Tuesday, September 4, 2012

Kodi, Utawala bora na Maendeleo ya Taifa


Prof Ibrahim Lipumba
Mwenyekiti Wa Cuf Taifa
Katika nchi nyingi maskini, mipango na miradi ya maendeleo na usambazaji wa huduma za msingi unakwamishwa na serikali isiyokuwa na fedha za kutosha. Katika kusimamia maendeleo hakuna sera muhimu ya serikali inayozidi mfumo na viwango vya kodi. Hata hivyo kurekebisha mfumo na kuongeza viwango vya kodi kunaweza kusababisha serikali kuanguka. Matumizi ya serikali yanahitajika katika kuhakikisha kuwepo kwa amani, utulivu na usalama wa raia. Huduma za msingi za jamii kama vile elimu bora kwa watoto wote, huduma za afya za msingi kwa wananchi zinahitajika ili wananchi wafurahie maisha yao lakini vile vile wananchi wenye elimu na afya bora wanakuwa na tija kubwa katika uzalishaji wa bidhaa na huduma. Kukuza uchumi utakaowaletea neema wananchi wote kunahitaji miundombinu ya barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege, ufuaji na usambazaji wa umeme, utafiti wa kilimo na huduma za ugani. Katika maeneo mengi ya miundimbinu, sekta binafsi haiwezi kuwekeza. Serikali ina jukumu la kuendeleza miundombinu na kusambaza huduma za jamii.
Kwa muda mrefu bajeti ya Tanzania imetegemea kwa kiwango kikubwa cha asilimia 30-40 fedha kutoka kwa wahisani wa nchi za nje. Ukusanyaji wa mapato ya ndani umeongezeka. Lakini nakisi ya bajeti ya serikali pia imekuwa inaongezeka mpaka kufikia zaidi ya asilimia 11 katika miaka mitatu ya fedha 2009/10 – 2011/12. Katika miaka ya fedha 15 iliyopita mapato ya ndani hayakidhi matumizi ya kawaida. Kwa hiyo mapato ya kodi hayachangii bajeti ya maendeleo. Tanzania inahitaji iongeze ukusanyaji wa kodi ufikie asilimia 22 – 25 ya pato la taifa ukilinganisha na ukusanyaji wa mapato ya ndani ya asilimi 16 hivi sasa.
Mchakato wa ujenzi na uimarishaji wa dola unaenda sambamba na uwezo wa serikali kukusanya kodi na mapato mengine. Ulipaji na ukusanyaji wa kodi na usambazaji wa huduma za serikali unatoa fursa ya ujenzi wa uhalali wa dola katika jamii. Ikiwa ukusanyaji wa kodi ni wa kutumia mabavu na kuwanyanyasa wananchi kama ilivyokuwa katika ukusanyaji wa kodi ya kichwa wakati wa ukoloni ambayo baada ya uhuru ilibatizwa jina zuri na kuitwa kodi ya maendeleo, uhalali wa dola unaathirika na mahusiano ya dola na raia yanakuwa mabovu. Ikiwa mfumo na viwango vya kodi vinatokana na majadiliano na makubaliano kati ya serikali na wananchi, ulipaji na ukusanyaji wa kodi una fursa ya kuchangia katika ujenzi wa dola yenye uhalali mbele ya jamii. Mapinduzi ya Marekani ya mwaka 1776 yalianza kama mgomo wa kulipa kodi kwa serikali ya Mfalme wa Uingereza. Kauli mbiu ya Wamarekani ilikuwa “No taxation without representation” tafsiri yake ikiwa hakuna kulipa kodi bila kuwakilishwa.
Sera za kodi zinapaswa kutazamwa na kuchambuliwa kwa upana zaidi. Ulipaji na ukusanyaji kodi uwe nyezo ya kujenga dola yenye uhalali na inayowajibika kwa wananchi. Ili azma hii ya ujenzi wa dola yenye uhalali iweze kufikiwa ni lazima mfumo wa kodi uwe na uonekane kuwa ni wa haki na unaendeleza usawa katika jamii. Matumizi ya serikali yawe adilifu na wananchi waone wananufaika na kodi wanazolipa. Ikiwa kazi kubwa ya polisi ni kupokea rushwa na kuwabambikizia kesi wananchi, majambazi yanawapora wananchi, hakuna usalama wa raia na mali zao, mahakama zimejaa rushwa, huduma za afya mbovu, watoto hawapati elimu bora, barabara hazitengenezwi, umeme unakatika kila wakati ni vigumu kuwahamasisha wananchi kulipa kodi na kutumia mfumo wa kodi kujenga dola yenye uhalali kwa wananchi.
Watanzania wengi wanaamini kuwa mfumo wa kodi hauna haki na unawabana wananchi maskini. Theluthi moja ya mapato ya kodi inatokana na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ambayo kila mnunuzi wa bidhaa na huduma analipa kiwango sawa cha kodi bila kujali kama ana kipato kikubwa au kidogo. Makampuni makubwa na hususan makampuni ya madini yamepewa misamaha ya kodi. Wawekezaji wa nje wanasamehewa kodi lakini makampuni ya ndani yanabanwa kulipa kodi. Mawaziri, Wabunge, Maafisa waandamizi katika serikali na mashirika ya umma wanasamehewa kodi wanapoagiza magari na vifaa vingine kutoka nje.
Ili kujenga utamaduni wa kulipa kodi kwa hiari na kuongeza mapato ya serikali ni lazima kurekebisha mfumo wa kodi uwe wa haki na usawa. Wananchi washirikishwe kwa kupewa elimu ya kweli kuhusu mfumo wa kodi. Mijadala kuhusu mfumo wa kodi iwe wazi.
Kuwepo kwa utamaduni mzuri wa kulipa kodi unamfanya mwananchi aone fahari kulipa kodi kwa mujibu wa sheria zilizopo. Ulipaji kodi wa hiari unategemea sana imani ya walipa kodi kuhusu mfumo mzima wa kodi na jinsi mamalaka ya kodi inavyotekeleza wajibu wake. Ulipaji wa kodi wa hiari unakuwepo ikiwa wananchi wanahisi kuwa kama raia wana wajibu wa kulipa kodi. Kuwa na hisia kuwa kulipa kodi ni wajibu kanategemea sana wananchi kuamini kuwa serikali inatumia vizuri na kwa uadilifu fedha za kodi kwa manufaa ya umma.
Utendaji ulio wazi na wa haki wa wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato unasaidia sana katika kujenga utamaduni wa kulipa kodi kwa hiari. Ikiwa jamii inaamini kuwa rushwa imekithiri katika mamlaka ya mapato, utamaduni wa kulipa kodi kwa hiari hauwezi kujengeka. Kuongeza uwezo na nguvu za mamlaka ya mapato zinaweza kusaidia zaidi kuongeza mapato ya wakusanya kodi kuliko mapato ya serikali. Katika kuandaa na kutekeleza sera za kodi ni muhimu kuzingatia hali halisi ya uchumi na jamii ya nchi husika. Sera za kodi za nchi zilizoendelea zinasisitiza sana ufanisi katika mfumo, viwango na ukusanyaji wa kodi. Pia huzungumzia masuala ya kukwepa kulipa kodi lakini mara nyingi hawachambui matatizo ya rushwa katika ulipaji na ukusanyaji wa kodi. Tatizo la kukabiliana na rushwa linapaswa kuzingatiwa kwa makini katika kuandaa na kutekeleza sera za kodi. Mfumo wa kodi unaofaa kwa nchi nyingi zinazoendelea kama Tanzania ni ule utakaopunguza mianya ya rushwa.
Viwango vya kodi vinaweza kukwaza ilipaji wa kodi wa hiari. Mzigo wa kodi ukiwa mkubwa sana watu watakwepa kulipa kodi. Ikiwa utaratibu wa kulipa kodi ni mwepesi na hauna gharama kubwa ya muda na pesa, ulipaji wa kodi wa hiari utaongezeka. Kama kuna watu wengi na kampuni nyingi zinazokwepa kulipa kodi, zitawakatisha tamaa wale wanaolipa kodi kwa hiari. Kuwepo kwa ukwepaji kodi ambao hauadhibiwi kunaongeza ukwepaji kodi. Kama wananchi wanaamini kuwa hakuna ukwepaji wa kodi mkubwa, wengi watajitokeza kulipa kodi.
Maeneo muhimu ya kuimarisha ulipaji wa kodi wa hiari ni pamoja na sera za kodi, utawala na uendeshaji wa mamlaka ya kukusanya mapato na uadilifu katika matumizi ya fedha za umma.
Sera za kodi zinapaswa kuwa wazi, nyepesi kuzielewa na zisimamie haki na usawa. Viwango vya kodi viwe vya wastani na vichache. Changamoto kubwa inayoathiri ujenzi wa mfumo wa kodi ulio na uwazi na unaowajibika kwa jamii ni misamaha ya kodi kwa wawekezaji wa nje. Misamaha ya kodi inapunguza mapato na kuchochea rushwa na ukwepaji wa kodi. Likizo za kodi ya mapato ya wawekezaji wa nje zinatumiwa vibaya kujenga utaratibu wa kuongeza gharama za uendeshaji ili kupunguza faida na kwa hiyo kulipa kodi kidogo. Kwa mfano makampuni binafsi ya usafiri wa ndege yalikopa katika benki za hapa hapa nchini kununua ndege za abiria. Baada ya kumaliza kulipia mkopo, walihamisha usajili wa ndege hizo kwenda Cyprus haidhuru ndege zimenunuliwa hapa hapa na zipo nchini. Sasa makampuni haya yanaandaa hesabu za mapato na matumizi zinazoonyesha kuwa  wamekodisha ndege toka Cyprus na kwa hiyo wanalipa ada ya kukodisha na kupunguza faida wanayopata na kodi ya mapato wanayolipa. Vitendo kama vinaendelea kufanyika kwa sababu ya kuwepo rushwa ndani ya mamlaka zinazosimamia usafiri wa anga na ukusanyaji wa kodi.
Watanzania wengi wanaamini kuwa mfumo wa kodi hauna haki unapendelea wawekezaji wa nje. Katika mazingira haya ni vigumu kujenga utamaduni wa kulipa kodi kwa hiari. Kufuta misamaha ya kodi ni hatua muhimu katika kuhamasisha ulipaji wa kodi wa hiari na kuishirikisha wananchi katika mijadala ya kodi itakayosaidia kujenga jamii itakayokuwa na fahari katika ulipaji wa kodi.
Mamlaka ya mapato ina kazi muhimu tatu. Mosi kujenga utaratibu rahisi wa kulipa kodi. Pili, kufuatilia na kuhakikisha kuwa wahusika wote wanalipa kodi zinazowahusu na wale wanaokwepa kulipa kodi wanachukuliwa hatua za kisheria. Tatu kuboresha utaratibu wa kulipa kodi ili wananchi wengi walipe kodi kwa hiari. Mamlaka ya mapato ina wajibu wa kujenga mazingira ya kurahisha ulipaji wa kodi na iwe na ufuatiliaji makini wa kuhakikisha kodi zinalipwa na wanaokwepa wanaadhibiwa kwa mujibu wa sheria.
Ili wananchi wajue wajibu wao wa kulipa kodi, elimu ya uraia kuhusu kodi ni muhimu. Kwa wananchi wa kawaida katika sekta isiyo rasmi ni vizuri elimu kuhusu kodi iambatane na mafunzo ya ujasiriamali na uendeshaji wa shughuli za biashara. Huduma kwa walipa kodi zihakikishe kuwa utaratibu wa kulipa kodi unakuwa mwepesi. Gharama za kukwepa kodi kwa maksudi ziwe kubwa ili wananchi wawe na motisha wa kulipa kodi. Wanaolipa kodi kwa hiari wataongezeka ikiwa maafisa wa Mamalaka ya Mapato itawaheshimu na kuwatendea haki bila upendeleo kwa baadhi ya walipa kodi. Vitendo vya ufisadi vya baadhi ya maafisa wa Mamlaka ya Mapato ya kuwabana wafanyabiashara watoe rushwa ili wasiongezewe kodi vinaathiri sana ujenzi wa utamaduni wa kulipa kodi.
Ni muhimu kuwepo na uhusiano wa karibu na unaoonekana kati ya kulipa kodi na huduma za serikali. Uadilifu katika matumizi ya serikali na huduma bora zinazogharimiwa na serikali zinasaidia kuongeza motisha wa kulipa kodi. Kwa mfano serikali iwe wazi katika kuonyesha ujenzi na ukarabati wa barabara unaolipiwa na kodi ya mafuta ya petroli kwa ajili ya kujenga barabara.
Watanzania wengi hawashiriki katika kulipa kodi ya mapato. Katika nchi yenye watu milioni 44, ni wananchi laki tano tu ndiyo wenye namba za kulipia kodi. Wananchi wengi wameajiriwa au kujiajiri katika sekta ya kilimo asilia vijijini na sekta isiyo rasmi. Baadhi ya wananchi katika sekta isiyo rasmi wana vipato vikubwa vya kuweza kulipa kodi. Kuzirasimisha shughuli za sekta isiyo rasmi kuna faida kwa wajasiriamali wa sekta hiyo. Shughuli zao zinapofahamika wanaweza kupata mikopo ya kupanua biashara zao, mafunzo ya ujasiriamali, masoko na teknolojia bora ya kuendeleza shughuli zao. Mkakati wa kupanua wigo wa walipa kodi toka sekta isiyo rasmi ujikite katika mafunzo ya ujasiriamali yatakayoongeza ufanisi na faida kwa wafanya biashara wa sekta isiyo rasmi na kuwawezesha kulipa kodi bila kuathiri sana mapato yao.
Athari kwa utawala bora kwa nchi inayotegemea wigo mkubwa wa walipa kodi na uwezo wa serikali kukusanya kodi ni pamoja na kuwa na dola inayowajibika katika matumizi ya fedha za walipa kodi kuhakikisha inawaletea neema wananchi wake wote. Ili serikali ikusanye kodi za kutosha toka kwa wananchi inabidi ijenge uwezo wa kupata taarifa ya mapato na matumizi ya raia ili kuweza kukusanya kodi kwa ufanisi na uadilifu. Juhudi za kujenga uwezo wa kukusanya kodi zinaifanya serikali kwa ujumla wake kuwa na uwezo wa kiutawala.
Raia wanaotozwa kodi wanakuwa na shauku ya kujua matumizi ya kodi zao na kwa hiyo kuishinikiza serikali kuwajibika katika matumizi yake. Mchakato wa kutoza na kukusanya kodi unawafanya raia kuafiki kulipa kodi kwa hiari ikiwa wanaamini kodi zao zinatumiwa vizuri kwa manufaa ya umma. Viwango vya kodi visiwe vya juu sana vinavyoathiri vibaya maisha ya mlipa kodi. Kushiriki kwa wananchi katika mijadala ya sera za kodi na matumizi ya serikali kunasaidia kuweka viwango na mfumo wa kodi unaotabirika. Bunge linapata nguvu ya kuiwajibisha serikali.
Bila kuweka utaratibu wa mkataba wa jamii (social contract) kati ya wananchi na dola kupitia ulipaji kodi, wananchi hawawezi kuwa na motisha wa kujenga uwezo wa kuchunguza na kukagua matumizi ya serikali na kuiwajibisha. Bila wananchi kuwa ngangari wa kujua matumizi ya fedha zao za kodi, hapawezi kuwepo na ufanisi wa kutosha katika matumizi ya serikali.
Wananchi watakuwa na motisha kufuatilia ufanisi wa matumizi ya serikali ikiwa kwa kiasi kikubwa matumizi hayo yanatokana na ulipaji wa kodi wa wananchi wenyewe na siyo misaada kutoka nje. Kuendelea kutegemea misaada ya nje kunaathiri kujenga dola inayowajibika kwa wananchi. CCM imejenga dola tegemezi. Ni muhimu kwa Watanzania kujipanga na kuchagua uongozi wenye dira utakaouhakikisha kuwa misamaha holela ya kodi inaondolewa, wawekezaji wa nje wanalipa kodi, mfumo wa kodi unakuwa wa haki sawa kwa wote na utaratibu wa kulipa kodi unaasisi mkataba wa jamii wa kuiwajibisha serikali na kuhakikisha matumizi ya serikali yanaelekezwa kukidhi mahitaji ya wananchi na kuchochea maendeleo.



Saturday, August 25, 2012

MUDA WA KULITEKA JANGWA UMEWADIA.

Mh Abdul Kambaya-
Naibu Mkurugenzi wa Habari,
Mahusiano na Haki za Binadamu
wa Chama cha Wananchi (CUF)
KATIKA KUJIANDAA NA SAFARI YA KUELEKEA ARUSHA TUTALIKABILI JANGWA TAREHE 09-09-2012
CUF-Chama Cha Wananchi, kinawatangazia Mkutano Mkubwa wa Hadhara utaofanyika siku ya Jumapili kwa tarehe tajwa hapo juu.
Mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na Viongozi wote wa Kitaifa wa CUF. Mkutano utaanza saa nne asubuhi mpaka saa kumi na mbili jioni. Profesa Ibrahim Lipumba atawaoongoza Wanachama wa CUF katik

a Mkakati mdogo Ujulikanao kwa jina la MCHAKA MCHAKA MPAKA 2015 kuzunguka Mikoa sita kukutana na Watanzania ili kuweza kujadili muelekeo wa Nchi yetu na hatima ya Watanzania chini ya siasa Uchwara za Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Kila Mwanacuf unaesoma taarif a hii, tafadhali mjulishe na mwenzio. Makabwela na Walala hoi wote tafadhalini ASIBAKI MTU NYUMBANI . Mabepari wamefanya Mkutano wao na mmewashuhudia, sasa ni zamu ya MAKABWELA NA WALALA HOI kukumbuka historia ya mababu zetu ndani ya Jangwa la MAKABWELA. MCHAKA MCHAKA MPAKA 2015

Thursday, August 23, 2012

KUPANDA KWA BEI YA CHAKULA KATIKA SOKO LA DUNIA KUWE CHACHU YA KUASISI MAPINDUZI YA KILIMO TANZANIA


Prof Ibrahim Haruna Lupumba-Mwenyekiti Wa Cuf Taifa.
Mwanzono mwa mwezi wa Agosti nilienda Tabora kumtazama na kumpa pole shangazi yangu anayeumwa. Hali ya bei ya chakula hasa mahindi ilinitisha. Kwa kawaida mwezi wa Agosti ni baada ya mavuno. Bei ya mahindi huwa bado iko chini. Debe la mahindi huwa halizidi shilingi 5000/- Mwaka huu agosti mwanzoni bei ya debe la mahindi ni shilingi 10000/-. Ifikapa Disemba bei ya mahindi inaweza kuruka na kufikia shilingi 15000/- au zaidi.
Tathmini ya serikali kama ilivyoelezwa na Waziri wa Kilimo na Ushirika katika hotuba yake ya bajeti kuwa “ Matokeo ya tathmini ya awali ya hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula na utabiri wa hali ya chakula kwa mwaka 2012/2013 yanaonesha kwamba uzalishaji wa mazao ya chakula utafikia tani 13,572,804 ikilinganishwa na mahitaji ya chakula yanayokadiriwa kuwa tani 11,990,115 kwa mwaka 2012/2013. Taifa linatarajia kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 113 na hivyo kuwa na ziada ya tani 1,582,690. Tathmini hiyo ilibaini kuwepo na ziada ya chakula katika mikoa nane (8) ya Iringa, Rukwa, Mbeya, Kagera, Mtwara, Kigoma, Ruvuma na Morogoro; utoshelevu katika mikoa saba (7) ya Pwani, Mara, Tanga, Lindi, Mwanza, Singida na Dodoma; na uhaba katika mikoa sita (6) ya Shinyanga, Tabora, Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Dar es Salaam”
 Hali ya bei ya vyakula katika maeneo mengi ya nchi haionyeshi kuwepo kwa ziada kubwa. Vile vile hali ya biashara ya mazao ya vyakula ndani ya mipaka ya Tanzania ina vikwazo. Maeneo yenye ziada hayauzi chakula cha kutosha kwenye maeneo yenye upungufu. Bei ya mahindi  Tabora ingekuwa ya chini kama wafanyabiashara wangenunua mahindi toka Mpanda mkoa wa Rukwa na kuyauza Tabora.
Hata katika miaka ambayo chakula kilichozalishwa nchini kinaonekana kukidhi mahitaji ya taifa, ukosefu wa lishe bora ni tatizo la muda mrefu. Miaka 50 baada ya uhuru, theluthi moja  ya Watanzania ikimaanisha Mtanzania mmoja katika kila Watanzania watatu hawana lishe bora. Asilimia 44 ya watoto wote wenye umri wa chini ya miaka 5 wana utapiamlo, ni wafupi kuliko wanavyostaili kuwa kwa sababu ya kukosa chakula cha kutosha na lishe bora. Watoto wasiokuwa na lishe bora wanashindwa kujenga kinga ya mwili, maungo yao siyo imara na hawajengi ubongo wao vizuri na kwa hiyo wanakuwa wagumu  kujifunza na kufundishwa. Kuhakikisha kuwa kina mama wajawazito na watoto wote wanapata lishe bora ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele na familia, jamii na serikali kwa ujumla.
Hali ya bei ya mazao ya nafaka  hasa mahindi katika soko la dunia  inatisha. Tathmini ya Waziri wa Kilimo katika hotuba yake ya bajeti imepitwa na wakati kwani alieleza kuwa  taarifa ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (Food and Agriculture Organisation - FAO) iliyotolewa mwezi Juni 2012, inaonesha kuwa katika mwaka 2011/2012, uzalishaji wa nafaka duniani unatazamiwa kuongezeka kwa asilimia 3.2. Jumla ya tani  bilioni 2.42 za nafaka zitazalishwa ikilinganishwa na matumizi ya nafaka ya tani bilioni 2.38 kwa mwaka 2012/2013, matumizi ya nafaka kwa ajili ya chakula cha mifugo yataongezeka kwa asilimia 3.8 wakati matumizi ya chakula yanatazamiwa kuongezeka kwa asilimia moja (1). Akiba ya nafaka duniani inatazamiwa kuongezeka kwa tani milioni 36 na kufikia tani milioni 548 sawa na ongezeko la asilimia saba (7) kutoka kiwango cha mwaka jana.”
Marekani ya Magharibi ya Kati ndiyo eneo linalozalisha mahindi kwa wingi. Mwezi wa julai mwaka huu ulikuwa na joto kali katika eneo hili kuliko miaka yote 117 iliyopita tangu kumbukumbu za hali ya joto kuanza kutunzwa. Marekani kwa ujumla imekumbwa na ukame mbaya kupita yote kwa muda wa miaka 50. Marekani ndiyo inayoongoza katika kuzalisha na kuuza nafaka katika soko la dunia. Kwa sababu ya ukame uzalishaji wa mahindi na maharage ya soya utapungua sana mwaka huu na tayari bei za mahindi na soya zimevunja rekodi ya bei ya mwaka 2008.
Nchini Marekani na Ulaya mahindi yanatumika sana kama chakula cha mifugo. Mexico, nchi za Marekani ya kati na Afrika, mahindi ni chakula muhimu cha binadamu. Nchini Marekani ng’ombe analishwa kilo 30 za mahindi ili kupata kilo moja ya nyama.
Wamarekani pia wanatumia mahindi kutengeneza ethanol inayotumiwa kama petroli mbadala. Katika kila majunia 100 ya mahindi yanayozalishwa Marekani, 40 yanatumiwa kutengeneza ethanol. Mahindi yanayotumiwa kutengeneza ethanol kujaza tenki la gari ya familia ya Marekani yanatosha ugali wa mwaka mzima wa mkulima wa Tabora. Utumiaji wa mahindi kutengeneza ethanol kunaongeza bei ya mahindi katika soko la dunia.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa – FAO, Jose Graziano da Silva ameiomba Marekani kusitisha mara moja utumiaji wa mahindi kutengeneza ethanol ili kupunguza mfumko wa bei ya mahindi katika soko la dunia. Katika mwaka wa uchaguzi mkuu, Serikali ya Marekani haielekei kukubali wito wa Jumiya ya Kimataifa ya kusitisha matumizi ya mahindi kutengeneza ethanol kwa sababu wakulima wa mahindi wa Marekani ya magharibi ya kati wanaipenda sera ya kutumia mahindi kutengeneza ethanol kwa kuwa inaongeza bei ya mahindi. Majimbo yenye wakulima wa mahindi kama vile Iowa ni muhimu katika mkakati wa Rais Obama na chama cha Democrats kushinda uchaguzi Novemba 2012.
Kupanda kwa bei ya chakula duniani ni changamoto na fursa. Bei  ya chakula katika soko la dunia itaendelea kuwa juu kwa muda mrefu kwa sababu ya mahitaji ya nafaka kulisha mifugo na matumizi ya mazao kutengeneza petroli mbadala.
Kilimo chetu kimeendelea kuwa duni kwa sababu zisizokuwa na msingi. Tuna ardhi ya kutosha, mito na maziwa makubwa. Jiografia ya Tanzania inafanya nchi yetu iwe na majimbo yenye hali ya hewa tofauti. Mazao mbali mbali ya chakula na biashara yanastawi katika ardhi ya Tanzania, nchi yetu ina uwezo mkubwa wa kuzalisha mazao ya chakula na biashara kukidhi mahitaji ya ndani na kuuza nchi za nje. Lakini miaka 50 baada ya Uhuru, Tanzania haijitoshelezi kwa chakula kwa sababu ya sera na uongozi usiokuwa na dira sahihi ya maendeleo.
 Nchi yetu ina ardhi kubwa inayokubali aina mbambali ya mazao. Tunatumiai robo tu ya ardhi yote inayofaa kwa kilimo. Ardhi inayolimwa haipandwi mbegu bora. Kati ya wakulima 100 wa Tanzania, 90 wanatumia mbegu za kienyeji zisizokuwa na uwezo wa uzalishaji mkubwa. Wakulima wengi hawatumii mbolea. Mfumo wa usambazaji wa mbegu bora, mbolea na pembejeo nyingine ni hafifu sana. Utaratibu wa mikopo kwa wakulima wakununulia zana na pembejeo haupo. Chini ya asilimia 1 ya ardhi inayofaa kilimo cha umwagiliaji imeendelezwa na kutumiwa. Maeneo yenye mfumo wa umwagiliaji  hayatunzwi na kukarabatiwa na kwa hiyo hayazalishi kwa uwezo wake. Matumizi ya matrekta katika kilimo bado ni madogo sana. Kwa mfano mkoa wa Kigoma wenye ardhi kubwa, mabonde yenye rutuba mito na vijito vingi ina matrekta makubwa 25 na matrekta ya mkono 176 tu.
Tanzania imekosa sera sahihi ya kukuza kilimo na kuinua hali za maisha ya wakulima. Zana za kilimo na pembejeo haziwafikii wakulima na hata zinapowafikia huwa zimechelewa na kufika nje ya wakati. Pamoja na serikali kudai kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wetu, kilimo hakipewi kipaumbele. Tangu tupate uhuru wa taifa letu matumizi halisi ya sekta ya kilimo ya kila mwaka hayajawahi kuzidi asilimia tano ya bajeti yote ya Serikali. Nchi yetu haina huduma bora kwa ajili ya kukuza kilimo cha kisasa na kwa ujumla kumekuwa na udhaifu mkubwa hasa katika maeneo ya uwekezaji kwenye tafiti, motisha kwa wakulima ili wajaribu mambo mapya, ushauri na utaalamu kwa wakulima, mikopo ya zana za kilimo na pembejeo, barabara na mawasiliano vijijini.
Hatua za muda mfupi za kukabiliana na ongezeko kubwa la bei katika baadhi ya wilaya za Tanzania ni kuruhusu na kurahisisha biashara ya ndani ya mazao ya chakula. Serikali irahisishe mfumo wa kodi na ushuru wa mazao ya kilimo; ikiwa ni pamoja na kufuta ushuru na ada zote za mazao katika ngazi ya mkulima ili kuongeza motisha kwa wananchi kuwekeza juhudi zaidi katika uzalishaji wa mazao ya kilimo. Vizuizi vyote visivyo na msingi katika biashara ya mazao yote ndani ya nchi viondolewe.
Wafanyabiashara wa ndani wapewe motisha wa kuwekeza katika ununuzi wa nafaka toka maeneo yenye ziada na kuuza kwenye maeneo yenye upungufu. Sera za serikali katika mazao ya chakula hazitabiriki. Wakuu wa Wilaya wanaweza kuzuia uuzaji wa nafaka nje ya wilaya zao. Matokeo yake hakuna wafanyabiashara wa nafaka inayozalishwa nchini wenye mtazamo wa muda mrefu badala yake kuna walanguzi wenye mtazamo wa muda mfupi.
Hivi sasa serikali ianze uhamasishaji wa uzalishaji wa mazao yanayokomaa kwa muda mfupi katika maeneo yanayopata mvua za vuli. Utaratibu mzuri wa usambazaji wa mbegu bora, mbolea na pembejeo unahitajika. Usambazaji wa vocha za mbolea umejaa ufisadi. Mbolea inachakachuliwa na haikidhi viwango na kuwapa hasara wakulima.
Wakuu wengi wa wilaya wameteuliwa kwa upendeleo wa kisiasa na hisia binafsi na hawana uwezo wa kusimamia maendeleo ya kilimo. Badala yake Wakuu wa wilaya ni vikwazo vya maendeleo ya kilimo. Wanatoa maagizo na amri zinazowakwaza wakulima. Uteuzi wa Wakuu wa wilaya na wa mikoa uzingatie uwezo wa kuongoza na kusimamia maendeleo ya kilimo.
 Sera ya Kilimo Kwanza imejikita katika kuwatumia wakulima wakubwa kuwaendeleza wakulima wadogo wadogo. Hii ni ndoto ya Alnacha. Wakulima wakubwa wanahitaji ardhi na vibarua. Maslahi ya wakulima wakubwa yanakinzana na maslahi ya wakulima wadogo wadogo. Kwa kuwa tuna ardhi ya kutosha wakulima wakubwa wenye mitaji wana nafasi katika kukuza kilimo cha Tanzania lakini wasitegemewe kuwa ndiyo chachu ya kuwaendeleza wakulima wadogo wadogo. Sera muafaka kwa Tanzania ni kuhakikisha kuwa wakulima wadogo wadogo wanashiriki katika kilimo cha biashara cha kuzalisha mazao ya ziada na kuyauza kwenye soko. Mafunzo kwa wakulima na huduma za ugani kuhusu kilimo cha kisasa ni muhimu sana. Taaluma ya ubwana na ubibi shamba irejeshewe hadhi yake na wataalam wa kilimo wapewe motisha ya kufanya kazi yao. Wakulima wapate pembejeo ikiwa ni pamoja na mbegu bora na mbolea, na zana za kilimo.
Ile ahadi ya serikali za nchi za nchi za SADC ya kutumia alau asilimia 10 ya bajeti ya serikali katika sekta ya kilimo itekelezwe. Maeneo muhimu ya kuwekeza ni pamoja na utafiti wa kilimo, barabara za vijijini na mawasiliano, mfumo wa kilimo cha umwagiliaji maji, usambazaji wa pembejeo, huduma za fedha za kuweka akiba na kukopa kununulia pembejeo.
Tanzania ina fursa ya kukuza sekta ya kilimo kwa wastani wa asilimia 8 kwa mwaka kwa muda ya miaka 10 ijayo ukilinganisha na ukuaji wa wastani wa asilimia 4 katika miaka 10 iliyopita . Tuna ardhi ya kutosha kukidhi mahitaji yetu ya chakula na kuuza nchi za nje. Sekta ya kilimo inapokua kwa kasi inachochea ukuaji wa sekta nyingine. Upatikanaji wa chakula kwa bei nafuu unapunguza gharama za maisha na gharama za kuajiri wafanyakazi wenye afya njema. Kilimo cha kisasa kinahitaji mbolea, mbegu bora na utaalamu. Gesi iliyonguduliwa inaweza kutumiwa kutengeneza mbolea. Kilimo kinahitaji huduma za usafiri – kusafirisha pembejeo na mazao ambao unaongeza ajira. Mazao ya kilimo ni malighafi katika viwanda vya kusindika nafaka, matunda, maziwa na nyama. Viwanda vya nguo na bidhaa za ngozi vinatumia malighafi inayozalishwa na kilimo. Kipato cha wakulima kinapoongezeka wananunua bidhaa za viwandani kama vile nguo, vyombo vya nyumbani, samani, mabati, saruji na vifaa vinginevyo. Mapinduzi ya kilimo yatachochea ukuaji wa sekta ya viwanda na kuongeza ajira katika sekta rasmi.
Ili kuasisi mapinduzi endelevu ya kilimo yatakayomsaidia mkulima wa kawaida Tanzania inahitaji uongozi wenye dira. Serikali ya CCM imewasaliti wakulima wa Tanzania na kuwaongezea umaskini. Jukumu muhimu la wanaharakati wa dira ya mabadiliko ni kuwaelimisha na kuwahamasisha wakulima washiriki kikamilifu katika mabadiliko ya kisiasa yatakayoasisi mapinduzi ya kilimo yatakayowanufaisha Watanzania wote.







Friday, August 17, 2012

TANZANIA INAHITAJI UONGOZI WENYE DIRA NA SERIKALI MADHUBUTI ILI KUJINASUA TOKA DIMBWI LA UMASKINI

Mwenyekiti Wa Cuf Taifa-Prof Ibrahim Lipumba

Nchi ambazo zimefanikiwa kukuza uchumi kwa kasi ya juu na kuwa na maendeleo kwa muda mrefu zimefanya hivyo kwa kuwa na uongozi adilifu, wenye dira na ulio imara katika uamuzi, utekelezaji na kujifunza toka kwenye makosa waliofanya na kujirekebisha.Kuzungumzia uongozi na uadilifu katika siasa si jambo jepesi. Hisia na mitazamo ya watu wa kawaida kuhusiana na ‘siasa’ imekuwa ya kuihusisha fani hiyo na tamaa, ubinafsi, uroho, unafiki, ulaghai, upotovu, uovu, fitina, hiyana, na hata hujuma. Tena si watu wa kawaida tu bali hata baadhi ya wasomi wetu wanaonekana kuiona hivyo. Kwa wananchi wetu wa kawaida mtu akisifiwa kuwa huyo kwa siasa humuwezi, maana yake ni gwiji wa uongo na laghai. Hali hiyo kwa kiasi kikubwa imesababishwa na ubabaishaji wa uongozi wa kisiasa tuliokuwa nao na tunaoendelea kuwa nao.Katika nchi masikini kama Tanzania, uongozi wa kisiasa ni muhimu katika kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa, kukuza na kupanua demokrasia na kuhakikisha kuwa nchi inaendeshwa kwa misingi ya utawala wa sheria, ambapo haki inatendeka na inaonekana inatendeka. Utawala wa sheria na haki sawa kwa wananchi wote ndio msingi imara wa amani na utulivu. Changamoto kubwa ya nchi yetu ni kujenga uchumi unaokua kwa kasi, kuongeza ajira na kuneemesha wananchi wote.


Tanzania inakabiliwa na changamoto mbili kubwa kujenga uchumi wenye manufaa kwa wananchi wote na kujenga demokrasia ya kweli itakayohakikisha nchi inaendeshwa kwa kufuata sheria zinazotoa haki sawa kwa wananchi wote. Nchi yetu inahitaji uongozi ambao unaona siasa ni utumishi wa dhati na uliotukuka kwa umma uliozindukana na siyo nyenzo ya kukimbilia na kupigania vyeo, fursa na nguvu ya ushawishi kwa malengo ya kujilimbikizia uwezo wa maamuzi na wa utajiri binafsi usiohojiwa.

Uongozi wa nchi unawajibika kubuni sera kwa kuzingatia uhalisia na hali ya uchumi wa nchi, fursa zilizopo na vikwazo vinavyoikabili nchi katika kukuza uchumi wake.  Baada ya kubuni sera uongozi unawajibika kuzieleza sera hizo kwa wananchi na kuwahamasisha waziunge mkono na waelewe kuwa ili kujinasua toka dimbwi la umaskini wanawajibika kuchapa kazi kwa bidii, kuweka akiba, kuwa wajasiriamali wabunifu na kukubali kasi ya mabadiliko inayoendana na ukuaji wa uchumi.  Uongozi utafanikiwa ikiwa sera zake zinaaminika na zinatekelezeka, na matunda ya sera hizo yanaleta neema kwa wananchi wote.

Uongozi makini utakaoweza kuchochea maendeleo ya muda mrefu unapaswa kuwa na subira, uwe na dira na mipango ya muda mrefu na ujikite katika lengo la kukuza uchumi utakaoongeza ajira na kuleta neema kwa wananchi wote. 

Katika zama za demokrasia ya vyama vingi ni muhimu kwa wadau vikiwemo Vyama Vya Siasa kukubaliana alau kwa ujumla dira ya maendeleo ya nchi na kila chama kitakachoingia madarakani kitekeleze sera zitakazokuza uchumi unaoleta tija na neema kwa wananchi wote.  Watendaji wazuri wa serikali walio waadilifu na uwezo mzuri wanasaidia sana katika kushauri wanasiasa walioko madarakani sera zinazotekelezeka na zenye manufaa kwa wananchi.

Baada ya muda mrefu bila ya kuwa na maendeleo ya kutosha, urekebishaji wa sera ni jambo muhimu.  Hata hivyo kurekebisha siyo lengo la mwisho.  Lengo ni matunda yanayotokana na kurekebisha sera hizo.  Nchi zilizofanikiwa kupata maendeleo ya muda mrefu, zimetegemea na kuutumia mfumo wa uchumi wa soko. Kuutegemea na kuutumia Uchumi wa soko hakumaanishi kuwa soko huria pekee ndiyo chanzo cha kukua uchumi.  Serikali madhubuti zilijenga mazingira ya kuwezesha sekta binafsi kutumia uchumi wa soko kuongeza kasi ya kukua kwa uchumi.

Uchumi wa soko ulioendelea unajikita katika historia na asasi muhimu katika jamii husika.  Asasi hizo ni pamoja na kuwepo haki na uhuru wa kumiliki mali, mikataba, hususan katika shughuli za biashara na uchumi huheshimiwa na inapovunjwa kuna mamlaka zinazosuluhisha na kuhakikisha kuwa mikataba inasuluhishwa kwa gharama za wastani wa wale wenye haki wanapata fidia na hawadhulumiwi.  Taarifa kuhusu masoko zinawafikia wadau wote.

Katika hatua za awali za kutafuta na kuleta maendeleo, serikali makini zinafanya majaribio ya sera zake katika maeneo machache kabla ya utekelezaji katika nchi nzima.  Moja ya mapungufu makubwa katika kubuni na kutekeleza sera katika Tanzania ni ukosefu wa kufanya majaribio na kupima mafanikio yake kabla ya kutekeleza nchi nzima.  Matatizo haya yalikuwa makubwa wakati wa sera za ujamaa.  Kwa mfano sera za kuhamia vijiji vya kudumu kuwa ni amri mwaka 1974, Sera ya elimu kwa msingi kwa wote katika mwaka mmoja, sera ya kufunga maduka binafsi na kadhalika zilitekelezwa kabla ya kufanyiwa majaribio.  Hivi karibuni sera ya kuanzisha shule za sekondari za kata haikufanyiwa majaribio kabla ya kuitekeleza nchi nzima.  Ni muhimu katika utekelezaji wa sera, serikali ikafanya majaribio (pilot projects) na kujifunza katika majaribio hayo kabla ya kuitekeleza sera katika eneo kubwa.

Kubuni sera nzuri ni mwanzo tu.  Sera zinazopaswa kuwekwa katika mipango ya utekelezaji na kutekelezwa kwa umakini wa hali ya juu.  Utekelezaji na matokeo yake yafanyiwe tathmini ya mara kwa mara ili makosa yangunduliwe na kurekebishwa.  Kujenga utumishi bora, wenye ujuzi, usiyoyumbishwa na rushwa ndani ya serikali ni changamoto muhimu.  Utumishi mzuri ulio imara haujengwi siku moja.  Viongozi wa kisiasa ni wepesi kuhujumu kuwepo kwa utendaji mzuri serikalini ikiwa watawatumia watendaji wa serikali kufanikisha malengo ya kisiasa ya kubaki madarakani kwa kuiba kura wakati wa uchaguzi au utekelezaji wa miradi ya muda mfupi kwa malengo ya kuvutia wapiga kura.  Serikali inawajibika kuvutia watumishi wenye uwezo na ari ya kufanya kazi.  Ni muhimu mishahara ya wafanyakazi serikalini iwe inavutia lakini utunishi serikalini uzingatie uwezo na siyo mtoto wa nani au unamjua nani!

Serikali yenyewe siyo inayoleta ukuaji wa uchumi.  Kazi hiyo kwa sehemu kubwa ni ya sekta binafsi yenye wajasiriamali wazuri wanaowekeza na kutumia teknolojia bora na kuzitumia fursa zilizopo katika uchumi wa soko.  Hata hivyo serikali adilifu, yenye sera nzuri zinazojulikana na kutekelezwa kwa makini, isiyoyumba ni muhimu sana kwa maendeleo ya muda mrefu.  Kazi muhimu ya serikali ni pamoja na kuhakikisha kuna utulivu katika uchumi mpana kwa maana ya kutokuwepo mfumko wa bei kuwepo kwa akiba ya kutosha na fedha za kigeni kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nchi za nje, matumizi ya serikali na sekta ya umma yalingane na mapato ya serikali, na serikali iwekeze katika miundo mbinu muhimu.

Nchi zilizofanikiwa kukuza uchumi kwa muda mrefu zinafanya hivyo kwa kuwa na sera zinazoenda na mabadiliko ya uchumi ndani na nje ya nchi.  Mikakati ya kukuza uchumi ibadilike kufuatana na mabadiliko ya mfumo wa uchumi.  Siasa za ndani ya nchi pia zinastahiki kubadilika na kwenda na wakati.  Kukua kwa uchumi kutaongeza idadi ya watu wenye kipato cha kati na watu wenye elimu ambao watadai kushiriki katika maamuzi ya sera zinazowagusa na kuwa na sauti nchi yao.

Sera za kurekebisha uchumi ili kuchochea ukuaji wake na maeneo ya kuwekeza katika miundo mbinu ni mengi na yanazidi uwezo wa mapato ya serikali. Mkakati wa kukuza uchumi lazima uweke vipaumbele vya maeneo ambayo serikali itayashughulikia mwanzo.

Sera za kukuza uchumi endelevu zinajenga, mazingira mazuri ya uwekezaji mkubwa wa vitega uchumi, ongezeko la ajira, ushindani wa kibiashara, wepesi wa raslimali kutumiwa kwa shughuli mbadala (mobility of resources) hifadhi ya jamii na wananchi wote kufaidi matunda ya kukua kwa uchumi.

Hakuna nchi iliyofanikiwa kukuza uchumi kwa kasi ya juu kwa muda mrefu bila serikali kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika miundo mbinu – barabara, nishati, reli, bandari na mawasiliano, elimu na afya.  Uwekezaji wa serikali  katika sekta ya miundo mbinu, elimu na afya unajenga msingi imara unaovutia sekta binafsi kuwekeza katika shughuli za uzalishaji na biashara.  Uwekezaji wa sekta ya umma katika maeneo hayo unatengeneza njia yakuwezesha viwanda na makampuni mapya kuanzishwa na kuongeza faida ya shughuli zote za kibiashara zinazofaidika kwa kuwepo wafanyakazi wenye afya njema na walioelimika, kuwepo kwa barabara nzuri zinazopitika wakati wote, na kuwepo kwa umeme wa uhakika.

Nchini Tanzania, uwekezaji katika miundombinu umekuwa mdogo na hutegemea fedha za misaada toka nje.  Ukarabati wa miundo mbinu haufanyiki ipasavyo.  Barabara inajengwa inatumiwa mpaka inaharibika kabisa.  Ili ikarabatiwe tunaomba msaada kwa wafadhili waijenge upya.  Mifano ni Mingi.  Barabara ya Mandera, Barabara ya Dar es Salaam - Morogoro, Barabara ya Chalinze – Segera – Tanga, n.k

Ukuaji wa uchumi unaambatana na mabadiliko ya mfumo wa uchumi kutoka kutegemea sana kilimo na kuelekea kwenye ongezeko la ajira viwandani, kutoka nguvu kazi inayoishi vijijini kuelekea nguvu kazi inayoishi mijini.  Mabadiliko ya mfumo wa uchumi husababishwa na ushindani wa soko.  Serikali zenye malengo ya kukuza uchumi endelevu zinawajibika kujenga ushindani katika masoko yote kuruhusu makampuni mapya yenye tija kuanza na makampuni yanayopata hasara kufilisika.  Soko la ajira liwe jepesi kuruhusu makampuni mapya kuajiri wafanya kazi na makampuni yanayopata hasara kupunguza wafanyakazi.  Sheria za kazi zijikite katika kurahisisha uanzishwaji wa ajira. Ni muhimu sana kuwa na utaratibu wa hifadhi za jamii kwa wafanya kazi wanaopoteza ajira ili kupunguza makali na kuwepo kwa soko la ajira linalonyumbulika.  Wanaopoteza ajira wapate kipato cha kuwawezesha kuishi wakati wakitafuta ajira mpya.

Elimu bora inayowapa wafanyakazi uwezo wa kujifunza na kupata ujuzi mpya ni kinga muhimu ya kutopoteza ajira kwa muda mrefu.  Vile vile zinaongeza kasi ya ajira mpya kuanzishwa kwa wingi na kwa hiyo kuhakikisha nguvu kazi inaajiriwa. 

Mkakati wa kukuza uchumi lazima uzingatie kuwa toafuati kubwa za vipato vya wananchi kati ya maskini na matajiri havisaidii ukuaji wa uchumi na vinaongeza upinzani dhidi ya sera za kurekebisha uchumi.  Ni wazi uchumi unapoanza kukua tofauti za vipato zinaongezeka.  Sera zijikite katika kutoa fursa ya kupata ajira kwa wananchi wengi iwezekanavyo  na misaada maalum itolewe kwa watu maskini waweze kujinasua toka dimbwi la umaskini.  Vurugu za kisasa kupinga wachache kuwa matajiri wakati wengi ni maskini zitaathiri mikakati ya kukuza uchumi.

Kigezo muhimu cha kupima kama sera zinatoa fursa sawa kwa wote ni fursa za wasichana kupata elimu iliyo bora.  Wanawake walipata elimu, wanakuwa na watoto wachache wenye afya bora ambao wanawazaa wakati maungo yao yamekua.  Kina mama wenye elimu wanasisitiza na kuhakikisha kuwa watoto wao nao wanapata elimu.  Kuwaelimisha wasichana na kuwapa fursa ya kupata ajira ni nyenzo madhubuti ya kuutokomeza umaskini.

Nchi zilizofanikiwa kukuza uchumi kwa kasi zilitumia vizuri fursa zilizopo katika soko la dunia na kuongeza uuzaji wa bidhaa zao za viwandani katika soko hilo.  Sera za kuongeza uzalishaji wa bidhaa za viwanda hazikutegemea utaratibu wa soko huria tu.  Serikali zilijaribu sera mbali mbali za kutoa motisha wa kuongeza uzalishaji viwandani na kuuza bidhaa za viwandani nchi za nje.  Sera za kukuza sekta ya viwandani ni pamoja na ruzuku katika uzalishaji wa bidhaa mpya, uwekezaji wa miundo mbinu mizuri katika maeneo maalum ya kuanzisha viwanda vipya, misamaha ya kodi.  Ni muhimu motisha maalum kwenye viwanda vitakavyouza bidhaa nchi za nje zisiwe za kudumu.  Ikiwa sera hazikufanikiwa kuongeza kasi ya kukua kwa sekta ya viwanda na uuzaji wa bidhaa nchi za nje, sera hizo zibadilishwe.

Utandawazi umefanya uchumi wa dunia hivi sasa kuwa wazi zaidi na kuingiliana sana katika biashara, uwekezaji, huduma za fedha na teknolojia.  Nchi zilizokua kwa kasi ya juu zimefanya hivyo kwa kuingiza maarifa, teknolojia na ujuzi kutoka nchi za nje.  Njia moja ya kupata maarifa na teknolojia kutoka nje ni kupitia uwekezaji unaofanywa na makampuni ya nje.  Njia nyingine ni kupata elimu, maarifa na teknolojia iliyopo katika nchi zilizoendelea na kuitumia kwa kuzingatia uhalisi na mazingira ya nchi yako.

Uchumi wa dunia unatoa fursa ya soko kubwa kwa nchi zinazoendelea. Kinadharia, Tanzania inaweza  kuuza bidhaa zote za viwandani inazozalisha kwa bei ya soko la dunia. Suala la msingi ni je kuuza nchi za nje ndiyo njia pekee ya kukuza uchumi au tunaweza kukuza uchumi kwa kutegemea soko la ndani ya nchi?

Mikakati ya kuendeleza uchumi kwa kutumia soko la ndani inaweza kufanikiwa kwa muda mfupi hasa kwa nchi kubwa zenye watu wengi.  Zaidi ya hapo matatizo ya kutetereka uchumi yanaweza kutokea ikiwa nchi itafungua mipaka yake ghafla kwa bidhaa kutoka nje.  Hata hivyo mikakati ya uchumi inayotegemea soko la ndani tu hufikia ukomo wake mapema. Soko la ndani ni dogo mno kuendeleza ukuaji wa uchumi kwa muda mrefu na hautoi fursa ya kujikita na kubobea katika eneo la uzalishaji ambalo nchi ina ushindani au inaweza kujijengea ushindani mkubwa.

Ukuaji wa haraka wa uchumi katika nchi maskini hutegemea upatikanaji wa ajira kwa nguvu kazi ya ziada iliyomo nchini. Kwa kadri uchumi unavyokua ndivyo unavyoajiri nguvukazi ya ziada iliyomo nchini hasa vijijini katika sekta ya kilimo na iliyoko mijini katika sekta isiyo rasmi yenye tija ndogo.  Raslimali za nchi hasa nguvu kazi ni lazima ziwe tayari kuhama toka eneo au sekta yenye tija ndogo kwenda kwenye eneo na sekta zenye tija kubwa ambazo kwa kawaida huanzishwa mijini ambako ni rahisi kupata watu wengi wenye ujuzi na huduma muhimu kwa viwanda kama vile umeme na maji.  Ukuaji wa uchumi huambatana na ukuaji wa miji na nguvu kazi kuhamia mijini. Hata hivyo ili miji iwe vitovu vya ukuaji endelevu ya uchumi inahitaji miundombinu mizuri.

Sera za kukuza uchumi ni lazima zizingatie kuweko na utulivu katika uchumi mpana kama vile kuepukana na mfumko wa bei, ukosefu wa fedha za kigeni, ulimbikizaji mkubwa wa madeni ya sekta ya umma unaotokana na nakisi katika bajeti ya serikali na hasara za mashirika ya umma.  Vile vile mkakati wa uchumi unapaswa kutoa motisha kwa wajasiliamali, wadogo, wa kati na wakubwa kuwekeza katika sekta mbali mbali kwa kuwahakikishia kuwa wakifanya shughuli zao kwa ufanisi na kufanikiwa kupata faida, faida yao hiyo haitaporwa na vyombo vya dola au majambazi.  Vile vile ni muhimu kuwa na mikakati ya hifadhi ya jamii ya kupunguza makali ya maisha kwa watu watakao athirika na mabadiliko ya uchumi.

Kwa nchi zenye ziada ya nguvu kazi ukomo wa kasi ya kukua kwa uchumi unategemea kasi ya uwekezeshaji wa vitega uchumi.  Uwekezaji wa vitega uchumi hutegemea ukubwa wa akiba.  Ili uchumi ukue kwa kasi nchi inapaswa iweke akiba alau asilimia 25 – 30 ya pato la Taifa na kulimbikiza vizuri katika vitega uchumi vyenye tija kubwa.  Misaada kutoka nje haiwezi kuwa mbadala wa juhudi za kuweka akiba za ndani ya nchi za kila kaya, sekta binafsi na sekta ya umma ili akiba ilimbikizwe katika vitega uchumi muhimu.

Hivi sasa nchi yetu inakabiliwa na ombwe la uongozi na tumeshindwa kutumia raslimaliwatu na maliasili yetu kujenga uchumi unaoongeza ajira na kutokomeza umaskini. Nchi inahitaji uongozi utakaowaunganisha Watanzania kukabiliana na changamoto nilizozianisha katika mada hii. Watanzania tunapaswa kujiuliza bila kujali, itikadi, udini, ukabila na umajimbo nani katika viongozi wetu wa kisiasa wana dira na uwezo wa kuwaunganisha Watanzania kutekeleza dira ya mabadiliko itakayojenga uchumi imara, unaongeza ajira na kutokomeza umaskini? Tukiipoteza fursa ya kulijibu swali hili kwa vitendo mwaka 2015, tunaweza kujikuta tunapoteza miaka mingine 50 ya uhuru wetu bila kujiletea maendeleo na wananchi wengi kiendelea kubakia maskini wa kutupwa.

KAULI YA NAPE DHIDI YA CHADEMA NI KAMA MTU ANAEOGOPA KIVULI CHAKE

Mh Abdul Kambaya-
Naibu Mkurugenzi wa Habari,
Mahusiano na Haki za Binadamu
wa Chama cha Wananchi (CUF)
CUF –Chama cha Wananchi kimeshangazwa na Kauli ya Katibu Muenezi wa CCM, alietoa kwa Vyombo vya Habari na kukituhumu chama cha CHADEMA , kwamba kimeingia mikataba ya kufisadi na Wafadhili walionje ya Nchi kwa lengo la kutaka kuja kupora Mali ya Asili inayoendelea kugunduliwa hapa Nchini kwetu Tanzania. Katika maelezo yake Katibu huyo iliita kile kilichofanywa na CHADEMA katika HARAMBEE ya kutafuta Fedha ni USANII, na kwamba CHADEMA wanataka kuhalalisha mabilioni waliopata toka kwa Wafadhili wao, na kwamba CCM inaushahidi na inawafahamu Wafadhili hao.
CUF –Chama cha Wananchi kinashangazwa na kauli hii ya kisanii iliotolewa na CCM kupitia Katibu wake Muenezi, CCM ni Chama kinachoongoza Nchi, jambo ambalo walipaswa kusema sio kuishitaki CHADEMA kwa Wananchi bali ni kuzuia hayo babilioni na kuwataja hao wafadhili ambao wameingia Mikataba na CHDEMA kwa lengo la kuja kupora utajiri mkubwa unaoendelea kugunduliwa katika masiku ya hivi karibuni. CUF- Chama cha Wananchi kinaamini kwamba CCM na CHADEMA ni watoto wa familia moja , na Wanafadhili wanao wafadhili ni wa aina moja wa ndani na nje ya Nchi. Iwapo Chadema wameingia mikataba ya kupewa mabilioni ili baadae wataposhika Madaraka waweze kulipa mabilioni hayo kwa kutukmia Mali ya asili tulionayo, basi watakuwa wanaendeleza utaratibu ule ule wa CCM wa kuiuza Nchi kwa bei poa ili mradi wao wawepo madarakani kama ambavyo CCM inafanya hivi sasa kuingia Mikatba mibovu isiokuwa na Manufa na Wananchi ili mradi wao wawafurahishe Wafadhili wao.
CUF- Chama cha Wananchi kinaamini kwamba Mti wa Matatizo ya Nchi yetu, ni Mufumo mbovu unaoendesha Serikali yetu na Nchi kwa ujumla wake. Kuwa na Vyama vyenye tamaa ya Madaraka, kama CCM na Chadema, ni matokeo ya awali ya Mfumo mbovu wa Nchi yetu, na kukithiri kwa wizi na matumizi mabaya ya Fedha za Umma na ukiukwaji wa Haki za binaadamu ni matokeo ya kati ya Mfumo mbovu. Watanzania waliowengi kuwa masikini wa kutupwa, ukosefu wa huduma bora kwa jamii,kudumaa kwa maendeleo ya Nchi na ukosefu wa ajira ni Matokeo ya muda mrefu yanayosababishwa na Mfumo mbovu wa Nchi yetu. Kwa maana hiyo basi, CUF –Chama cha Wananchi kinaamini kwamba , njia sahihi ya kulinda Rasilimali zilizopo na zinazoendelea kugunduliwa ndani ya Nchi yetu, ni kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitafa, Serikali ambayo itashirikisha Vyama vyote venye wabunge, na kwa utaratibu huo, kutakuwa hakuna Chama kitakachokuwa na maauzi ya pekee katika matumizi ya Rasilimali na Mali ya asili ya Nchi yetu. Jambo hili limekuwa linahubiriwa sana na CUF , lakini pia limekuwa linapingwa sana na CCM na Chadema na kwa mantiki hiyo,
CUF – Chama cha Wananchi hakioni tafauti ya CCM na Chadema kisera na kimtazamo. CUF kinawataka Watanzania waelewe kwamba, kinachonekana hapa ni kwamba ,Chadema inaonyesha imewazidi kete CCM huko kwa Wafadhili wa nje kama ilivyowazidi kete kwa ufadhili wa Sabodo ndio maana unaona CCM inapiga kelele.
CUF – Chama cha Wananchi kina wataka CCM waache kuogopa kivuli chao na badala yake washughulike na kubadili Mufumo unaoendesha Nchi yetu iwapo kweli wanataka mabadiliko ya Kiuchumi na Kijamii .