Friday, August 17, 2012

KAULI YA NAPE DHIDI YA CHADEMA NI KAMA MTU ANAEOGOPA KIVULI CHAKE

Mh Abdul Kambaya-
Naibu Mkurugenzi wa Habari,
Mahusiano na Haki za Binadamu
wa Chama cha Wananchi (CUF)
CUF –Chama cha Wananchi kimeshangazwa na Kauli ya Katibu Muenezi wa CCM, alietoa kwa Vyombo vya Habari na kukituhumu chama cha CHADEMA , kwamba kimeingia mikataba ya kufisadi na Wafadhili walionje ya Nchi kwa lengo la kutaka kuja kupora Mali ya Asili inayoendelea kugunduliwa hapa Nchini kwetu Tanzania. Katika maelezo yake Katibu huyo iliita kile kilichofanywa na CHADEMA katika HARAMBEE ya kutafuta Fedha ni USANII, na kwamba CHADEMA wanataka kuhalalisha mabilioni waliopata toka kwa Wafadhili wao, na kwamba CCM inaushahidi na inawafahamu Wafadhili hao.
CUF –Chama cha Wananchi kinashangazwa na kauli hii ya kisanii iliotolewa na CCM kupitia Katibu wake Muenezi, CCM ni Chama kinachoongoza Nchi, jambo ambalo walipaswa kusema sio kuishitaki CHADEMA kwa Wananchi bali ni kuzuia hayo babilioni na kuwataja hao wafadhili ambao wameingia Mikataba na CHDEMA kwa lengo la kuja kupora utajiri mkubwa unaoendelea kugunduliwa katika masiku ya hivi karibuni. CUF- Chama cha Wananchi kinaamini kwamba CCM na CHADEMA ni watoto wa familia moja , na Wanafadhili wanao wafadhili ni wa aina moja wa ndani na nje ya Nchi. Iwapo Chadema wameingia mikataba ya kupewa mabilioni ili baadae wataposhika Madaraka waweze kulipa mabilioni hayo kwa kutukmia Mali ya asili tulionayo, basi watakuwa wanaendeleza utaratibu ule ule wa CCM wa kuiuza Nchi kwa bei poa ili mradi wao wawepo madarakani kama ambavyo CCM inafanya hivi sasa kuingia Mikatba mibovu isiokuwa na Manufa na Wananchi ili mradi wao wawafurahishe Wafadhili wao.
CUF- Chama cha Wananchi kinaamini kwamba Mti wa Matatizo ya Nchi yetu, ni Mufumo mbovu unaoendesha Serikali yetu na Nchi kwa ujumla wake. Kuwa na Vyama vyenye tamaa ya Madaraka, kama CCM na Chadema, ni matokeo ya awali ya Mfumo mbovu wa Nchi yetu, na kukithiri kwa wizi na matumizi mabaya ya Fedha za Umma na ukiukwaji wa Haki za binaadamu ni matokeo ya kati ya Mfumo mbovu. Watanzania waliowengi kuwa masikini wa kutupwa, ukosefu wa huduma bora kwa jamii,kudumaa kwa maendeleo ya Nchi na ukosefu wa ajira ni Matokeo ya muda mrefu yanayosababishwa na Mfumo mbovu wa Nchi yetu. Kwa maana hiyo basi, CUF –Chama cha Wananchi kinaamini kwamba , njia sahihi ya kulinda Rasilimali zilizopo na zinazoendelea kugunduliwa ndani ya Nchi yetu, ni kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitafa, Serikali ambayo itashirikisha Vyama vyote venye wabunge, na kwa utaratibu huo, kutakuwa hakuna Chama kitakachokuwa na maauzi ya pekee katika matumizi ya Rasilimali na Mali ya asili ya Nchi yetu. Jambo hili limekuwa linahubiriwa sana na CUF , lakini pia limekuwa linapingwa sana na CCM na Chadema na kwa mantiki hiyo,
CUF – Chama cha Wananchi hakioni tafauti ya CCM na Chadema kisera na kimtazamo. CUF kinawataka Watanzania waelewe kwamba, kinachonekana hapa ni kwamba ,Chadema inaonyesha imewazidi kete CCM huko kwa Wafadhili wa nje kama ilivyowazidi kete kwa ufadhili wa Sabodo ndio maana unaona CCM inapiga kelele.
CUF – Chama cha Wananchi kina wataka CCM waache kuogopa kivuli chao na badala yake washughulike na kubadili Mufumo unaoendesha Nchi yetu iwapo kweli wanataka mabadiliko ya Kiuchumi na Kijamii .

Thursday, August 16, 2012

Kuporomoka kwa uchumi wa dunia na mikakati ya Tanzania kujikwamua kiuchumi


Mwenyekiti Wa Cuf Taifa-Prof Ibrahim Haruna Lipumba

Uchumi wa nchi muhimu zilizoendelea ikiwemo Marekani, Jumuia ya Ulaya na Japan bado unayumba miaka minne baada ya mtikisiko mkubwa wa uchumi mwaka 2008. Mtikisiko huo ulisababishwa na sera mbovu ya usimamizi wa sekta ya fedha ilioruhusu mfumko wa bei za nyumba na uwekezaji mkubwa katika sekta hiyo. Tufe la mfumko wa bei za nyumba lilipopasuka na bei hizo kuporomoka, mabenki mengi yalikabiliwa na tatizo la kufilisika kwa sababu mikopo yao katika sekta ya nyumba haikuweza kulipika na amana zilizohusiana na sekta ya nyumba ziliporomoka. Familia nyingi zilikopa kwa kutumia thamani ya nyumba zao kama dhamana. Kuporomoka kwa bei za nyumba ziliondoa uwezo wa kukopa na kuwalazimisha walipe madeni yao na kwa hiyo kupunguza matumizi ya kununua bidhaa na huduma. Familia zinapopunguza matumizi ya kawaida makampuni yanayotengeneza bidhaa na kutoa huduma yanakosa soko na kulazimika kupunguza uzalishaji wa bidhaa na huduma na kupunguza wafanyakazi. Watu wa kikosa ajira wanapunguza matumizi na hivyo kuathiri uzalishaji wa bidhaa na huduma na kuchochea uachishwaji wa kazi wa watu wengi zaidi. Makampuni yanayoshindwa kuuza bidhaa zao yanapunguza wafanyakazi na yanaacha kuwekeza vitega uchumi kupanua shughuli zao kwa ukosefu wa soko la bidhaa na huduma zao. Kupunguza uwekezaji kunaongeza ukosefu wa ajira.
Mahitaji ya soko la bidhaa na huduma yanapopungua, Benki Kuu inaweza kusaidia kuongeza mahitaji hayo kwa kupunguza riba. Riba inapopungua gharama za mikopo inakuwa rahisi na kwa hiyo familia na wawekezaji wanaweza kukopa. Katika mtikisiko wa uchumi ulioanza mwaka 2008, riba za Benki Kuu zimepunguzwa mpaka kufikia karibu ya sufuri na kwa hiyo haziwezi kupunguzwa zaidi ya hapo. Uwezo wa sera za riba kusaidia kuongeza matumizi ya sekta binafsi na kaya umetoweka kwa sababu riba za Benki Kuu haziwezi kwenda chini ya sufuri. Zaidi ya hapo ikiwa makampuni hayana imani kuwa kutakuwa na ongezeko la mahitaji ya bidhaa zao, hawewezi kuongeza uwekezaji hata kama riba ni za chini.
Benki Kuu inaweza kuongeza matumizi ya kaya na sekta binafsi ikiwa itaonyesha kuwa sera zake zitaongeza mfumko wa bei. Ikiwa mfumko wa bei ni wa juu, akiba ya fedha taslimu inapungua thamani yake. Watu watabaini kuwa vyema kununua bidhaa za kudumu kuliko kuweka akiba ya pesa taslimu. Wachumi wengi wamependekeza sera hii ya kuongeza mfumko wa bei kutoka asilimia 2 na kufikia asilimia 4. Hata hivyo Benki Kuu nyingi za nchi zilizoendelea zinaongozwa na mahifidhina wanaoamini kuwa jukumu lao kubwa ni kuhakikisha mfumko wa bei hauzidi asilimia 2. Hawaikubali kabisa sera itakayoongeza mfumko wa bei kwa muda ili kuhamasisha sekta binafsi inunue bidhaa na huduma badala ya kuweka akiba.
Katika hali ya ukosefu wa soko la kuuza bidhaa na huduma kila kampuni inafanya uamuzi wa busara wa kupunguza matumizi na uwekezaji. Familia zinazokabiliwa na kupungua kwa utajiri walionao na kuongezeka kwa madeni wanaamua kupunguza matumizi na kuongeza akiba. Uamuzi wa familia moja moja na kampuni moja moja una mantiki lakini kwa pamoja kila familia na kampuni zikipunguza matumizi pato lao la pamoja linapungua kwani matumizi yako ndiyo mapato ya mwingine. Ili kukabiliana na tatizo hili serikali ya nchi zilizoendelea zinawajibu wa kuongeza matumizi kuziba pengo lililoachwa na sekta binafsi. Serikali inaweza kuongeza matumizi kwa kuongeza nakisi ya bajeti. Sekta binafsi inapokuwa na kipato kidogo, mapato ya serikali ambayo yanatokana na kodi yanapungua. Kuongeza matumizi wakati mapato yanapungua maana yake ni kuongeza nakisi ya bajeti na kwa hiyo kuongeza deni la serikali. Sera ya kuongeza matumizi ya serikali na nakisi ya bajeti ni ya muda mfupi.Uchumi ukiimarika serikali itakusanya kodi nyingi na pia ina fursa ya kupunguza matumizi na kwa hiyo kuwa na ziada katika bajeti yake na kupunguza deni lake.
Sera za kuongeza matumizi ya serikali na hivyo kuwa na nakisi ya bajeti kubwa na kuongeza deni la serikali imepingwa na wahafidhina. Nchini Marekani Chama cha Republican ambacho kina Wawakilishi wengi katika Baraza la Wawakilishi kinapinga kuongeza matumizi ya serikali kwa madai kuwa itaongeza nakisi na kuongeza deni la taifa. Sera za nchi za Jumuiya za Ulaya, kanda ya euro zinaongozwa na fikra za Serikali ya Ujerumani ambayo inapinga serikali kuwa na nakisi kubwa ya bajeti. Nchi wanachama wa kanda ya euro hawana Benki Kuu zao zilizo huru na hawana sarafu zao wenyewe. Hawana uwezo wa kuongeza nakisi ya bajeti zao bila kuongeza riba. Serikali za nchi za Ulaya Kusini – Hispania, Italia, Ureno na Ireland wanalipa riba kubwa sana wanapokopa katika masoko ya fedha. Uingereza ambayo nakisi yake ya bajeti ni kubwa zaidi ya Hispania inatozwa riba ndogo kwa sababu ina Benki Kuu na  sarafu yake yenyewe na kwa hiyo ina uwezo wa kulipa madeni yake kwa kuchapisha fedha zake kwa wingi.
Hatua za mwanzo za kukabiliana na mtikisiko wa uchumi mwaka 2008 ulikuwa sahihi. Nchi nyingi ziliongeza matumizi ya serikali. Kwa sababu ya itikadi za kihafidhina, kuongezeka kwa nakisi ya bajeti na kukua kwa deni la taifa likaleta mabadiliko ya sera serikali zikaanza kubana matumizi kabla ya uchumi kutengamaa na sekta binafsi kuimarika. Sera sahihi ni kuendelea kuongeza matumizi ya serikali katika kipindi cha muda mfupi na kuweka mpango wa kukabiliana na nakisi ya bajeti na deni la serikali kwa muda wa kati baada ya sekta binafsi kuimarika na hivyo kuongeza ajira na kodi za serikali. Misamaha ya kodi kwa matajiri iondolewe wakati wananchi wenye kipato cha chini na cha kati waendelee kunufaika na misamaha ya kodi katika kipindi cha muda mfupi mpaka uchumi utakapoimarika.
Baada ya mgogoro wa fedha duniani wa mwaka 2008, jumla la pato la dunia lilianguka kwa asilimia 0.6 mwaka 2009. Uchumi wa nchi zilizoendelea ndiyo ulioanguka zaidi. Pato la taifa la Ujerumani lilianguka kwa asilimia 5.1, Japan na Italia kwa asilimia 5.5, Uingereza asilimia 4.4 na Marekani kwa asilimia 3.5. China haikuathirika sana na mtikisiko wa uchumi wa dunia kwa sababu ya hatua zilizochukuliwa na serikali ya China za kuongeza matumizi kukabiliana na kupungua kwa mahitaji katika soko la bidhaa. Kasi ya kukua kwa pato la taifa la China ulipungua kutoka asilimia 14.2 mwaka 2007 na kufikia asilimia 9.2. Juhudi za pamoja za  kufufua uchumi za Marekani, nchi za Jumuiya ya Ulaya na nchi zinazoendelea hasa Uchina, India na Brazil zilisaidia kuongeza ukuaji wa uchumi wa dunia na kufikia asilimia 5.3 mwaka 2010. Lakini kupunguza kwa matumizi ya serikali na mgogoro wa Euro umepunguza ukuaji wa uchumi na kufikia asilimia 3.9 mwaka 2011 na makadirio ya 3.5 mwaka 2012.
Nchi za Jumuiya ya Ulaya zinakabiliwa na mdororo mwingine wa uchumi kwa sababu ya matatizo ya Euro. Pato la kanda ya Euro linakadiriwa kupungua kwa asilimia 0.3 mwaka 2012. Nchi za Ulaya ya Kusini – Ugiriki, Hispania, Italia na Ureno ndizo zimeathirika zaidi kwa kuporomoka kwa uchumi na kuongezeka kwa ukosefu wa ajira. Pato la taifa la Marekani litakua kidogo tu kwa asilimia 2.1. Ukosefu wa ajira unabakia juu sana zaidi ya asilimia 8.0.
Inasikitisha kuwa nchi zilizoendelea zimekumbwa na itikadi ya kihafidhina na wameshindwa kufuata ushauri wa wachumi wa kimataifa wa kuongeza matumizi ya serikali katika kipindi cha muda mfupi na kushughulikia nakisi ya bajeti na ukuaji wa deni la taifa katika kipindi cha muda wa kati. Kususua kwa uchumi wa nchi zilizoendelea kunaongeza matatizo kwa nchi maskini katika mikakati yao ya kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuutokomeza umaskini. Nchi maskini kama Tanzania inategemea soko la nchi zilizoendelea kuuza bidhaa zake, wengi wa watalii wanaokuja Tanzania wanatoka nchi za Ulaya, Wawekezaji wa vitega uchumi wanatoka nchi zilizoendelea na serikali inategemea misaada na mikopo toka nchi hizo.
Kati karne ya 21 nguvu za uchumi za mataifa umeanza kubadilika. Uwezo wa kiuchumi wa nchi za magharibi unapungua ukilinganisha na nchi za Asia. Nchi nyingi zinazoendelea na hasa China zimeendelea kukuza uchumi wao pamoja na kuathiriwa na mtikisiko wa uchumi wa nchi zilizoendelea. Nchi yetu inabidi iweke mkakati wa kushirikiana na nchi zinazoibuka na kuwa na nguvu za kiuchumi kwa manufaa ya nchi yetu lakini tusigezwe kuwa soko la bidhaa duni toka nchi hizo.
Kwa kuwa nchi yetu iko nyuma katika maendeleo ya uchumi, tuna fursa nyingi za kutumia elimu, utaalamu na teknolojia ambayo imeishagunduliwa ili tukuze pato letu la taifa, tuongeza ajira yenye kipato kizuri, na hatua kwa hatua tuotokomeza umaskini. Ni muhimu kwa Watanzania tujihamasishe na tuwe na motisha wa kujifunza na kutumia teknolojia iliyopo tukizingatia mazingira tuliyonayo. Kuna fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji na tija kwa kutumia teknolojia bora katika sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu, madini, nishati, viwanda, usafiri na mawasiliano, na huduma za jamii.
Kuwepo kwa fursa za kukuza uchumi katika sekta mbalimbali hakuna maana kuwa fursa hizo zinaweza kutumiwa kirahisi. Kuwa na uchumi wa soko na utengamano wa uchumi mpana (macroeconomic stability), fedha za kigeni kupatikana kwa bei ya soko na kuondoa vikwazo vya biashara ya nje hakutoshi kuiwezesha nchi kukua kwa asilimia 8-10 kwa muda wa miaka 20-30 na kuubadilisha mfumo wa uchumi wake kutoka kutegemea kilimo na sekta isiyo rasmi na kuongeza ajira katika sekta ya viwanda na huduma za kisasa.  Kukua kwa uchumi kwa kasi hiyo kunahitajika ili kuhakikisha tunautokomeza umaskini.
Tunahitaji sera za maksudi za kuasisi maendeleo makubwa ya viwanda kwa kuanzia na viwanda vinavyotumia malighafi inayozalishwa nchini. Kuanzisha na kuendeleza viwanda hakutafanikiwa kwa kuachia mfumo wa soko peke yake uamue maeneo ya uwekezaji. Juhudi maalum ya serikali na nidhamu ya hali ya juu ya utekelezaji inahitajika. Serikali inapaswa kutambua vikwazo vinavyokwamisha maendeleo ya viwanda na kuviondoa. Miundombinu ya usafiri na umeme ni muhimu kwa maendeleo ya kasi ya viwanda na uchumi kwa ujumla. Pamoja na kuelewa kuwepo kwa tatizo hili kwa muda mrefu, inasikitisha kuwa serikali imeshindwa kabisa kutekekeleza mipango yakutatua matatizo ya miundombinu. Serikali imeshindwa kuweka vipaumbele na kutekeleza miradi michache ikakamilika kabla ya kuanza miradi mingine.
Serikali imekuwa na mipango mingi isiyo tekelezwa au kutekelezeka. Kuna Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 ambayo inalenga kuwa Tanzania iwe ni nchi yenye kiwango cha kati cha mapato (middle income country) na hali bora ya maisha kwa wananchi. Mpango Maalum wa Kuharakisha Maendeleo ya Tanzania (Tanzania Mini Tiger Plan 2020) ambao haijulikani umeishia wapi.  Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania – MKUKUTA I na MKUKUTA II na Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano 2010-15. MKUKUTA I na MKUKUTA II hazikufanyiwa makadirio ya gharama za utekelezaji wake. Gharama za mpango wa miaka mitano ni kubwa mno na serikali haina fedha ya kuugharamia.
Pamoja na matatizo ya uchumi wa dunia, Tanzania inaweza ikatumia fursa ya kuwa nyuma na kutumia teknolojia iliyopo kukuza uchumi wake. Watanzania tunahitaji tutafakari hali halisi tuliyonayo na tubuni sera na mikakati ya pamoja inayotekelezeka ili tujikwamue toka dimbwi la umaskini. Misingi muhimu ya sera na mikakati hiyo iwe kuitumia vizuri mali ya asili ya Tanzania kwa manufaa ya wananchi wote huku tukilinda mazingira yetu. Kuwekeza kwenye afya ya watoto wa Tanzania toka wakiwa katika mimba za mama zao kwa kuhakikisha kina mama wajawazito na watoto wachanga wanapata lishe bora. Kuwekeza katika elimu ya watoto wa Tanzania toka shule za chekechea na kuendelea. Kuweka msisitizo maalum katika elimu ya hesabu, sayansi na teknolojia. Kuwekeza katika kilimo hasa cha chakula kama vile mahindi, mpunga, maharage, jamii ya kunde na mbegu za mafuta kukidhi mahitaji ya ndani na kuuza masoko ya nje hasa nchi za jirani. Kuwekeza katika miundombinu ya barabara, umeme, maji na mawasiliano. Kuweka mkakati madhubuti wa kuanzisha na kuendeleza viwanda vinavyotumia malighafi ya ndani na kuajiri watu wengi kama vile viwanda vya nguo na mavazi, viatu na bidhaa za ngozi, vifaa vya matumizi ya nyumbani na vifaa vya umeme na elektroniki.
Kubuni na kutekeleza mikakati hii Tanzania inahitaji uongozi wenye dira utakaowaunganisha na kuwahamasisha Watanzania tujielimishe na tutumie raslimali na mali ya asili ya nchi yetu kuwaletea neema wananchi wote.

Wednesday, August 8, 2012

JUMUIYA YA VIJANA YA CUF YALAANI MAUAJI YA WANASIASA VIJANA KUKITHIRI NCHINI:

Naibu Katibu JUVICUF
Jumuiya ya Vijana ya CUF inasikitishwa na kusononeshwa na vitendo vya mauaji ya wanasiasa vijana inayoendelea hapa nchini Tanzania. Hii ni kutokana na mauaji ya kila mara ya vijana hasa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambayo yanaonekana kama mauaji ya kulipizana kisasi. Huu si ustaarabu wa kidemokrsia bali ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Ni hivi karibuni watanzania walishuhudia mauaji ya kikatiri ya kiongozi wa vijana wa CHADEMA kule Arusha mara baada ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki. Lakini pia tumeshitushwa na mauaji mengine ya kijana kiongozi wa CCM jimboni Iramba Magharibi juzi baada ya mkutano wa hadhara wa CHADEMA.
Mauaji ya namna hii huleta hofu kwa vijana kushiriki siasa za moja kwa moja kwa kuogopa kuuawa. Iwapo mauaji haya ya vijana wanasiasa hayatapatiwa ufumbuzi kuna hatari ya vijana wenye uwezo kuikimbia siasa na hatimaye Taifa likakosa viongozi bora wa sasa na baadaye.
Jumuiya ya Vijana ya CUF inaamini kuwa bila kuwa na utamaduni wa kuvumiliana  japokuwa tunatofautiana kimtazamo, itkikadi, dini na kabila zetu , kamwe hatutaifikia demokrasia ya kweli. Uvumilivu ni msingi mkuu wa Demokrasia ha hivyo ni wajibu wetu vijana kuacha kutumikia hisia na mihemko ya miili yetu na vyama vyetu na kuutanguliza Utanzania wetu na udugu wetu mbele.
Jumuiya ya Vijana ya CUF inawaomba vijana wa CCM na CHADEMA kuwa makini wakati tukiwa katika mchakato huu wa kuitafuta Demokrasia ya kweli inayojali misingi ya Haki za binadamu, utawala bora na ushindani wa hoja bila kuchukiana na kujenga uadui baina yetu kwani sote tuna nia ya kuijenga Tanzania yenye neema ambayo rasilimali zake zitawafaidisha watanzania wote.
Jumuiya ya Vijana ya CUF imesikitishwa sana na mauaji hayo ya vijana yanayofanywa na vijana wenyewe kwa wenyewe. Hii ni ishara kuwa Vijana wa CCM na CHADEMA hawajaiva kisiasa kwani wanashindwa kutofautisha Upinzani na Uadui. Na kutokana na mauaji haya ni wajibu wa watanzania kutambua kuwa CCM na CHADEMA hawana dira na sera za kuwafikisha watanzania kwenye neema bali wana nia ya kuwamaliza kwa kuwaua kikatiri.
Jumuiya ya Vijana ya CUF inawaomba watanzania wawe macho na mienendo ya vijana wa CHADEMA na CCM maana mauaji wanayoendelea kulipizana hayatakwisha leo wala kesho. Kwa hiyo wanapaswa kukigeukia chama chao kipenzi cha Wananchi –CUF ambacho ni chama cha makabwela na  wanyonge wa Tanzania.
Imetolewa na:
Thomas D.C Malima
Naibu Katibu Mkuu
 Sekretarieti ya Vijana-Taifa
CUF-Chama Cha Wananchi.

JUVICUF YATOA POLE KWA WANAFUNZI NA WAZAZI WA SHULE YA SEKONDARI YA MOROGORO

Naibu Katibu Wa JUVICUF
JUMUIYA ya Vijana  wa Chama Cha Wananchi-CUF (JUVICUF) inapenda kutoa pole kwa wanafunzi , wazazi na walimu wa Shule ya Sekondari ya Morogoro (Wasichana) kutokana na ajali ya moto iliyowakumba kwa baadhi ya majengo yake yakiwemo mabweni ya wanafunzi kuungua na kuteketetea kwa moto uliotokana na hitilafu ya umeme na kusabaisha zaidi ya wanafuzi 600 kuathirika kwa namna moja au nyingine.
JUVICUF inatambua kuwa japokuwa hakuna aliyepoteza maisha lakini wanafunzi wamepoteza masomo, mali, na wamekubwa na athari za kisaikolojia wakati wote wa ajali na baada ya ajali. Tunatambua nafasi yenu kama vijana wa Tanzania katika ujenzi wa Taifa lenu na mmepata ajali hii mkiitafuta elimu ili muijenge nchi yenu vizuri. Ni kutokana na umuhimu huo, ndio maana JUVICUF inaungana nanyi katika kipindi hiki cha matatizo.

JUVICUF inakubaliana na taarifa za awali za Jeshi la Polisi, wanafunzi na walimu wa shule hiyo kuwa  ajali hiyo ilitokana na miundombinu mibovu ya umeme shuleni hapo. Na kwa kuwa tatizo hili haliko katika shule ya Sekondari ya Morogoro(wasichana) pekee bali ni kwa zaidi ya shule 50 kongwe hapa nchini. Hii ni kwa sababu ya serikali kushindwa kuzipangia bajeti ya kutosha ya ukarabati kila mwaka. Shule hizi zilijengwa kabla na mara tu baada ya uhuru lakini hazifanyiwi ukarabati kabisa.

JUVICUF inaitaka serikali ifanye utafiti wa kina kwa shule zote za zamani kutokana na uchakavu mkubwa  wa miundombinu ya umeme na maji katika mazingira yake. Shule nyingi ziko taabani kwani majengo yake yamezeeka, miundombinu ya maji safi na majitaka pamoja na miundombinu ya umeme vimezeeka na kuharibika kabisa kiasi cha kuhatarisha afya na uhai wa wanafunzi na walimu wao.

Pia JUVICUF inaitaka serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais (Maafa) iangalie namna ya kuwawezesha wanafunzi hao waliopoteza nguo na vifaa vyao vya kusomea wapate nguo na vifaa vya kusomea ili waendelee kusoma bila matatizo wakati huu wa matatizo bila kuathiri ratiba za masomo yao ya kila siku.

Na ni wajibu wa serikali kuwahudumia  kimatibabu wanafunzi wote waliopatwa na majeraha pamoja mshituko wakati wa ajali hiyo ya moto shuleni hapo bila kuhitaji malipo kutoka kwa wazi/walezi wa wanafunzi hao. Hili ni jukumu la serikali siyo hisani kwao. Kwa hiyo tunaitaka serikali igharimie matibabu yao.

Leo tukio hili limetokea Morogoro Sekondari (Wasichana), kesho tukio kama hili linaweza likatokea shule nyingine na kuleta maafa makubwa. Kwa hiyo lazima serikali iwe makini kuzuia majanga kabla ya

kusubiri kuokoa pindi majanga yanapotokea. Lazima tuwe makini kulinda maisha ya vijana wetu hata kwa gharama kubwa maana ndio tegemeo letu kwa maendeleo ya Taifa letu. Ni heri kulinda maisha na ustawi wa watu wako kwa gharama kubwa kuliko kusubiri kuwaokoa kwa gharama kubwa.

JUVICUF inatambua athari kubwa zinazoweza kujitokeza endapo serikali haitakuwa makini na uboreshaji wa miundombinu ya shule zakekwani zinawakutanisha wanafunzi wengi katika mazingira mabovu yanayoweza kusababisha magonjwa ya milipuko, hitilafu za umeme au janga la aina yoyote ile.

JUVICUF inawapa pole na kuungana na wanafunzi hao pamoja na wazazi wao kwa kuwaomba wawe wavumilivu katika kipindi hiki cha matatizo.
Imetolewa na:
Thomas D.C Malima
Naibu Katibu –TAIFA
JUMUIYA YA VIJANA YA CUF (JUVICUF)






Tuesday, August 7, 2012

DIRA YA MABADILIKO – VISION FOR CHANGE: MANIFESTO YA CUF YA 2010


A Vision for Change
“Watanzania wameweka matumaini yao kwa Chama cha CUF na misingi yake ya sera ya kuleta “Haki sawa kwa wananchi wote” na “Kujenga uchumi imara unaoongeza ajira na utakaoleta neema na tija kwa wote.” Chama chetu kimekuwa ni Chama kikuu cha upinzani nchini kwa muda mrefu sasa na wananchi wanaendelea kuteseka kwa kuona matatizo yao yakizidi kuongezeka bila kuchukuliwa kwa hatua za msingi kushughulikia matatizo yao. Hali hii inawafanya wananchi wengi hasa vijana na wanawake kuwa katika shauku kubwa ya kuona utawala wa nchi yetu unabadilishwa kwa amani kupitia karatasi za kura. CUF kwa kutambua nafasi yake katika kuyaongoza Mabadiliko yanayohitajika, kikiwa siyo tu chama kikuu cha upinzani hapa nchini bali pia kutokana na mjengeko wake wa kuwa kweli ni chama cha kitaifa chenye kukubalika na chenye mtandao mpana katika pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano, imezindua DIRA YA MABADILIKO – VISION FOR CHANGE. Dira ya Mabadiliko ndiyo msingi wa ILANI yetu ya uchaguzi. Vision for Change chini ya Serikali ya CUF itatujengea Tanzania Mpya inayojali haki sawa kwa wananchi wote na itakayojenga uchumi imara unaoongeza ajira na utakaoleta neema na tija kwa wote.” Kwa kuisoma Manifesto yetu ya Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa mwaka 2010, unaweza kupakuwa kwenye kiungo hapo chini.
 CUF Manifesto 2010

Monday, August 6, 2012

JUVICUF waionya JUVICCM na BAVICHA kutotumikia matakwa ya Mafisadi wa vyama vyao.

Naibu katibu Wa Jumuiya Ya Vijana
CUF(JUVICUF)Bwana.Thomas Malima
Jumuiya ya Vijana ya CUF-Chama Cha Wananchi (JUVICUF) inapenda kutoa mwito kwa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kufanya uchaguzi utakaozingatia matakwa ya vijana siyo ya watu Fulani. JUVICUF inatambua kuwa uchaguzi wa vijana ni changamoto katika taasisi za kisiasa kwani wanasiasa wakubwa hutambua kuwa Vijana ndio nguvukazi kubwa na wapiga kura wakubwa katika nchi yetu. Na ni vijana pia ndio wana matatizo makubwa hasa la ajira. Kwa hiyo hulazimika kuwapanga vijana katika mabaraza yao ili waingiapo madarakani waweze kuwatumia watakavyo.
Hali hii husababisha Viongozi wengi wa Mabaraza ya Vijana ya vyama vya siasa hasa UVCCM na BAVICHA kuwa watumishi wa Viongozi wa vyama vyao badala ya kuwatumikia vijana walioko katika vyama vyao. Kwa sasa viongozi wa Jumuiya za vijana wamekuwa kama vipaza sauti vya Wazee badala ya kuwa vipaza sauti vya vijana. Na hii inaanza tangu wakati wa uchaguzi wa Jumuiya za vijana za vyama vya siasa ambapo wakubwa huwa wanatumia mbinu chafu za kuvuruga chaguzi na maamuzi ya vijana wakati na baada ya chaguzi za Jumuiya za vijana nchini.
JUVICUF inaamini kuwa jukumu lake kubwa ni kuwaunganisha vijana nchini kutambua umuhimu wao, jinsi wanavyoonewa, wanavyonyanyaswa, wanavyokandamizwa na wanavyonyonywa na viongozi dhalimu watokanao na kizazi kilichopitwa na wakati lakini kinangangania kukaa madarakani kwa nguvu.
JUVICUF inatambua kuwa ukombozi wa Vijana kifikra ndio msingi wa ukombozi wa wao kiuchumi , kisiasa na kijamii. Hivyo basi, ni jukumu letu kuwashauri Vijana wenzetu nchini kujitambua na kuungana nasi kutetea maslahi ya vijana nchini bila kutumikia wakubwa. Na kimsingi hatuwezi kuufikia ukombozi wa kweli wa vijana kama bado tunaendelea kutumika kwa manufaa ya wakubwa wetu.
JUVICUF inatambua kuwa RUSHWA ni adui wa haki ya kijana. Tunatambua kuwa endapo UVCCM watairuhusu rushwa kutembea wakati huu wa uchaguzi wao hakika watawapata viongozi wabovu wasiokidhi matakwa ya vijana.
Vile vile JUVICUF inaamini kuwa kampeni chafu za kupakana matope, ni ishara ya uchanga wa Demokrasia. Tunaitambua UVCCM kama jumuiya ya vijana ya siku nyingi lakini tuasikitika kwa wagombea na wapambe wao kuanza kufanya siasa chafu za kupakana matope. JUVICUF inaamini kuwa vijana wa sasa wanapingana kwa hoja sio kwa kuchafuana. Hizi siasa za kuchafuana ni siasa za kizamani zilizotumika enzi za ukoloni na ni za wazee. Ukimuona kijana wa leo anafanya siasa za namna hiyo ujue ana walakini au anatumiwa na wazee wa zamani waliozizoea na wanataka kuzirithisha kwa vijana.
Mwisho, JUVICUF inawatakia Vijana wa CCM uchaguzi mwema wenye utulivu, amani, upendo na heshima baina ya wagombea na wanachama kwa ujumla. Kiongozi bora atapimwa kwa busara, uwezo na matendo yake kwa jamii ya wanaomchagua. Hakika Chama imara kinategemea Vijana imara.
Thomas D.C Malima
Naibu Katibu -Jumuiya ya Vijana ya CUF-Taifa (JUVICUF)

Lipumba:Madai ya Walimu yanalipika

Mwenyekiti wa CUF Taifa,Prof.Ibrahim Lipumba
CUF – Chama cha Wananchi kimekuwa kikifuatilia kwa ukaribu matatizo mbalimbali yanayowakumba wafanyakazi na watumishi wa serikali wakiwemo madaktari, walimu na wafanyakazi wa kada zingine
Hivi karibuni Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kilitangaza mgomo ambao umefanyika kwa siku 3 kabla ya mahakama kuu kitengo cha kazi kuamua shauri la walimu na serikali na kusisitiza kuwa mgomo huo ni batili. CWT ilitumia kifungu cha 80-(1) (d) cha Sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004 kuanza mgomo huo na walimu wanachama wa CWT walianza zoezi la kupiga kura tarehe 25 Julai 2012.
Kwa mujibu wa taarifa baada ya kura zote kupigwa , asilimia 95.7 ya wanachama (walimu) waliunga mkono mgomo, ambao ni walimu wanao fundisha katika shule za awali, msingi, sekondari, maafisa walioko kwenye ukaguzi wa shule za awali, msingi, sekondari, maafisa walioko kwenye ukaguzi wa shule na wakufunzi wa vyuo vya ualimu na maendeleo ya jamii.
Madai makubwa ya walimu na chama chao CWT pamoja na kudai ongezeko la mishahara kwa asilimia 100, posho ya kufundishia kwa walimu wa Sayansi asilimia 55, posho ya kufundishia asilimia 50 kwa walimu wa masomo ya  sanaa na posho kwa  walimu wanaoishi katika mazingira magumu.
Ikumbukwe kuwa madai ya walimu ya aina hii na mengine yamedumu kwa zaidi ya muongoz mzima bila kupatiwa dawa. Serikali imekuwa imekuwa ikitoa ahadi nyingi sana za kukamilisha madai na stahiki za walimu bila kutekeleza kwa dhati.
Pamoja na kuwa CUF- Chama Cha Wananchi hakiamini migomo ya wafanyakazi kama suluhisho la kuisha kwa matatizo yao na bila kuingilia maamuzi ya mahakama tunasisitiza kuwa walimu wana madai sahihi, ya haki na yanayopaswa kutekelezwa haraka sana.
Sote ni mashahidi kuwa hali za walimu ni mbaya sana, wanalipwa mishahara kiduchu, wanalipwa posho ndogo ambazo hugeuzwa na kuwa malimbikizo, wanaishi katika nyumba mbovu na wengi wao wamepanga mitaani katika makazi dhaifu, wanafundisha wanafunzi wengi na katika mazingira magumu, walimu ndiyo wamekuwa sehemu ya CCM kujifunzia utawala. CUF Chama cha Wananchi kinawapongeza sana walimu wa Tanzania kwa kazi kubwa wanayoifanya japokuwa hii inayojiita serikali SIKIVU haikuwahi kusikiliza madai yao zaidi ya kutishia kuwafukuza kazi, kuwakamata, kuwashtaki n.k. kama ilivyotokea kwa baadi ya maeneo katika mgomo uliokuwa umeanza mwezi huu kabla mahakama haijangilia kati na kuubatilisha.

Mwajiri wa walimu ni rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, chama chetu kilidhani kuwa, rais angelikuja na kauli mahsusi na mpango maalum unaokidhi matatizo yanayowakumba walimu yakiwemo madai ya mambo ya msingi. Badala yake, Rais kikwete akilihutubia taifa kupitia kwa wahariri wa vyombo vya habari katika hotuba yake ya ya mwisho wa mwezi Julai aliyoitoa tarehe 01 Agosti 2012 Ikulu jijini Dar Es Salaam anasema “Madai ya safari hii ni makubwa mno, yametuzidi kimo.  Athari za kuyatimiza yalivyo yataifanya bajeti ya Serikali kutumia asilimia 75 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Serikali na kubakiza asilimia 25 kwa kuendeshea Serikali na kutimiza majukumu ya maendeleo kwa wananchi.  Haitakuwa sawa.  Ndiyo maana tumeshindwa kuelewana walipokataa rai hiyo na wao kusisitiza kugoma.”

Rais anaendelea tena, “Wakati tunaendelea kusubiri uamuzi wa Mahakama, nina maombi mawili kwa walimu:  Moja, wasiwalazimishe walimu wasiotaka kugoma wafanye hivyo, wawaache waendelee na kazi.  Pili,wasitumie watoto isivyostahili kujenga hoja zao.  Nawasihi warudi kwenye meza ya mazungumzo.”
Ukitizama nukuu hizo, zinathibitisha danadana ya serikali ya CCM katika kutekeleza madai ya walimu. Rais hataji serikali yake ina mipango gani na kwa kiasi gani itatekeleza mipango hiyo. Serikali isiyo na mipango kwa vyovyote vile haiwezi kuwatumikia wakulima na wafanyakazi wa nchi yetu. Ni aibu kubwa kwa serikali kuwahadaa walimu kwa mambo yaliyo wazi kabisa.
CUF – Chama Cha Wananchi tunaamini kuwa, kuna fursa nyingi ambazo nchi yetu inazo na ingeweza kuzitumia na kumaliza madai ya walimu na wafanyakazi wengine, likiwapo hili dai kuu la kuongezewa mishahara. Kwa kweli elimu ya Tanzania itaendelea kuwa duni mno ikiwa mchezo huu wa kuwapiga danadana walimu utaendelea. Vigogo wa CCM ambao watoto wao wanasoma katika shule za kimataifa na za kimombo , katu hawawezi kuwafikiria watoto wa masikini wasio na mbele wala nyuma.
Katika utaratibu wa ulipaji mishahara serikalini, TGS A hadi C ni kiwango cha mishahara kwa watumishi wa serikali wanaoanza kazi bila kuwa na shahada ambapo hapa kuna kundi kubwa sana la walimu wa shule za msingi hadi sekondari kwa maana ya wanaofundisha kidato cha 1 hadi cha 4.
Uchambuzi huu hapa chini, unaonesha viwango vya mishahara serikalini kwa mwaka 2011/2012 kwa baadhi ya sekta muhimu ikiwemo elimu, viwango hivi havijahusisha makato ya kodi mbalimbali, ukifanya makato mfanyakazi na hasa mwalimu anabakia na pesa ya kununulia matunda tu.
SEKTA VS TAALUMA CHETI DIPLOMA SHAHADA
UALIMU/ELIMU 244,400 325,700 469,200
AFYA 472,000 682,000 792,200
SHERIA 630,000 871,500 1,000,000

Unaweza kujiuliza, kwa nini leo kuna tofauti kubwa sana ya mishahara kati ya sekta moja muhimu ya huduma na nyingine muhimu. Mambo haya yangeshatatuliwa iwapo serikali ya CCM ingekuwa inasema ukweli na kutekeleza ahadi zake. Kwenye ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010 – 2015, Rais Kikwete  na CCM wanaahidi kuwa; “Serikali kuanzisha mchakato utakaohakikisha kwamba pamoja na kuthamini mchango wa kila mfanyakazi na kufanya kazi katika taaluma zao na kuziheshimu ni muhimu ione tofauti kubwa iliyopo kati ya malipo ya wafanyakazi wa ngazi za juu na wale wa ngazi za chini”.

Leo utawala wa Kikwete unaende kumalizika na tofauti ya mishahara bado ni kubwa mno kati ya walimu na kada zingine za wafanyakazi huku Rais akiendelea kuwabembeleza walimu kwa lugha tamu ati serikali yake inawajali.
Kama tunaendelea kuwalipa walimu namna hii, ina maaana ualimu ni wito tu na siyo taaluma kama zilivyo taaluma zingine muhimu, vinginevyo tusishangae kuwa walimu wetu watakuwa mstari wa mbele kuuza bagia na vitumbua shuleni badala ya kufundisha kwa sababu fedha hizo hazilingani kabisa na hali halisi ya maisha.
Ikiwa mwalimu mwenye familia ya watoto wanne mke na wazee wake vikongwe wanamtegemea na ana shahada moja, ukimlipa 469,200 kwa mwezi ina maana kuwa kila mtegemezi asiyeepukika wa mwalimu huyu atatumia tzs 58,625 kwa mwezi na kwa siku kila mwanafamilia atatumia shilingi 1954.16.
Ikiwa tunawafikisha walimu wetu hapo ina maana kuwa hawataweza kujihudumia kimatibabu, kimakazi na huduma zote muhimu hawatazipata, watahudumia matumbo yao tu wakati wote wa kufundisha na watastaafu wakiwa masikini hohehahe, lazima serikali ichukue hatua haraka.
Ni vyema pia mawasiliano kati ya wizara ya elimu na walimu yakaimarishwa ili kujenga mazingira ya wazi ya majadiliano. Mawasiliano yakiimarishwa kati ya wadai na mdaiwa hakuwezi kutokea migomo. Migomo ni uthibitisho wa kuwepo usiri, uzembe, dharau au ubabe. Inasikitisha kwamba mvutano kati ya serikali na walimu hauonyeshi mazingira ya kuaminiana katika kutatua mgogoro husika.
Kukua kwa uchumi wa kisasa wenye uwezo wa kuboresha maisha ya wananchi kunategemea wafanyakazi wenye ujuzi na maarifa. Kwa hakika utafiti unaonyesha kuwa kukua kwa uchumi wa taifa lolote kunashabihiana kwa karibu na kiwango cha kuwekeza katika sekta ya elimu. Na huwezi kuwekeza katika elimu ikiwa huwalipi walimu kama inavyostahili.
Katika kutilia mkazo elimu ndani ya nchi CUF – Chama Cha Wananchi katika ILANI YA UCHAGUZI YA MWAKA 2010tumesisitiza kuwaSerikali ya CUF itaongeza mishahara ya walimu (katika ngazi zote) ili kukidhi mahitaji yao muhimu. Suala la makazi bora ya mwalimu litakuwa ni jukumu la msingi kabisa la serikali ya CUF ambalo litaanzisha mradi mkubwa wa ujenzi wa nyumba za walimu utakaosimamiwa na Serikali kwa haraka ndani ya miaka mitano ya kwanza ya uongozi wa nchi”.
Pamoja na hali mbaya ya kiuchumi waliyonayo walimu huku wanaendelea kupata mishahara midogo mno, CCM katika ilani zake za uchaguzi imeendelea kujisifia kwa eti kusimamia elimu kwa uhakika bila kukumbuka kuwa kusimamia mfumo wa elimu ni pamoja na kuwalipa walimu vizuri, ilani ya CCM 2005 – 2010 inajisifia “Mfano mzuri unajitokeza katika sekta ya elimu. Pamoja na mafanikio mengine katika sekta hii, idadi ya wanafunzi wa shule za msingi imeongezeka kutoka milioni tatu na nusu mwaka 1995 na kufikia zaidi ya milioni saba na nusu mwaka 2005. Wakati huo huo wanafunzi wa shule za sekondari wameongezeka zaidi ya maradufu kutoka wanafunzi 190,000 mwaka 1995 hadi wanafunzi 520,000 mwaka wa 2005”
CCM wanasifia idadi ya ongezeko la wanafunzi bila kusema ongezeko hilo litashughulikiwa na walimu wangapi na wao kama serikali wataboreshaje maslahi muhimu ya walimu, huu ni udahifu mkubwa sana.

Bila kujua nini wamekifanya katika elimu katika ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 – 2015 wanasema, “Katika kipindi cha 2010-2015, CCM itaendelea kuwa karibu na wafanyakazi na kuhakikisha kuwa Serikali zinayatambua na kuyashughulikia kwa ukamilifu na kwa wakati muafaka matatizo yao”.

Huu ni mfano mdogo wa ulaghai wa CCM, kwenye ilani ya kutafuta madaraka ya dola wanaahidi kuyatambua na kuyashughulikia madai na matatizo ya wafanyakazi, tena wanasema “tutayashughulikia kikamilifu” lakini leo kero na matatizo ya wafanyakazi vinaonekana kama mzigo mkubwa kwa serikali na inatamka hadharani kuwa “madai ya walimu hayatekelezeki”. CUF – Chama Cha Wananchi tunawashauri walimu watambue kuwa CCM haipo madarakani kutatua matatizo yao, muhimu walimu wakaungana wote ili kuhakikisha CUF inaongoza dola na kuleta mabadiliko makubwa.

“Serikali kuanzisha mchakato utakaohakikisha kwamba pamoja na kuthamini mchango wa kila mfanyakazi na kufanya kazi katika taaluma zao na kuziheshimu ni muhimu ione tofauti kubwa iliyopo kati ya malipo ya wafanyakazi wa ngazi za juu na wale wa ngazi za chini”.

Migomo ni uthibitisho wa kuwepo usiri, uzembe, dharau au ubabe. Inasikitisha kwamba mvutano kati ya serikali na walimu hauonyeshi mazingira ya kuaminiana katika kutatua mgogoro husika.

Prof. Ibrahim Haruna Lipumba,
Mwenyekiti,
05 Agosti 2012, Dar Es Salaam.