Camera
person wa Star TV alikuwa kwenye shughuli nyingine na kwa hiyo sikuweza
kufanya mahojiano na Star TV. Vilevile wapiga picha wa Mlimani TV
hawakuwepo kwenye studio. Pia nilipatabahati ya kuzungumza na Radio Iman
inayosikilizwa na Waislam wengi na kueleza maoni yangu kuwa Waislam
wasiandamane baada ya sala ya Ijumaa.Baada ya kutoa taarifa kwenye vituo
vitatu vya televisheni na Radio Iman kuwa Sheikh Ramadhan Sanze na
wenzake wataachiliwa na kuwasihi Waislam wasishiriki maandamano baada ya
sala ya Ijumaa nilimpigia simu Abdul Kambaya kuulizia kama naweza
kuzungumza na Sheikh Ramadhan Sanze. Kambaya akanieleza mambo
yamebadilikana hawajaachiwa. Niliwasiliana na RCOna nikabaini kuwa suala
hilo haliko tena chini ya uamuzi wake na litakamilishwa siku
ijayo.Usiku wa alhamisi kuamkia Ijumaa nilijaribu kuwasiliana na Rais
Kikwete kupitia wasaidizi wake ili nimfahamishe mantiki na sababu ya
hatua nilizochukua na atumie uwezo wake alionao Sheikh Ramadhan Sanze na
wenzake waachiliwe. Kwa bahati msaidizi mmoja alipata ujumbe wangu wa
simu na akanipigia simu saa 6:50 usiku na kunifahamisha atajitahidi
kuufikisha ujumbe wangu kwa Mhe. Rais ili nipate kuongea naye kuhusu
jamaa wanaoshikiliwa na polisi waachiwe ili kupunguza jazba na kuepusha
shari. Niliyezungumza naye alikuwa Dodoma na Rais alikuwa Arusha na
ratiba yake ilikuwa imebana sana na kwa hiyo hakuweza kupata fursa ya
kunipigia simu siku hiyo ya Ijumaa.Siku ya Ijumaa Abdul Kambaya
aliendelea kufuatilia kuachiwa kwa Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake
Central Police Station. Nami katika kuhangaika ili waliokamatwa
waachiliwe nilipata fursa ya kuzungumza na IGP na kumfahamisha sababu ya
juhudi nilizochukua na mategemeo yangu kuwa Sheikh Sanze na wenzake
wangeachiwa. Ninakiri kuwa katika mazungumzo ya simu, IGP Mwema alikuwa
msikivu na mkarimu sana katika kauli yake. Alinishukuru kwa kauli
niliyoitoa katika vituo vya televisheni na kuwa atafuatilia suala
nililomueleza. Hatimaye Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake waliachiwa.Naam
ini kama Sheikh Ramadhan Sanze na wenzake wangeachiwa ingesaidia sana
kupunguza jazba. Hata hivyo Waislam wengi na wananchi wengine kwa ujumla
walipokea vizuri wito wangu na hawakushiriki katika maandamano. Baadhi
wamenikosoa na kushauri kuwa ilifaa nisubiri mpaka baada ya maandamano
kufanyika na kama patatokea majeruhi na vifo ndipo nitoe tamko la
kulaani vitendo vya polisi na serikali.Katika mitandao ya kijamii
wengine wamekejeli juhudi zangu. Nilikubali kushiriki katika kipindi cha
Makutano show kinachoendeshwa na Bi. Fina ambapo hupata maswali toka
Jamii Forum. Moja ya swali lililotolewa ni “Muulize very very solid,
kuna agenda gani kati ya Cuf na uislam? mtaani leo wanasema kauli ya
Lipumba ya jana kusitisha maandamano wameitii, na ukiangalia mikutano
yake pale jangwani utafikiri kuna mawaidha ni balaghashia na baibui.”
Fina hakupata muda wa kuniuliza swali hili. Jibu lake ni la wazi. CUF
inasimamia Haki Sawa kwa Wananchi Wote. Kuna Watanzania wengi ambao ni
Waislam na wao pia wanastahiki kutendewa haki katika nchi yao. Kuhusu
balaghashia na baibui ni vyema vijana wakatazama picha za umati wa watu
uliokuwa unahutubiwa na Mwalimu Nyerere wakati wa kupigania uhuru wa
nchi hii. Picha hizo pia zinaonyesha waliokuwa wakipigania uhuru wengi
walivaa balaghashia na baibui hata Mwalimu Nyerere alipewa zawadi nyingi
za balaghashia na akaamua kuzivaa. Kushamiri kwa demokrasia ya kweli
msingi wake mkubwa ni amani na utulivu. Amani ya kweli haipatikani bila
kuwepo haki. Kesi ya Sheikh Ponda msingi wake na madai ya kiwanja. Ki
msingi kesi ya madai ya kusuluhishwa na Mahakama ya ardhi. Sheikh Ponda
ana haki ya msingi ya kupewa dhamana hata kama kauli zake haziifurahishi
serikali.Nasiki tika sana katika kipindi hiki tete,viongozi wa serikali
wameshindwa kuchukua juhudi za makusudi kuzungumza na Maimam wa
misikiti na viongozi wa asasi za Kiislam kupunguza jazba. Badala yake
wameachia kauli za vitisho vya Kamanda Kova ndiyo viwe mawasiliano kati
ya serikali na Waislam.Ni vyema serikali ikatumia busara na kuwasiliana
na Maimamu wa misikiti na viongozi wa asasi za Kiislam kuelewa hoja na
malalamiko yao.Hatimaye nimepata fursa ya kuzungumza na Mheshimiwa Rais
leo asubuhi na nikamueleza juhudi nilizozichukua kuweza kupunguza jazba
na kuwaomba Waislam wasishiriki kwenye maandamano baada ya sala ya
Ijumaa. Ni wazi hali hii ya mtafaruku ndani ya jamii inamsononesha sana
Mheshimiwa Rais na ninaamini atajitahidi kwa uwezo wake wote kutafuta
suluhisho.Katik a kutafuta suluhu ya mtafaruku huu nitaendelea na
jitihada za kutafuta fursa niweze kubadilishana mawazo na Rais Kikwete.
Nitazungumza na viongozi wa asasi za Kiislam. Nitazungumza na viongozi
wa Makanisa ya Kikristo. Madhumuni ya mazungumzo yangu nikuwafahamisha
mantiki ya juhudi nilizofanya na kushauriana misingi muhimu ya Waumini
wote kuheshimiana na kuvumiliana ili tujenge Tanzania yenye haki sawa
kwa wote.
Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti
Novemba 4 2012
KWANINI ANATUKANWA PROF LIPUMBA PEKEE? HUHU MUANDISHI NI MBUMBU AU HANA AKILI TIMAMU?, WAANDISHI WENYE UPENDELEO WA DHAHILI NDIO WALIOSABABISHA MAUAJI YA KIMBALI RWANDA NA BURUNDI. WAANDISHI TUACHE UNAFKI.